read

Aya 75 – 78: Miongoni Mwao Wako Walio Mwahidi Mwenyezi Mungu

Maana

Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema. Lakini alipowapa katika fadhila zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza

Watu wa Tafsir wamesema kuwa Aya hii ilimshukia mtu mmoja katika Ansar anayeitwa Tha’lab bin Hatib. Alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw): Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniruzuku mali.

Mtume akamwambia: Ee Tha’laba! Kichache unachoweza kishukuria ni bora kuliko kingi usichokiweza. Kwani hupati kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi kwake! Lau ningelitaka jabali linigeukie dhabu na fedha, lingegeuka.

Lakini Tha’laba, hakukinai, akamnaga’ang’ania Mtume na kusema: Naapa kwa ambaye amekupa utume kwa haki! Kama Mungu akiniruzuku mali nitampa kila mwenye haki haki yake. Mtume akasema: Ewe Mola wangu! Mruzuku Tha’alaba mali.

Basi Tha’laba akawa na mbuzi wakazaana kama wadudu. Pakawa pale mjini, hapamtoshi, akahamia nje. Ikawa tena hawezi kuhudhuria Swala ya Jamaa wala ya Ijumaa.

Mtume akamtumia mtu akachuke zaka kwake, akakataa na kufanya ubakhili, akasema. Hii tena ni kama kodi. Mtume akasema: Ole wake Tha’laba. Ndipo zikashuka Aya hizo.

Iwe ni kweli Aya hizi zimeshuka kwa Tha’laba au kwa mwengine, lakini tukio hilo linabainisha kwa ufasaha sana makusudio ya Aya hizi. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 4 (3:143) kifungu cha: ‘Mabadiliko ya hulka na fikra’

Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kukutana nao

Katika Tafsir Albahrul Muhit kuna maelezo kuwa Hasan, Qatada na Abu Muslim, walisema kuwa dhamir ya ukawalipa inarudia kwenye ubakhili.

Pia kauli hiyo ameichagua Tabrasi na Maraghi. Yaani ubakhili umewalipia unafiki hautaachana nao mpaka siku ya kukutana na malipo ya ubakhili.

Mwenyezi Mungu ametaja sababu mbili za hayo:

1. Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi.

2. Kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

Sifa hizi mbili za kuhalifu ahadi na uwongo ni sifa mahsusi za wanafiki zilizoelezwa katika Hadith. Anasema Mtume Mtukufu (saw): “Alama za mnafiki ni tatu: Akizungumza husema uwongo na akiahidi huhalifu na akiaminiwa hufanya hiyana.”

Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong’ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu.

Siri ni ile iliyo moyoni, na mnong’ono ni maneno ya siri wanayoizungumza wawili au zaidi na ghaibu ni ile wasiyoijua viumbe wote. Maana ni kuwa vipi hawa wanafiki wanathubutu kuficha ukafiri na kuunong’ona? Hawajui kuwa Mwenyezi Mungu anajua yaliyo katika nyoyo zao na yanayozunguka katika ndimi zao, na kwamba halifichiki kwake lolote la kufichika katika ardhi na mbingu.?

الَّذِينَ يَلْمِزُونَ الْمُطَّوِّعِينَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ وَالَّذِينَ لَا يَجِدُونَ إِلَّا جُهْدَهُمْ فَيَسْخَرُونَ مِنْهُمْ ۙ سَخِرَ اللَّهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {79}

Wale wanaowabeza waumin wanaotoa sana sadaka na wale wasiopata ila juhudi yao, wakawafanyia maskhara; Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo.

اسْتَغْفِرْ لَهُمْ أَوْ لَا تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ إِنْ تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ سَبْعِينَ مَرَّةً فَلَنْ يَغْفِرَ اللَّهُ لَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ۗ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ {80}

Uwaombee msamaha au usiwombee, hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu wao wamememkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.