read

111 – 113: Aina Ya Watu Aya

Na lau kama tungewateremshia Malaika, na wafu wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu ana kwa ana, wasingeliamini ila atake Mwenyezi Mungu.

Tumesema katika Tafsir ya Aya iliyotangulia kuwa jamaa katika washirikina walimtaka Mtume (s.a.w.) awaletee muujiza maalum; na kwamba waumini walitamani lau Mwenyezi Mungu angeliitikia maombi yao; na Mwenyezi Mungu akawajibu waumini kwa kauli yake: “Na ni kitu gani kitakachowatambulisha ya kuwa zitakapowafikia hawataamini?”

Baada ya kuishiria yote hayo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amemfafanulia Mtume wake mtukufu, kwamba hawa washirikina ambao wamekutaka waliyoyataka katika miujiza, hawatakuamini kwa hali yoyote; hata kama tutawateremshia Malaika kutoka mbinguni, na tukawafufulia wafu wakashuhudia kwa lugha fasaha ya Kiarabu kuwa wewe ni Mtume, bali hata kama utakushuhudia ulimwengu ardhi yake na mbingu yake, wasingelikusadiki wala kukufuata ‘ila atake Mwenyezi Mungu;’ yaani Mwenyezi Mungu awalazimishe wakuamini wewe kwa nguvu.

Unaweza kuuliza: Je, kukadiria huku ni sawa? Na je aina hii ya watu inaweza kupatikana, katika hali ya kawaida? Itakuwaje kikundi kidogo kiukadhibishe ulimwengu na vilivyomo? Je, inawezekana mtu asiamini masikio yake na macho yake, kwa kuwaona wafu wanafufuka kutoka katika makaburi yaliyochakaa maelefu ya miaka na waseme. ‘Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu (na) Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu;’ wasikie wanyama na ndege na samaki na miti na nyota zote, zikinadi shahada mbili; inawezekana kweli aweko mtu atakayekadhibisha miujiza yote hii? Si ajabu hiyo?

Jibu: Kukadiria hivi si sawa, bali ni muhali kwa wale wanaoathirika na haki na dalili yake, na wanaokwenda pamoja na wahyi wa mantiki ya kiak- ili na umbile la Mwenyezi Mungu alilowaumbia watu. Kwa sababu miu- jiza hii ni dalili mkato isiyokuwa na shaka yoyote.

Ama kukadiria huku kwa watu ambao hisia zao zote zinatawaliwa na masilahi mahususi na kuyaona kuwa ndio akili, ndio umbile na ndiyo haki na uadilifu, basi ni sahihi. Kwa sababu aina hii ya watu ipo, nao ni wakoloni na walanguzi na wengineo mfano wao, ambao wanaishi kwa unyang’anyi na ufisadi.

Wale wanaoona ajabu kukadiria huku hawaitambui hali halisi ya kundi hili, na wamechanganya baina ya mantiki ya kiakili na ya yule mwenye kuongozwa na manufaa.

Akili kwa maana ya akili ni ile tu iliyo mwongozi, anayeamrisha na kukataza; wala haimsikilizi isipokua anayetafuta haki kwa njia ya haki. Ama chenye kuongoza na kuelekeza kwenye manufaa basi hicho ni manufaa ya kibinafsi.

Hicho peke yake ndicho kinachowaongoza katika mambo yao na silika zao. Ndiyo dini yao, ndiyo akili yao, bali ndiyo utu wao na uhai wao. Kwa sababu hiyo, hakuna mantiki yoyote yanayowafaa isipokuwa nguvu aliyoiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: ‘Ila atake Mwenyezi Mungu.’

Lakini wengi wao wamo ujingani

Hawajui kuwa wao ni kikundi kiovu ambacho hakifaliwi na mantiki ya kiakili na maumbile wala na mantiki ya dini na utu; wala kitu chochote ila nguvu na kushindwa. Ni makosa na ni kupoteza wakati kuzungumza na watu hawa kwa lugha ya elimu na ubinadamu.
Na kama hivyo tukamfanyia kila Nabii adui, mashetani watu na majini.

Shetani mtu ni maarufu, ni kila anayehadaa watu kwa kuwaingiza kwenye batili na kuwavisha nguo ya haki. Ama jinni yeye ni katika mambo ya ghaibu ya Mwenyezi Mungu. Nasi tunaamini kijumla na kimsingi; wala hautuhusu ufafanuzi; kwani hatutaulizwa kuhusu yeye; sawa na ilivyo katika Malaika. Wala si ajabu kwa Manabii kuwa na maadui. Kwa sababu, ni kawaida kuwe na uadui kati ya kheri na shari, na baina ya haki na batili.

Unaweza kuuliza: Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyewajaalia Manabii wawe na maadui, kama inavyoonyesha katika Aya, kwa nini basi awaadhibu kwa kuwafanyia uadui Mitume? Vilevile vipi ameamrisha kuwafuata Mitume kisha akawafanyia maadui watakaowapinga na kuwahadaa watu kuwapinga na kuupinga Utume wao?

Jibu: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewatuma Mitume na akafanya kazi yao ni kulingania Tawhid na uadilifu na kuondoa dhuluma na ushirikina.

Kazi hii, kwa tabia yake, huleta mgongano na vita baina ya Manabii na wale waabudu masanamu na wanyonyaji. Hivyo basi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni sababu ya kutumwa Manabii, na Manabii ni sababu ya uadui. Kwa kuzingatia haya umenasibishwa uadui kwake kimajazi. Anasema Mwenyezi Mungu akimsimulia Nuh (a.s.):

قَالَ رَبِّ إِنِّي دَعَوْتُ قَوْمِي لَيْلًا وَنَهَارًا {5}

فَلَمْ يَزِدْهُمْ دُعَائِي إِلَّا فِرَارًا {6}

“Ewe Mola wangu! Kwa hakika nimewalingania watu wangu usiku na mchana, lakini mwito wangu haukuwazidishia ila kukimbia.” (71: 5 6).

Kwa hiyo kukimbia kumenasibishiwa mwito wa Nuh (a.s.), na mwito wa Nuh (a.s.) ni amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa ufasaha zaidi tupige mfano huu: Mtu amemwachia mwanawe utajiri, na ule utajiri ukamsababishia uadui na husda. Basi kimajazi: “Mzazi wake ndiye aliyempa husda ile mwanawe!”

Baadhi yao wanawapa wenzao maneno ya kupambapamba kuwahadaa.

Maneno ya kupambapamba ni maneno yaliyochanganywa na uwongo. Dhahiri yake ni rehema na ndani yake ni adhabu. Maana ni kuwa waovu wanawatia wasiwasi wenzao kwa mambo ya batili yaliyochanganywa haki, kwa makusudio ya kuhadaa na kuipinga haki na watu wake.

Na kama Mola wako angelitaka wasingeliyafanya.

Dhamir ya wasingeliyafanya inarudia kwenye amali zao mbaya; yaani uadui kwa Mitume na kuambiana wao kwa wao maneno ya kupamba. Maana ni kuwa lau Mola wako angelitaka kuwazuia kwa nguvu kufanya ubaya wasingelikuwa na uadui huo wala kuambiana. Lakini hekima yake imepitisha kuwaacha kama walivyo, wawe na hiyari bila ya kuendeshwa, wapate kuhisabiwa waliyoyafanya na kuadhibiwa wanayostahiki.

Basi waache na wanayoyatunga katika uwongo.

Wajibu wako ni kufikisha na ni juu yetu kuhisabu na malipo.

Na ili zielekee hayo nyoyo za wale wasioamini akhera.

Yaani waovu wanaambiana kauli za kupambapamba ili wazisikilize makafiri na waridhie baada ya kuzisikiliza na wazitumie bila ya kufanya utafiti. Na ili wayachume wanayoyachuma katika maasi na madhambi; na apambanuke mumin na kafir na mwenye ikhlasi na mnafiki.

Kwa ufupi ni kuwa maiblis waovu wanapambapamba kauli ili wawahadae wenye nafsi dhaifu na wapondokee kwao na wachume dhambi.

Amesema Abu Hayani Al-andalusi: “Maneno haya yako katika upeo wa fasihi, kwani mwanzo inakuwa ni hadaa, inayofuatiwa na kupondokea, kisha kuridhia na kuchuma (dhambi); kama kwamba kila moja linasababishwa na lililo kabla yake.

أَفَغَيْرَ اللَّهِ أَبْتَغِي حَكَمًا وَهُوَ الَّذِي أَنْزَلَ إِلَيْكُمُ الْكِتَابَ مُفَصَّلًا ۚ وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْلَمُونَ أَنَّهُ مُنَزَّلٌ مِنْ رَبِّكَ بِالْحَقِّ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ {114}

Je, nimtafute hakimu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na hali yeye ndiye aliyewateremshia Kitab kinachofafanua. Na wale tuliowapa Kitab wanajua kwamba imeteremshwa na Mola wako kwa haki. Basi usiwe miongoni mwa wanaotia shaka.

وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ صِدْقًا وَعَدْلًا ۚ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ {115}

Na limetimia neno la Mola wako kwa ukweli na uadilifu. Hakuna wa kubadilisha neno lake. Na Yeye ni msikizi, mjuzi.

وَإِنْ تُطِعْ أَكْثَرَ مَنْ فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۚ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ {116}

Na kama ukiwatii wengi katika waliomo ardhini watakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana na hawakuwa ila wenye kuzua tu.

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ مَنْ يَضِلُّ عَنْ سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ {117}

Hakika Mola wako anawajua vyema wanaopotea njia yake na anawajua sana wanaoongoka.