read

Aya 79 – 80: Wanaowabeza Wanaotoa Sadaka

Maana

Wale wanaowabeza waumin wanaotoa sana sadaka

Bado maneno yako kwa wanafiki. Aya mbili hizi tulizo nazo zinaonyesha aina nyingine ya dhambi zao na maudhi yao kwa Mtume na kwa waumin.

Wakati ambapo Mtume (saw) alihimiza kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na waumini wakamwitikia miongoni mwa sahaba zake; wakawa wengine wanajitolea maelfu na wengine pishi ya tende, kila mtu kwa uwezo wake, basi wanafiki wakawabeza wakamwambia aliyetoa kingi kuwa ni ria, na yule aliyetoa kichache kuwa anajikumbuka yeye tu.

Kawaida ya wanafiki ni kufanya ria kwa wanayoyasema na wanayoyafanya, kwa hiyo wanawakisia wengine vile walivyo wao. Kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

Na wale wasiopata ila juhudi yao, inaashiria mafukara waliotoa kichache, kwa vile ndio uwezo wao.

Wakawafanyia maskhara kwa kudharau kile walichokitoa.

Imam Ali (as) anasema: Usione haya kutoa kichache, kwani kuzuia ndio uchache zaidi.

Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo

Maana ya maskhara ya Muumbaji Mtukufu ni kwamba yeye atawalipa wafanyao maskhara kwa adhabu iumizayo.

Uwaombee msamaha au usiwombee, hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hatawasamehe.

Sabini ni fumbo la wingi. Bado waarabu wanafanya wingi kwa saba na sabini.

Kuna msemaji mmoja aliyesema kuwa Mwenyezi Mungu ameacha hiyari ya kuzindua kuwaombea msamaha wanafiki au kuacha kuwaombea.

Kwamba au katika Aya ni ya hiyari, kama anavyodai. Lakini huu ni mkanganyo, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu ‘hatawasamehe’ ni dalili mkataa kwamba hakuna njia ya kuwasamehe wala kuwaghufiria. Kwa hiyo ‘au’ katika Aya, ni ya usawa.

Kuna riwaya isemayo kuwa ilipo shuka Aya ‘wale wanaowabeza,’ wanafiki walimtaka Mtume awatakie msamaha, ndipo Mwenyezi Mungu akataremsha: ‘Uwaombe msamaha au usiwaombee ’
Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu anapenda wenye kutubia na huwaghufuria dhambi zao vyoyvote zitakvyokuwa kubwa. Sasa kuna siri gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hatawasamehe?’ Mwenyezi Mungu (swt) amelijibu swali hili pale aliposema:

Hayo ni kwa sababu wao wamemekufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki

Wao walitaka udhuru na wakamtaka Mtume awaombe msamaha, lakini ni kwa unafiki na ria. Ama katika hali yao halisi wao wanaendelea na ukafiri na inadi. Anaowatakabalia Mwenyezi Mungu ni wanaogopa tu, sio wanafiki ambao wanasema wasiyoyafanya.

فَرِحَ الْمُخَلَّفُونَ بِمَقْعَدِهِمْ خِلَافَ رَسُولِ اللَّهِ وَكَرِهُوا أَنْ يُجَاهِدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَقَالُوا لَا تَنْفِرُوا فِي الْحَرِّ ۗ قُلْ نَارُ جَهَنَّمَ أَشَدُّ حَرًّا ۚ لَوْ كَانُوا يَفْقَهُونَ {81}

Walifurahi walioachwa nyuma kwa sababu ya kubakia nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na walichukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wakasema: Msiende katika joto. Sema: Moto wa Jahanamu una joto zaidi lau wangelifahamu.

فَلْيَضْحَكُوا قَلِيلًا وَلْيَبْكُوا كَثِيرًا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {82}

Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

فَإِنْ رَجَعَكَ اللَّهُ إِلَىٰ طَائِفَةٍ مِنْهُمْ فَاسْتَأْذَنُوكَ لِلْخُرُوجِ فَقُلْ لَنْ تَخْرُجُوا مَعِيَ أَبَدًا وَلَنْ تُقَاتِلُوا مَعِيَ عَدُوًّا ۖ إِنَّكُمْ رَضِيتُمْ بِالْقُعُودِ أَوَّلَ مَرَّةٍ فَاقْعُدُوا مَعَ الْخَالِفِينَ {83}

Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kundi miongoni mwao. Na wakakutaka idhini ya kutoka. Sema: Hamtatoka pamoja nami milele, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Hakika nyinyi mliridhia kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na watakaobaki nyuma.