read

Aya 9-15: Wanaziuza Aya Za Mwenyezi Mungu

Maana

Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

Dhamir inawarudia washirikina ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha wauawe. Maana ni kuwa hawa wameupinga Uislam wakaupiga vita na kuzuilia watu nao, kwa kuhofia masilahi yao waliyoathirika nayo kuliko ishara za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake uliowajia.

Aya hii sio kama inahusika na washirikina na watu wa Kitab tu, bali inawakusanya ambao wanaiharibu dini kwa ajili ya kuafiki matakwa ya wakoloni na wanyonyaji.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 4 (3:187).

Hawaangalii kwa Mumin ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

Utauliza kuwa Aya hii ni mfano wa Aya iliyotangulia (ya nane) kwa nini imerudiwa?
Jibu: Mwenyezi Mungu (swt), katika Aya iliyotangulia, alikuwa akiwambia maswahaba wa Mtume (saw) na kuwa lau washirikina watawashinda basi watafanya maajabu. Huenda hapo mtu akadhania kwamba washirikina wanadhamiria chuki na uadui kwa Mtume (saw) na maswahaba tu.

Ndipo Mwenyezi Mungu (swt) akaondoa dhana hii kwamba uadui wa washirikina, kwa waislamu wakati huo ni uadui wa msingi wenyewe, sio uadui wa watu; ni uadui wa kufuru kwa imani na batili kwa haki:

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَنْ يُؤْمِنُوا بِاللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ {8}

“Nao hawakuwachukia ila ni kwa vile wamemwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu mwenye kusifiwa”. (85:8)

Kama wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua.

Aya hii inaafikiana na Aya ya tano katika sharti (wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka), lakini inatofautiana katika jawabu la sharti. Jawabu katika Aya iliyotangulia ni kuwachia njia na mambo yao na kutowataaradhi na chochote. Jawabu katika Aya hii ni kuwa ni ndugu zenu, yaani nyinyi na wao mkeo sawa katika haki, hakuna bwana wala mtumwa; mwenye kula au kuliwa; kama ilivyokuwa hali ya washirikina.

Kwa kutofautiana huko katika jawabu la sharti, kunafutika kukaririka, ingawaje kukaririka katika Qur’an sio jambo la nadra.

Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo (vya maana). Ili wapate kukoma.

Mwenyezi Mungu (swt) ameleta ibara ya kupigana na makafiri kwa kusema ‘piganeni na viongozi wa makafiri,’ kwa vile wao ndio wanaowaon- goza kwenye vita na kuvunja ahadi, na wanatukana na kuwahimiza wafuasi wao wamtukane Mtume (saw) na Qur’an.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ili wapate kukoma,’ inaashiria makusudio ya kupigana. - Kuwazuia washirikina wasiendelee kupigana na waislam.

Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza?

Maneno yanaelekezwa kwa waislamu na dhamir inawarudia makafiri wa Kiquraish, kwa sababu wao ndio waliomwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu kuacha kupigana miaka kumi, kuishi kwa amani makundi yote mawili na walioungana nao.

Hapo ilikuwa ni mwaka wa sita wa Hijra. Lakini hawakudumu na mkataba huo. Vile vile wao ndio waliodhamiria kumuua Mtume (saw) mpaka akalazimika kuhama na ndio wao walioanza kupigana siku ya Badr.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kuwakumbusha waislam walivyofanya washirikina kuvunja ahadi na kumtoa Mtume na kuanza vita, aliwahimiza jihadi na kupigana, ambapo hakuna njia nyingine isiyokuwa hiyo.

Kisha Mwenyezi Mungu (swt) akawaondolea hofu waumini kwa kusema:

Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini, inaashiria kwamba kumwogopa Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa, hakuwi wala haku-takuwa ila kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa.

Ama mwenginewe, hamwogopi Mwenyezi Mungu hasa, ispkokuwa kumwogopa kwake ni kama njozi tu zinazopita.

Imam Ali anasema: “Kila hofu ina uthibitisho, isipokuwa kumhofia Mwenyezi Mungu, huko kuna ila”. Yaani Mtu kumwogopa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni jambo la uhakika, lakini kumhofia Mwenyezi Mungu hakuwi na uhakika halisi, isipokuwa ni njozi tu zinazoondoka kwa kitu kidogo.

Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin na aondoe hasira ya nyoyo zao.

Sifa hizi zinanasibiana na ushindi wa kuiteka Makka. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwadhalilisha na kuwafedhehesha vigogo vya Maqureish na kuwapa ushindi waislamu na kuvipoza vifua vya waumini ambao walikandamizwa na waonevu wa Kiqureish kabla ya Hijra, na kuwepo aina kwa aina ya mateso.

Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

Makka ulikuwa ndio makao makuu ya nchi ya Hijaz na kituo cha harakati zote katika Bara Arabu. Wakuu wake walikuwa wakimchomolea upanga wa dhulma na utisho kila mwenye kutaka kujiunga na Mtume Muhamad (saw).

Baada ya kutekwa, Makka ilikuwa chini ya kivuli cha Uislamu na wakasilimu wale mataghuti. Hata hivyo baadhi yao walisilimu kwa kupenda sio kwa kuhofia. Wakasilimu kidhati na kindani. Hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu amewakubalia toba na atawalipa kwa ikhlasi yao na ukweli wa nia yao.

Baada ya hayo, hakika kila hukumu iliyofungamana na Aya hizi inahusika na washirikina wa Kiarabu wakati huo. Kwa sababu wao ndio waliomtoa Mtume (saw), wakampiga vita na wakaacha kuheshimu mkataba.

Lakini kwa kukadiria kwamba Aya hizo zinawajibisha jihadi dhidi ya washirikina kila mahali na kila wakati, basi jihadi hiyo haijuzu ila kwa uongozi wa dola ya Kiislamu kwa kuongozwa na Maasum au naibu wake.

Yuko wapi huyo hivi sasa? Amedai hayo mwenye kudai, akaanzisha chama kwa ajili kwa uongozi wake, kisha akabainika kuwa ni kibaraka, wakamuepuka wale aliowahadaa waliokuwa wameghafilika na wala hajulikani alipo mpaka sasa.

Hata hivyo, jihadi ya mtu kulinda uhuru wake, mali yake na nchi yake haingoji kupatikana dola ya Kiislam wala haihitaji idhini ya maasum au asiyekuwa maasum.

Kwa sababu kulinda nafsi na nchi na kuwapiga wakoloni wanyonaji ni haki inayotukuzwa na sharia zote na kanuni zote. Tumeyaeleza katika kufasiri Juz.1 (2:19-193) Juz.4 (3:95) na katika Juzuu hii tuliyonayo sura (8:47)

أَمْ حَسِبْتُمْ أَنْ تُتْرَكُوا وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنْكُمْ وَلَمْ يَتَّخِذُوا مِنْ دُونِ اللَّهِ وَلَا رَسُولِهِ وَلَا الْمُؤْمِنِينَ وَلِيجَةً ۚ وَاللَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ {16}

Je, mnadhani kuwa mtaachwa na hali Mwenyezi Mungu hajawabainisha wale wanaopigana jihadi miongoni mwenu, na hawakumfanya mwandani asiyekuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumin? Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyafanya.

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَنْ يَعْمُرُوا مَسَاجِدَ اللَّهِ شَاهِدِينَ عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ ۚ أُولَٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ {17}

Haiwi kwa washirikina kuamirisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali wanajishuhudia wenyewe ukafiri. Hao vitendo vyao vimeporomoka. Nawatadumu katika moto .

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّهَ ۖ فَعَسَىٰ أُولَٰئِكَ أَنْ يَكُونُوا مِنَ الْمُهْتَدِينَ {18}

Wanaoamirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale tu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakasimamisha swala na wakatoa zaka na wasiogope ila Mwenyezi Mungu. Basi hao huenda wakawa miongoni mwa waliongoka