read

Aya 11-18: Na Hakika Tuliwaumba

Asili Ya Mtu

Na hakika tuliwaumba, kisha tukawatia sura.

Maneno haya wanaambiwa wanaadamu. Maana ya ‘tuliwaumba’ ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliianzisha asili yetu ya kwanza kutokana na mchanga na sisi akatutoa kutokana na tone la manii ambalo linaishia kwenye mchanga. Makusudio ya tuliwatia sura ni kwamba yeye amejaalia mada ya kwanza aliyotuumba kwayo kuwa ni mtu kamili; kama alivyosema:

أَكَفَرْتَ بِالَّذِي خَلَقَكَ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ سَوَّاكَ رَجُلًا {37}

“Je, unamkufuru yule aliyekuumba kwa udongo, tena kwa tone la manii, kisha akakufanya mtu kamili?” (18:37)”

Kwa hiyo tofauti baina ya kuumba na kutia sura ni kwamba kuumba maana yake ni kukipatisha kitu na kukianzisha. Ama kukitia sura ni kukipa kitu sura hasa baada ya kukianzisha.

Unaweza kuuliza kuwa, wafuasi wa Darwin wanasema kwamba mtu kwanza alipatikana katika sura isiyokuwa hii aliyo nayo sasa; kisha ikageukageuka mpaka kufikia ilivyo sasa.

Jibu: sisi tuko pamoja na dalili za kielimu zisizokubali shaka na dhana za kupinga. Kwa sababu pale tu inapozuka dhana, basi dalili hubatilika. Hii ni hakika ya ubainifu iliyo wazi hawaipingi hata wenye nadharia ya majaribio ambao wamesema chimbuko la maarifa ni lazima litokane na majaribio ya kuhisi.

Dalili kubwa waliyoitegemea wenye nadharia ya mageuzi ni ufukuaji wa vitu vya kale; kuwa wamegundua aina za wanyama, wengine ni bora zaidi. Na kwamba muda wa wale waliokuwa bora zaidi umechelewa kuliko wa wale walio duni na kwamba kuna kushabihiana na binadamu katika mambo mengi.

Sisi hatupingi ugunduzi huu lakini, hauthibitishi nadharia ya Darwin. Kwa sababu hauleti uhakika usio na shaka kuwa aliye bora amekuwa kutokana na aliye duni, bali hilo haliwezekani na inawezekana kuwa kila mmoja kati ya aliye bora na duni ni aina nyingine iliyopatikana kutokana na hali inayo afikiana nayo, kisha ikatoweka wakati ilipobadilika hali yake, kama zilivyotoweka aina nyinginezo za wanyama na mimea.

Ikiwa mambo mawili yanawezekana, basi kuchukua moja tu, na kuacha jingine ni kujichukulia madaraka.

Katika niliyoyasoma ni kwamba wataalamu wengi, wakiwemo walahidi, walikuwa wakiamini nadharia ya Darwin, lakini walipoingia katika nyanja za elimu wakabadilika kutokana na yale tuliyoyataja; na kwamba mtu ana aina pekee za kiakili na kiroho zinzohusiana naye, zinazomfanya awe tofauti na viumbe vingine.

Kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam. Basi wakasujudu wote isipokuwa Iblisi hakuwa miongoni mwa waliosujudu.

Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:82)

Akasema: Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipoamrisha?

Makusudio ya kusujudu hapa ni kusujudu kwa kimaamkuzi, sio kwa kiibada, nako ni kumtii Mwenyezi Mungu, kwa sababu ni amri yake.

Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.

Chochote akifanyacho Iblisi, lazima atakitafutie visibabu; na sharti la msingi la kila kisababu katika mantiki yake ni kukhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu na radhi yake. Hiyo ndiyo asili ya kwanza anayoitege- mea Iblis katika kauli zake na vitendo vyake.

Fakihi anajitahidi kufanya utafiti ili aongoke kwenye hukumu alizoziwekea sharia Mwenyezi Mungu, lakini Iblisi kwake yeye sharia za hukumu ni zile zenye msingi wa “Mwenyezi Mungu anasema hivyo nami nase- ma hivi.”

Mwenyezi Mungu alimwamuru Iblisi amsujudie Adam, lakini akakataa wala asiombe msamaha, bali alijigamba kwa kusema: “Vipi nimsujudie ambaye mimi ni mbora wake.” Kama kwamba anamwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu: Ilikuwa wafaa wewe umwamuru Adam anisujudie mimi, sio mimi nimsujudie yeye.

Kwa hivyo utukufu, kwa mantiki ya Iblis ni kwa kuangalia asili, sio kwa kumcha Mwenyezi Mungu; na kwa Mwenyezi Mungu ni vitendo na takua si kwa asili. Na elimu kwa Iblis ni kukisia (Qiyasi) na matamanio; na kwa Mwenyezi Mungu ni Wahyi na hukmu ya kiakili ambayo uwazi wake haufanyi kutofautiana watu wawili.

Kwa hiyo, mwenye kuangalia asili yake au akaifanyia kiasi dini kwa rai yake, basi atakuwa amemfuata Iblis atake asitake.
Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Imepokewa Hadith kutoka kwa Jafar As-sadiq, kutoka kwa baba yake, naye kutoka kwa babu yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) amesema: “Wa kwanza aliyeifanyia makisio (qiyas) dini ni Iblis, Mwenyezi Mungu alimwambia amsujidie Adam, yeye akasema ni bora kuliko huyo”

Kisha akaendelea kusema Jafar: “Mwenye kulifanyia makisio (qiyas) jambo la dini, Mwenyezi Mungu atamkutanisha na Iblis siku ya kiyama.”

Utauliza: Aya hii inafahamisha kuwa uhai unapatikana kutokana na moto kama vile Aya nyingine isemayo:

وَخَلَقَ الْجَانَّ مِنْ مَارِجٍ مِنْ نَارٍ {15}

“Na akaumba majini kwa ulimi wa moto.” (55:15)

Na Aya nyingine inasema:

وَجَعَلْنَا مِنَ الْمَاءِ كُلَّ شَيْءٍ حَيٍّ ۖ {30}

“Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai” (21:30).

Jibu: Vitu hai vilivyotajwa katika Qur’an tukufu viko aina nyingi: Kuna ulimwengu wa Malaika, wa majini na vile vilivyomo katika ardhi hii. Aina hii ya tatu ndiyo ambayo uhai wake uko katika maji, kama vile wanyama, mimea na watu. Hiyo ndiyo iliyokusudiwa kiujumla katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Na tukafanya kwa maji kila kitu kilicho hai.’

Na kuna viumbe vingine ambavyo uhai wake uko katika moto. Kwa maneno mengine ni kwamba maji ni lazima kwa maisha ya mwanaadamu kulingana na maumbile yake, pia wanyama na mimea. Lakini hii haikanushi kuwa kuna viumbe vingine ambavyo moto ni lazima katika maisha yao. Wataalamu wa elimu ya wadudu wanasema: Kuna aina ya wadudu ambao maisha yao yanategemea hewa ya sumu na visima vya mafuta (Petroli)!

Akasema: Basi shuka kutoka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka, hakika wewe ni miongoni mwa walio duni.

Imesemeka kuwa dhamir ya ‘huko’ inarudia Pepo. Wengine wakasema ni mbinguni. Sisi hatujishughulishi na ufafanuzi ikiwa haukutajwa katika Qur’an wala Hadith, tunatosheka na ujumla.

Mfumo wa maneno unaonyesha kwamba dhamir inarudia kwenye daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu; maana yakiwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimfukuza Iblis kutoka katika rehema yake hadi kwenye laana yake, ikiwa ni malipo ya kiburi chake na kujizuilia kwake kumtii Mwenyezi Mungu. Kwani kumsujudia Adam ni amri ya Mwenyezi Mungu na ni kumtii Mwenyezi Mungu na sio Adam. Kila anayejiona kuwa sawa ni kukataa hukumu ya Mwenyezi Mungu, basi anastahiki laana mpaka siku ya malipo.

Akasema: Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.

Iblis alikuwa na haja nafsini mwake - atakayoifafanua - ya kutaka kupewa muda.

Akasema - Mwenyezi Mungu Mtukufu - Utakuwa katika waliopewa muda. Inasemekana Iblis alitaka muda mpaka siku ambayo watafufuliwa wafu wote kwa ajili ya hisabu na malipo, Mwenyezi Mungu akakataa maombi haya, akampa muda mpaka siku ya kufa wote walio hai, ambao umeashiriwa na Aya isemayo:

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ {37}

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ {38}

“Akasema: Hakika wewe ni katika waliopewa muda mpaka siku ya wakati maalum” (15: 37 38).

Na siku hiyo ni ile saa ya kupuziwa Parapanda ambayo imeelezwa na Aya isemayo:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَمَنْ فِي الْأَرْضِ {68}

“Na itapulizwa parapanda watoke roho waliomo ardhini na waliomo mbinguni …” (39: 68).

Akasema: Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako iliyonyooka.

Iblis alijiwekea mkakati kuwa atalipizia kisasi kwa kiumbe huyu aliyekuwa ni sababu ya kufukuzwa kwake kutoka katika rehema ya Mwenyezi Mungu kwenda kwenye laana. Akabainisha aina hii ya kujilipiza kwamba yeye ataikalia na kuziba njia, kwa Adam na kizazi chake, ile ielekeayo kwa Mwenyezi Mungu na kwenye twaa yake.

Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.

Kuwaendea kwake kwa pande hizi nne ni fumbo la ushawishi wake na jitihada yake katika kuwapoteza, kiasi ambacho hataacha maasi yoyote ila huwahada kwayo, wala twaa yoyote ila huwazuia.

Mwenyezi Mungu akiwaamrisha jihadi na kujitolea mhanga, basi Iblisi huwapendekezea uhai. Na kama Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akiwahimiza kujitolea mali katika njia yake Mwenyezi Mungu, basi mlaanifu huyu huwahofisha na ufukara.

Ikiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anawakataza pombe, zinaa na kamari, yeye huwavutia huko kwenye anasa na matamanio. Mungu akiwapa kiaga cha moto na kuwaahidi Pepo, basi adui huyu wa Mwenyezi Mungu huwaambia, hakuna Pepo wala moto.

Basi namna hii huhisabu kila haki kuwa ni batil na kila msimamo kuwa ni kombo. Hii inafanana kabisa na wale waliouza dini yao kwa shetani wak- iboresha vitendo vya wakoloni, wakiua wanawake na kuwafukuza wasio na hatia nchini mwao.

Akasema: Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kufedheheka na mwenye kufukuzwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemhusisha Iblisi na kufedheheka na kufukuzwa kwa kuwa yeye Mwenyezi Mungu alimteremsha cheo alichokuwa nacho.

Atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.

Yaani Jahannam itakuwa yake na wanachama wake waliomfuata. Aya hii ni kama ile isemayo:

لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْكَ وَمِمَّنْ تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ {85}

“Kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa wewe na wale wanaokufuata miongoni mwao wote” (38:85).

Hapa kuna maswali yanayotaka kujibiwa:

1. Kwanza, Je, maneno yalikuwa ni moja kwa moja au ni kwa kupitia hali fulani?

2. Pili, kauli ya Iblis: “Umenipoteza” inafahamisha kwamba kupotea kwake kulitokana na Mwenyezi Mungu, vipi atamwadhibu?

3. Tatu, kwa nini Mwenyezi Mungu amempa muda Iblis naye anajua ufisadi wake na kuwaharibu wengine?

Tutajibu maswali haya matatu kwa ufupi sana:

Jibu la kwanza, ni kuwa sisi tunaamini kuweko kwa majibizano hayo, kwa vile Wahyi umefahamisha hilo na akili hailipingi hilo, na si juu yetu kufanya utafiti wa aina ya majibizano hayo yalivyokuwa, maadamu Wahyi haukufafanua.

Kuhusu jibu la pili, upotevu unatokana na Iblis, na wala hautokani na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Iblis mwenyewe amekiri kuwa yeye ni mpotezaji katika Aya isemayo:

وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ {39}

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ {40}

“Na nitawapoteza wote isipokuwa waja wako waliosafishwa” (15: 39 –40).

Na vipi Mwenyezi Mungu ampoteze mja kisha amwadhibu kwa upotevu? Mwenyezi Mungu ametakata kabisa na hayo.

Ama kauli ya Iblis “Umenipoteza” Maana yake ni kwa kuwa umenifanyia mtihani wa kuniamrisha kumsujudia Adam, mtihani ambao umeniingiza katika uovu na uasi, basi nami nitafanya hivi na vile. Kwa maneno mengine ni kuwa Iblis anasema kwa kuwa umeniamrisha na nikaasi amri yako, basi sitamwacha yeyote atii amri yako.

Jibu la swali la tatu ni kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu yamehukumia kumpa mtu akili, ukumbusho kupita utume, uwezo wa kufanya kheri na shari na kumwachia hiyari na kumjaribu kwa matamanio na hadaa ana- zoshawishiwa na Iblis na majeshi yake; ili kumpambanua mwema na mwovu na mwenye ikhlas na mwenye khiyana.

Kwa maelezo zaidi angalia Juz.7 (5:94) kifungu ‘Maana ya mtihani wa Mwenyezi Mungu.’

وَيَا آدَمُ اسْكُنْ أَنْتَ وَزَوْجُكَ الْجَنَّةَ فَكُلَا مِنْ حَيْثُ شِئْتُمَا وَلَا تَقْرَبَا هَٰذِهِ الشَّجَرَةَ فَتَكُونَا مِنَ الظَّالِمِينَ {19}

Na Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani (Pepo); na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, wala msiukurubie mti huu msije mkawa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao).

فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ لِيُبْدِيَ لَهُمَا مَا وُورِيَ عَنْهُمَا مِنْ سَوْآتِهِمَا وَقَالَ مَا نَهَاكُمَا رَبُّكُمَا عَنْ هَٰذِهِ الشَّجَرَةِ إِلَّا أَنْ تَكُونَا مَلَكَيْنِ أَوْ تَكُونَا مِنَ الْخَالِدِينَ {20}

Basi shetani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa. Na akasema: Mola wenu hakuwakataza mti huu ila msije mkawa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele.

وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ {21}

Na akawaapia: Kwa hakika mimi ni miongoni mwa watoa nasaha kwenu.

فَدَلَّاهُمَا بِغُرُورٍ ۚ فَلَمَّا ذَاقَا الشَّجَرَةَ بَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِنْ وَرَقِ الْجَنَّةِ ۖ وَنَادَاهُمَا رَبُّهُمَا أَلَمْ أَنْهَكُمَا عَنْ تِلْكُمَا الشَّجَرَةِ وَأَقُلْ لَكُمَا إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمَا عَدُوٌّ مُبِينٌ {22}

Basi akatelezesha kwa hadaa. Walipouonja mti ule, tupu zao ziliwadhihirikia, wakaanza kujibandika majani ya kwenye Bustani (Pepo). Na Mola wao akawaita: Je, sikuwakataza mti huo na kuwaambia kwamba shetani ni adui yenu wa dhahiri?

قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنْفُسَنَا وَإِنْ لَمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ {23}

Wakasema: Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu; na kama hutatughufiria na kuturehemu tutakuwa miongoni mwa waliohasirika.

قَالَ اهْبِطُوا بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ ۖ وَلَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَىٰ حِينٍ {24}

Akasema: Shukeni, nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Na makao yenu na starehe yatakuwa katika ardhi kwa muda.

قَالَ فِيهَا تَحْيَوْنَ وَفِيهَا تَمُوتُونَ وَمِنْهَا تُخْرَجُونَ {25}

Akasema: Mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa kutoka humo.