read

Aya 84 – 89: Usimswalie Yeyote Miongoni Mwao

Swala Ya Maiti Mnafiki Na Fasiki

Wala usimswalie kamwe yeyote miongoni mwao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafa wakiwa ni mafasiki.

Maneno anaambiwa Mtume, na makusudio ya miongoni mwao ni wanafiki.

Iilikuwa ni desturi ya Mtume afapo mmoja wa maswahaba zake kumswalia na kusimama makaburini mwake akimwombea msamaha na kuwaambia waliohudhuria muombeeni msamaha mwenzenu na uthabiti, kwa sababu yeye hivi sasa anaulizwa.

Baada ya kushuka Aya hii Mtume (saw) alijizuia kuwaswalia wanafiki na kusimama kwenye kaburi zao kuwaombea dua. kwa sababu Aya iko wazi katika kulikataza hilo.

Ama sababu ya katazo hili ni kule kung’angania kwao kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuendelea hivyo hivyo kung’ang’a- nia ukafiri wao ambao umeelezewa na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: ‘Na wakafa wakiwa ni mafasiki.’

Haya ndiyo maana ya dhahiri ya Aya, na yanaambatana nayo masuala haya yafuatayo:

1. Mnaafiki ni fungu katika mafungu ya makafiri, bali yeye hali yake ni mbaya kuliko huyo. Kwa sababu anaficha ukafiri na kudhihirisha Uislamu. Ni kwa ajili hii imekuwa haramu kuswalia jeneza lake. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Wala usimswalie kamwe yeyote katika wao,’ zimeliweka wazi hilo. Iliyoweka wazi zaidi ni ile kauli yake iliyo katika Aya 114 ya sura hii.

Ama fasiki ni katika waislamu kwa sababu yeye anamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume kwa dhahiri na batini, lakini yeye anamwasi Mwenyezi Mungu katika hukumu zake. Kwa hiyo ni wajibu kumswalia, haifai kuacha.

Siku moja alinijia ulama kutoka Jabal Amil, tukawa na mazungumzo na majibizano haya:-

Alisema: Nimeitwa kumswalia maiti ninayemjua kuwa ni fasiki, je, itafaa nimswalie?
Nikasema: Bali ni wajibu kifaya kwako, Akasema: Na ufasiki je?
Nikamsomea kauli ya Imam Jaffer Assadiq (as): “Mswalie aliyekufa kati- ka waislamu na hisabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu.”

Akasema: Lakini mwenye kuswali ni lazima amwombee dua baada ya Takbira ya nne, na imezoeleka kumwombea kwa kusema: “Ewe Mola wangu sisi hatujui kwake isipokuwa heri.” Ikiwa nitasema si nitakuwa mwongo.
Nikwambia: Sema Ewe Mola wangu sisi tunajua kwake heri, ukusudie Uislamu.

2. Wamehitalifiana wafasiri kwa kutafutiana Riwaya kuwa je, Mtume (saw) aliswalia jeneza la kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya?

Kuna kauli tatu katika hilo: Kwanza, kwamba yeye alimswalia kwa kutu- maini kupata waislamu wengi, lakini hiyo ni dhana tu ambayo haifai kuithibitishia au kuifasiria chochote katika vitendo vya Maasum. Ya pili, kwamba hakumswalia.Alitaka kumswalia lakini Jibril akamshika nguo na akamsomea Aya hii. Ya tatu, kwamba yeye hakumswalia. Kuna maelezo katika Majmaul Bayan: “Riwaya nyingi zinasema kuwa yeye hakum- swalia.”

Bora ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni maelezo yaliyo katika Tafsiri ya Sheikh Maraghi juu ya kutosihi hadith iliyopokewa na Bukhari na wengineo kuwa mtume alimswalia bin Ubayya, na alipoulizwa, akasema: Mwenyezi Mungu amenihiyarisha kuwaswalia wanafiki, kwa vile yeye amesema: Uwaombee msamaha au usiwaombee.

Kisha akaongezea Maraghi, kwamba maulama wengi wame hukumu kutosihi hadith hii. Kwa sababu Aya ya kukataza kuwaswalia wanafiki ilishuka kabla ya kufa bin Ubaya na ni muhali kwa Mtume Mtukufu (saw) kuhalifu Kitab cha Mwenyezi Mungu. Vile vile ni muhali kusema kuwa Mwenyezi Mungu amenihiyarisha, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu hatawasamehe ni dalili mkataa kwamba au hapa si hiyari. Kwa hiyo hadith hiyo yenyewe inajifahamisha kuwa ni uwongo na uzushi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

3. Tabrasi katika Majamaul Bayan anasema: “Katika Aya hii kuna dalili kwamba kusimama kaburini kuomba dua na ibada iliyowekewa sharia.”

Hakuna faqih yoyote anayepinga kuwa kuwaombea Mungu maiti kunajuzu kisharia sawa na kuwaombea Mungu waliohai, bali kuna haja zaidi kwa waliokufa, maadamu tunaitakidi ufufuo, hisabu na adhabu; wala hakuna tofauti baina ya kuwa dua ni kaburini au pengine.

Ama kuzuru makaburi mafakihi wote wamegongana kuwa inajuzu isipokuwa Maimamu wa Kiwahabi. Sunni wamepokea, katika vitabu vitatu vya Sahih yao, Hadith inayoeeleza waziwazi kujuzu hilo; kama vile Hadith isemayo. “Alizuru Mtume kaburi la mama yake na akasema; Nimemtaka idhini Mola wangu kuzuru kaburi la mama yangu na akanipa idhini, basi yazuru makaburi, kwani yanakumbusha mauti”.

Sahih Muslim sehemu ya pili J1 mlango wa kutaka idhini Mtume (saw) kazuru kaburi la mama yake.

Amesema Ibn Hajar al-Asqalani katika Kitab Fathul-Bar Sharhil-Bukhar J3 Mlango wa Ziyara ya Makaburi: “Ametoa Muslim kutoka kwa Mtume (saw) kwamba yeye amesema: Nilikuwa ni kiwakataza kuzuru makaburi, sasa ya zuruni”.

Amezidisha Abu Daud na Nisai, wakiwa ni miongoni mwa wenye sahih, kuwa aliendelea kusema: “…Kwani yanakumbusha Akhera.” Hakim naye akazidisha: “… hulainisha moyo na huliza macho basi msiseme ni mahame…”

Hayo tumeyazungumzia katika Kitab Hadhihi hiyal wahabiyya (Huu ndio uwahabi), kisha tukaweka mlango maalum kwa anuani ya ziyara ya makaburi. Ama hisabu ya makaburi tumeizungumzia kwa ufafanuzi katika Juz. 3 (2:259) . Tunaweza huyarudia maudhui haya ikihitajika.

Wala zisikushangaze mali zao na watoto wao. Hakika tu Mwenyezi Mungu anataka kuwadhibu kwa hayo katika dunia na zitoke nyoyo zao wakiwa ni makafiri.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya 55 ya Sura hii. Wafasiri wamesema kuwa amerudia Mwenyezi Mungu kwa kusisitiza hadhari ya kuishangaa mali na watoto na kujishughulisha zaidi nao. Lakini tumesema mara nyingi kuwa kukaririka, katika Qur’an, ni jambo la kawaida.

Na inapoteremeshwa sura kuwa mwaminini Mwenyezi Mungu na piganeni jihadi pamoja na Mtume wake, wanakutaka idhini, wale wenye nguvu miongoni mwao, na husema: Tuache tuwe pamoja na wanaokaa.

Wenye nguvu hapa ni wale wenye nguvu na utajiri, nao ni wale mataghuti wapenda anasa ambao wanajiepusha na kila linalogusa masilahi yao kwa mbali au karibu. Na, kumwamini Mwenyezi Mungu maana yake ni kuwa sawa na watu wengine, kupigana jihadi maana yake ni kuwa dhidi ya dhulma na ufisadi; yaani kuwa dhidi yao.

Ikiwa kumwamini Mwenyezi Mungu na kupigana jihadi kunapinga masilahi yao, basi wao ni wa vita wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Lakini sasa wana tatizo, kuwa watakataa vipi na hali wao wanandai kuamini utume wake? Mwisho wakapata ufumbuzi – kutaka idhini ya kukaa. Lakini idhini hii imewafedhehesha na kufichua kufuru yao na unafiki wao na kwamba wao wanajificha kwa jina la Uislam wakihofia nafsi zao.

Wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma, ambao ni vikongwe, watoto na wanawake.

Hilo linatosha kuwa ni utwevu.

Na nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa hiyo hawafahamu malengo mengine na tamaa zimepofusha nyoyo zao na haki na kuwazuia kuifuata haki.

Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye walipigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao.

Yaani, ikiwa wanafiki watabaki nyuma, basi wako waumini wenye ikhlasi waliosimama na Mtume. Huo ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu katika Juz.6 (6:89)

Na hao ndio wenye heri; na hao ndio wenye kufaulu

Heri na kufaulu duniani na akhera ni natija ya kuwamini Mwenyezi Mungu na kupigana jihadi katika njia ya haki na uadilifu. Wale haihusiki heri na faida kimaada tu, bali ni maada na maana. La kushangaza ni kauli ya mfasiri mmoja anayesema kuwa makusudio ya heri hapa ni Hurilaini. Inaonekana anaelezea jambo analolipenda zaidi.

Mwenyezi Mungu amewaandalia Bustan (pepo) zipitazo mito chini yake, hali ya kudumu humo; huko ndiko kufuzu kukubwa.

Umetangulia mfano wake katika Aya 82 ya Sura hii na Juz. 2 (3:25)

وَجَاءَ الْمُعَذِّرُونَ مِنَ الْأَعْرَابِ لِيُؤْذَنَ لَهُمْ وَقَعَدَ الَّذِينَ كَذَبُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ ۚ سَيُصِيبُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {90}

Na walikuja wenye kutoa udhuru katika mabedui ili wapewe idhini. Na wakakaa wale waliomwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Itawafika wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

لَيْسَ عَلَى الضُّعَفَاءِ وَلَا عَلَى الْمَرْضَىٰ وَلَا عَلَى الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ مَا يُنْفِقُونَ حَرَجٌ إِذَا نَصَحُوا لِلَّهِ وَرَسُولِهِ ۚ مَا عَلَى الْمُحْسِنِينَ مِنْ سَبِيلٍ ۚ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {91}

Hapana lawama juu ya waliodhaifu, wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutumia, wakimsafia nia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakuna njia (ya kuwalaumu) wanaofanya wema; na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa msamaha mwenye kurehemu.

وَلَا عَلَى الَّذِينَ إِذَا مَا أَتَوْكَ لِتَحْمِلَهُمْ قُلْتَ لَا أَجِدُ مَا أَحْمِلُكُمْ عَلَيْهِ تَوَلَّوْا وَأَعْيُنُهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ حَزَنًا أَلَّا يَجِدُوا مَا يُنْفِقُونَ {92}

Wala (si lawama) juu ya wale waliokujia ili uwachukua ukasema: Sina cha kuwachukukulia; wakarudi hali macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kutopata cha kutumia.

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ وَهُمْ أَغْنِيَاءُ ۚ رَضُوا بِأَنْ يَكُونُوا مَعَ الْخَوَالِفِ وَطَبَعَ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {93}

Njia (ya kulaumu) iko tu juu ya wale wanaokuomba ruhusa hali wao ni matajiri, wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma. Na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao; kwa hivyo hawajui.