read

Aya 90-93: Walikuja Wenye Udhuru

Maana

Na walikuja wenye kutoa udhuru katika mabedui ili wapewe idhini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kubainisha hali za wanafiki ambao walikuwa Madina, hapa anawaelezea mabedui waliokaa nyuma ya jihadi na kwamba wao ni aina mbili:

Kwanza ni wale waliomwendea Mtume (saw), wakatoa udhuru na kutaka idhini ya kubaki nyuma. Aina hii ndiyo iliyokusudia na kauli hio ya Mwenyezi Mungu mtukufu: “Na walikuja wenye kutoa udhuru....”

Aina ya pili ni wale waliokaa wakiwa wanamwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao wameashiriwa na kauli isemayo:

Na wakakaa wale waliomwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Kuwagawanya wale waliobaki nyuma kwenye mafungu mawili, wenye udhuru na waongo, kunafahamisha kuwa makusudio ya wenye udhuru ni wale waliobaki nyuma kwa udhuru sahihi. Ndio maana Mwenyezi Mungu akawanyamazia wenye udhuru bila ya kuwatishia na adhabu iumizayo; kama alivyowatisha waongo kwa kauli yake:

Itawafika wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

Utauliza: Mfumo wa Aya unataka neno ‘miongoni mwao liondolewe,’ Kwa sababu wanaomuongopea Mwenyezi Mungu na Mtume wake wote ni makafiri, sio baadhi yao.

Razi amejibu kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa akijua kwamba baadhi yao wataamini na kuepuka adhabu, ndipo akataja neno miongoni, kufahaamisha baadhi.

Tuonavyo sisi ni kuwa wale waliokaa wakamdanganya Mwenyezi Mungu na Mtume wake wako aina mbili: Miongoni mwao wamo waliotoa udhuru wa uwongo kwa kutaka raha na kuepuka taabu ya jihadi, wakiwa wanamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa dhahiri na batini. Na hawa sio makafiri bali ni wapuuzaji.

Aina nyingine ni wlae waliotoa udhuru wakiwa wanakanusha utume wa Muhammad (saw) kwa ndani. Hawa ndio makafiri wanaostahiki kudumu katika adhabu. Ndipo likaja neno ‘miongoni mwao’ kufahmisha kuwa makafiri waliobaki nyuma kwa kupinga utume, kinyume cha wale waliobaki kwa kupuuza si kwa kukanusha.

Hapana lawama juu ya waliodhaifu, wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutumia.

Mtume (saw) alipiga mbiu ya jihadi wakajitokeza waliojitokeza na wengine wakabaki nyuma wakiwemo wanafiki, kama ilivyotangulia kuelezwa na yataaendelea kuelezwa. Vile vile walikuwemo wenye udhuru wa kiuhakika.

Hawa ndio ambao hawana dhambi wala lawama. Wao wako aina tatu:

1. Waliodhaifu wasioweza kupigana kwa uzee au wenye maumbile dhaifu wasioweza kupigana kwa hali yoyote.

2. Wagonjwa. Tofauti ya ugonjwa na udhaifu ni kuwa ugonjwa sio ila ya kimaumbile.

3. Mafukara ambao hawana posha wala mdhamini. Kwani kuweko watu wa hawa ndani ya wapiganaji kunawaletea matatizo ya kufikia lengo.

Mwenyezi Mungu (swt) amewahalalishia watu hawa watatu kubaki nyuma ya jihadi – wakimsafia nia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwa wenye ikhlasi katika imani yao wakisimamia majukumu yaliyobaki; kama vile kuulinda mji, kuchunga familia na mali za wapiganaji nk.

Hakuna njia (ya kulaumu) wanaofanya wema.
Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Kila mwenye kutekeleza wajibu wake wowote kwa ukamilifu, basi huyo ni mfanya wema, katika mtazamo wa Kiislamu. Na kila asiyetekeleza basi ni mwovu. Mwenyezi Mungu amewaondolea jihadi wagonjwa na mafukara, wakitekeleza wajibu mwingine basi hao ni wema, na haifai kwa yeyote kuwalaumu kwa njia yoyote.

Mafakihi wamechukua, kutokana na Aya hii, asili ya kisharia walionyumbua hukumu nyingi. Miongoni mwa hukumu hizo ni hizi zifuatazo:

Mtu akiweka amana mali yake kwa mtu mwingine na mali ile ikaharibika, basi hatalipa, ila ikiwa amezembea au kukusudia kuiharibu.

Hakimu wa Sharia, mwenye masharti kamili, akikosea katika hukumu, basi hakuna chochote kwake, ikiwa alifanya bidii kujua ukweli.

Ikiwa mtu anaona mali ya mwingine inataka kuangamia, akatumia sehemu ya mali ile ili kuukoa sehemu nyingine, basi hatalipa ile aliyoitumia au kuiharibu. Na mengineyo mfano wa hayo Kwa sababu wote hao wanafanya wema na: ‘Hakuna njia ya (kuwalaumu) wanaofanya wema.’

Wala si lawam juu ya wale waliokujia ili uwachukue, ukasema: Sina cha kuwachukulia; wakarudi hali macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kutopata cha kutumia.

Wameafikiana wapokezi wa Hadith na wafasiri kwamba Aya hii iliwashukia jamaa katika waislamu waliomjia Mtume (saw) akiwa anajiandaa kwa vita vya Tabuk; wakamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sisi hatuna chombo cha kusafiria pamoja nawe kwenda kwenye Jihadi. Wakamtaka Mtume (saw) awapatie kipando; Mtume akasema sina cha kuwapandishia; wakalia machozi kwa kutoweza kwenda kwenye jihadi na Mtume (saw).

Kisha wafasiri wakatofautiana kuhusu majina ya hawa na idadi yao; lakini hilo halina umuhimu wowote maadamu Aya iko wazi kufahamisha tukio hilo; na wala hakuna aliyelikanusha. Utauliza kuwa hawa wanaingia kaitka aina ya mafukara waliodokezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu wala juu ya wale wasiopata cha kutumia. Sasa je, kuna faida gani kurudia?

Baadhi ya wafasiri wamejibu kwamba mafukara hawakuwa na chakula wala cha kupanda, na hao waliolia walikuwa na chakula, lakini hawana cha kusafiria. Au huenda ikawa faida ni kutaja ukweli wa waliolia, ikhlasi yao na nafasi yao mbele ya Mwenyezi Mungu .

Vyovyote ilivyo ni kwamba Mwenyezi Mungu (swt) ameondoa jukumu kwa waliobaki nyuma kwa kushindwa; ni sawa iwe wameshindwa kwa maradhi, kukosa chakula au cha kupanda.

Njia (ya kulaumu) iko tu juu ya wale wanaokutaka idhini hali wao ni matajiri. wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma. Na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao; kwa hivyo hawajui.

Maana ya Aya hii inaafikiana na madhumuni ya Aya mbili zilizotangulia (86 na 87). Ufupi wa maana yaliyokusudiwa, ni kuwa Mwenyezi Mungu (swt) baada ya kuondoa majukumu kwa mafukara na wagonjwa, ameyathibitisha majukumu hayo kwa matajiri walio na afya ambao wanabaki nyuma ya jihadi.

Ni muhali kwa watu hawa kufanya kitu kwa maslahi ya uma na kusaidiana na wenye ikhlas katika jambo ambalo linagusa masilahi yao kwa mbali au karibu. Siku zote wao wako tayari kuiuza dini yao na nchi yao kwa mashetani ikiwa watawapatia faida.

Ndio hivyo, tangu zamani. Wanyonge wanapopambana kwa ujasiri kuondoa dhulma, kwa upande mwingine kunakuwa na matajiri wanaoongoza upinzani dhidi ya mapinduzi, kila wanapopata nafasi; vinginevyo wataficha vichwa vyao vyumbani wakingojea, kwa hamu, balaa liwafike wanapigana jihadi.