read

Aya 81 – 83: Walifurahi Walioachwa Nyuma

Maana

Walifurahi walioachwa nyuma kwa sababu ya kubakia nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na walichukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Amesimulia Mwenyezi Mungu (swt), katika Aya zilizotangulia, kauli ya baadhi ya wanafiki kwa Mtume kuwa waruhusiwe kukaa nyuma wasiende kupigana Jihadi. Katika Aya hii anatoa habari ya furaha yao kwa kukaa huko baada ya Mtume; wakachukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu; hasa katika vita vya Tabuk. Kwa sababu Aya ilishuka katika vita hivyo.

Wakasema: Msiende katika joto. Sema: Moto wa Jahanamu una joto zaidi lau wangelifahamu.

Walizihurumia nafsi zao kwa joto la dunia, lakini hawakujihurumia na moto wa Jahanamu ulio na joto zaidi na muda mrefu zaidi. Zaidi ya hayo ni kwamba mwenye kuacha Jihadi dhidhi ya Mataghuti amejivisha nguo ya udhalili duniani. Waarabu hawakupigwa vita ndani ya miji yao ila pale walipozembea na kujidhalilisha; wakaona ni heri wadhalilike kuliko kufa shahidi kulinda heshima yao.

Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Amri ya kucheka na kulia, maana yake ni kutoa habari kwamba wanafiki hata kama wakifurahi kukaa kwao nyuma na Jihadi, lakini furaha hii si chochote kuliganisha na hizaya na udhalili watakaokutana nao katika dunia na huko Akhera ni zaidi.

Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kundi miongoni mwao.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume. Maana ya kukurudisha ni kukurudisha kutoka vita vya Tabuk hadi Madina. Makusudio ya kundi ni wanafiki na miongoni mwao ni wale waliorudi nyuma kwenye vita vya Tabuk. Kwa sababu baadhi ya hawa walirudi kwa udhuru wa kweli.

Na wakakutaka idhini ya kutoka nawe kwenda kwenye vita au mahali pengine. Sema: Hamtatoka pamoja nami milele, wala hamtapigana na adui pamoja nami.

Walirudi nyuma ya Jihadi ya wajibu ndipo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa kuwanyima kusuhubiana na Mtume (saw) na kutoka naye kwenda vitani au kwengineko. Hii ni mojawapo ya adhabu iliyo kali kwenye nafsi kuliko kuchomwa mshale.

Yatakuja maelezo katika Aya 95. Kisha akabainisha Mwenyezi Mungu (swt) sababu ya kukataza kutoka pamoja na Mtume na kushirikiana nao katika kupigana na adui kwa kauli yake:

Hakika nyinyi mliridhia kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na watakaobaki nyuma.

Walibaki nyuma ya Mtume wakati wa shida, basi hawawezi kukubaliwa baada ya hapo. Na yeyote anayejichagulia utwevu, Mwenyezi Mungu humwacha na alilochagua. Makusudio ya walio baki nyuma ni watoto, vikongwe na wanawake.

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِنْهُمْ مَاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ {84}

Wala usimswalie kamwe yeyote miongoni mwao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafa wakiwa ni mafasiki.

وَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَأَوْلَادُهُمْ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ أَنْ يُعَذِّبَهُمْ بِهَا فِي الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنْفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ {85}

Wala zisikushangaze mali zao na watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwadhibu kwa hayo katika dunia na zitoke nyoyo zao wakiwa ni makafiri.

وَإِذَا أُنْزِلَتْ سُورَةٌ أَنْ آمِنُوا بِاللَّهِ وَجَاهِدُوا مَعَ رَسُولِهِ اسْتَأْذَنَكَ أُولُو الطَّوْلِ مِنْهُمْ وَقَالُوا ذَرْنَا نَكُنْ مَعَ الْقَاعِدِينَ {86}

Na inapoteremeshwa sura kuwa mwaminini Mwenyezi Mungu na piganeni jihadi pamoja na Mtume wake, wanakutaka idhini, wale wenye nguvu miongoni mwao, na husema: Tuache tuwe pamoja na wanaokaa.

رَضُوا بِأَنْ يَكُونُوا مَعَ الْخَوَالِفِ وَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ {87}

Wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma, Na nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa hiyo hawafahamu.

لَٰكِنِ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ جَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ ۚ وَأُولَٰئِكَ لَهُمُ الْخَيْرَاتُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ {88}

Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye walipigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na hao ndio wenye heri; na hao ndio wenye kufaulu.

أَعَدَّ اللَّهُ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ {89}

Mwenyezi Mungu amewaan- dalia Bustan (pepo) zipitazo mito chini yake, hali ya kudu- mu humo; huko ndiko kufuzu kukubwa.