read

Aya 114 – 117: Nimtafute Hakimu Asiyekuwa Mwenyezi Mungu

Maana

Je, nimtafute hakimu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na hali yeye ndiye aliyewateremshia Kitab kinachofafanua?

Aya hii inaambatana na ile Aya ya ugomvi na uadui baina ya Mtume na washirikina ambao walimtaka awaonyeshe muujiza. Maana ni kuwa Mtume (s.a.w.) aliwaambia washirikina kwamba nyinyi mnatoa hukumu katika kutaka miujiza na mnanipangia mambo, na mimi siwezi kuikiuka hukumu ya Mwenyezi Mungu.

Qur’an imekwisha washukia, inatosha na kutekeleza mnayoyahitajia kujua haki, halali na haramu. Haina mfano wake katika misingi yake na mafunzo yake. Ni yenye kuthibitisha ukweli wake kwa kutumia ufasaha wake ushindao, ina sharia zenye kudumu milele na kutoa habari nyingi za ghaibu. Kwa hiyo, huku kutaka kwenu mambo mengi si lolote ispokuwa ni inadi tu.

Na wale tuliowapa Kitab wanajua kwamba imeteremshwa na Mola wako kwa haki.

Yaani wale wenye insafu katika maulama wa kiyahudi na kinaswara, wana- jua kwa yakini ukweli wa Qur’an na Utume wa Muhammad (s.a.w.). Tazama Aya yenye maneno kama haya katika Juz. 2 (2:146).

Basi usiwe miongoni mwa wanaotia shaka.

Wafasiri wengi wamesema kuwa msemo huu (usitie shaka) anaambiwa Mtume na makusudio ni asiyekuwa yeye kwa njia ya fumbo.
Ama sisi tunaona kuwa msemo unaelekezwa kwa Mtume, na yeye ndiye makusudio, pamoja na kujua kuwa Mtume hatii shaka Qur’an, bali ni muhali kwake kutia shaka. Imesihi kuelekezwa msemo kwake pamoja na isma yake, kwa vile unatoka kwa aliye juu (Mwenyezi Mungu) kwenda kwa aliye chini. Hayo tumeyaeleza mara nyingi.

Na limetimia neno la Mola wako kwa ukweli na uadilifu.

Makusudio ya neno la Mola wako hapa ni Qur’an au Uislam ambao umeshinda juu ya dini zote wajapochukia washirikina. Haya ndiyo makusudio kwa ukamilifu. Ama maana ya kwa ukweli na uadilifu ni kuwa Qur’an ni kweli katika kila inayoyasema, na ni uadilifu katika kila inay- ohukumu na kuwekea sharia.

Hakuna wa kubadilisha neno lake.

Kwa sababu ni ukweli na uadilifu na kila ambalo ni ukweli na uadilifu basi ni hali halisi, wala haiwezi kusemwa jambo ni ukweli na uadilifu ikiwa halina msingi halisi. Na msingi huu haubadiliki wala haugeuki; yaani hauepukani na athari na natija iliyopangiwa.

Na yeye msikizi wa wanayoyasema mjuzi wa wanayoyafanya na wanayoyadhamiria.

Na kama ukiwatii wengi katika waliomo ardhini watakupoteza na njia ya Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana na hawakuwa ila wenye kuzua tu.

Kila mwenye kushikamana na dini basi huamini kwa imani ya moja kwa moja, na hushikamana nayo kwa upofu, na kila rai anayoiona huona ni kweli, na kwamba mengineyo ni njozi na dhana tu. Kwa hiyo tukizikusanya rai zote na itikadi zote na tukazipima kwa vipimo vya Mwenyezi Mungu, natija ni kuwa watu wengi hufuata dhana za makosa na za uongo.

Kwa ajili hiyo ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake asiwasikilize watu na kutowaheshimu na ada zao na itikadi zao; na kwamba ni juu yake kufuata yale aliyopewa Wahyi na Mwenyezi Mungu kwa sababu ndiyo njia ya haki na uwongofu.

Ikiwa watu wengi wako kwenye makosa katika rai na dini, basi hakuna kipimo cha kauli zao na hukumu zao kwa uwongofu wa hili na upotofu wa lile. Isipokuwa hukumu katika hilo ni ya Mwenyezi Mungu peke yake; yaani yale aliyoyabainisha katika misingi na uthabiti uliomo katika Kitabu chake chenye hekima.

Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Hakika Mola wako anawajua vyema wanaopotea njia yake na anawajua sana wanaoongoka.

Katika msingi hiyo ya Mwenyezi Mungu inayowapambanua wenye haki na wenye batili ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِمَّنْ دَعَا إِلَى اللَّهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ {33}

“Na ni nani mbora wa kusema kuliko alinganiaye kwa Mwenyezi Mungu, na akafanya amali njema na akasema: Mimi ni miongoni mwa waislamu.” (41:33).

فَكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ عَلَيْهِ إِنْ كُنْتُمْ بِآيَاتِهِ مُؤْمِنِينَ {118}

Basi kuleni katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake.

وَمَا لَكُمْ أَلَّا تَأْكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّهِ عَلَيْهِ وَقَدْ فَصَّلَ لَكُمْ مَا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ ۗ وَإِنَّ كَثِيرًا لَيُضِلُّونَ بِأَهْوَائِهِمْ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِالْمُعْتَدِينَ {119}

Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu? Na amewafafanulia aliyowaharamishia isipokuwa vile mnavyolazimika. Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya ilimu. Hakika Mola wako anawajua vyema wanaoru- ka mipaka.

وَذَرُوا ظَاهِرَ الْإِثْمِ وَبَاطِنَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَكْسِبُونَ الْإِثْمَ سَيُجْزَوْنَ بِمَا كَانُوا يَقْتَرِفُونَ {120}

Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana. Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa yale waliyokuwa wakiyachuma.

وَلَا تَأْكُلُوا مِمَّا لَمْ يُذْكَرِ اسْمُ اللَّهِ عَلَيْهِ وَإِنَّهُ لَفِسْقٌ ۗ وَإِنَّ الشَّيَاطِينَ لَيُوحُونَ إِلَىٰ أَوْلِيَائِهِمْ لِيُجَادِلُوكُمْ ۖ وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ {121}

Wala msile wale wasiosomewa jina la Mwenyezi Mungu kwani huko ni ufasiki. Na hakika mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi. Na kama mkiwatii, hakika mtakuwa washirikina.