read

Aya 118 – 121: Bismillah Kwa Kinachochinjwa

Maana

Basi kuleni katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake.

Waarabu wakati wa ujahiliya walikuwa wakila mfu, na wakitaja majina ya masanamu wanayoyaabudu wakati wa kuchinja. Mwenyezi Mungu akaharamisha hilo kwa Wailsamu; akahalalishia kula wanaochinjwa kwa sharti ya kutaja jina Lake na sio jina la mwengine.

Unaweza kuuliza kuwa kujuzu kula aliyechinjwa, aliyesomewa jina la Mwenyezi Mungu, hakuambatani na kumwamini Mwenyezi Mungu na ishara zake. Ambapo inajuzu kwa kafiri kumla huyo; kama ambavyo kumwamini Mwenyezi Mungu hakuambatani na kula aliyesomewa Jina la Mwenyezi Mungu. Ambapo Mumin anakuwa Mumin hata kama hakumla. Lakini dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa kuamini ni sharti la uhalali wa kula chinjo hilo. Kwa sababu maana yake ni, kuleni ikiwa nyinyi ni waumini.

Jibu: Kauli yake Mwenyezi Mungu, ‘Ikiwa nyinyi mnaziamini ishara zake,’ sio sharti la uhalali wa kula chinjo lililosomewa jina la Mwenyezi Mungu, isipokuwa hii ni kuonyesha kuwa anayemtaja asiyekuwa Mwenyezi Mungu kwa chinjo, basi amemfanyia Mwenyezi Mungu mshirika.

Kwa sababu, ameelekeza tendo lake hili kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kama walivyokuwa wakifanya washirikina wa Kiarabu; na kwamba mwenye kutaja jina la Mwenyezi Mungu kwa chinjo basi atakuwa amemwamini Mwenyezi Mungu na amemkanushia mshirika. Kwa vile atakuwa amemwelekea yeye tu peke yake.

Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu?

Inaonyesha, kutokana na Aya hii, kwamba baadhi ya Waislamu walijizuilia kula chinjo ambalo limesomewa jina la Mwenyezi Mungu kwa kujitatiza; kwamba inakuwaje mtu achinje mnyama kwa mkono wake na ataje jina la Mwenyezi Mungu kisha ale na isijuzu kula mnyama aliyeuliwa na Mwenyezi Mungu ambaye amekufa mwenyewe!

Ndipo Mwenyezi Mungu akalipingia hilo kwa kusema: Mna nini hamli katika wale waliosomewa jina la Mwenyezi Mungu Na amewafafanulia aliyowaharamishia isipokuwa vile mnavyolazimika.

Kuhusu aliyowafafanulia anakusudia wale aliowaishiria katika Aya 145, katika Sura hii, ambayo itakuja tafsir yake Inshaalah. Pia anaashiria wale waliotajwa katika Juz.2 (2:173).
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu walioharamishwa na hukumu ya aliyelazimika katika Juz.2 (2:173).

Na hakika wengi wanapoteza kwa matamanio yao bila ya ilimu.

Yaani wanahalalisha na kuharamisha kulingana na matamanio yao bila ya dalili. Miongoni mwa hayo ni kuwa washirikina wa Kiarabu walihalalisha kula nyamafu na kuharamisha kula bahira, saiba, wasila na hami. Umetangulia ufafanuzi wa hayo katika Juz.6 (5:3).

Hakika Mola wako anawajua vyema wanaoruka mipaka.

Ambao wanahalalisha na kuharamisha kwa hawaa zao na matamanio yao. Na kwamba atawaadhibu inavyostahiki.

Na acheni dhambi zilizo dhahiri na zilizofichikana.

Makusudio ya dhambi ni kitendo cha haramu kinacholeta dhambi; na dhahiri yake ni kufanya maasi dhahiri; na kufichikana ni kuyafanya kisiri. Mwenyezi Mungu amekataza kufanya maasi yote ya dhahiri na ya batini.

Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa yale waliyokuwa wakiy- achuma katika kufuata matamanio bila ya elimu; wala hawataachwa bure bure bila ya hisabu na adhabu.

Wala msile wale wasiosemowa jina la Mwenyezi Mungu kwani huko ni ufasiki.

Dhamiri ya huko inarudia kula. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuhalalishia waliochinjwa kwa jina lake, anaharamisha ambao hawakutajiwa.

Kwa kutegemea hilo, ndipo mafakihi wote, isipokuwa Shafii, wamekonga- mana kuwa mchinjaji akiacha kutaja jina la Mwenyezi Mungu kwa makusudi, basi ni haramu; sawa na nyamafu. Inatosha jina la Mwenyezi Mungu tu, mfano: Allah, Allahu Akbar, Al-Hamdulillah, Bismillah, Lailaha illa Ilah na mfano wake.

Wametofautiana kuacha kusoma jina la Mwenyezi Mungu kwa kusahau. Hanafi, Jaafariya (Shia) na Hanbal wamesema si haramu nyama hiyo. Malik akasema ni haramu na Shafii amesema kuwa akiwacha kusoma jina la Mwenyezi Mungu kwa makusudi pia si haramu, sikwambii tena kusahau.

Na hakika mashetani wanawafunza marafiki zao kubishana nanyi.

Makusudio ya mashetani hapa ni maiblis–watu ambao wanauviringa ukweli na kutunga maneno wanayowahadalia wale wenye akili za juu juu. Kwa mafano, baadhi ya washirikana na maiblis wao walikuwa wakiwaambia wafuasi wao.

Waulizeni Masahaba wa Muhammad, vipi mnakula mnyama mliyemuua nyinyi wenyewe, kumchinja kwa mikono yenu; na wala hamli mnyama aliyeuawa na Mwenyezi Mungu, aliyekufa mwenyewe ambapo aliyeuawa na Mwenyezi Mungu ni bora kuliko mliyemuua nyinyi?

Huo ndio mjadala wao ambao mashetani waliwashauri marafiki zao kwa makusudio ya kuingiza shaka katika nyoyo dhaifu za baadhi ya Waislamu na kuwafitini na dini yao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema kuwaambia hawa wadhaifu:

Na kama mkiwatii, hakika mtakuwa washirikina.

Yaani mwenye kuwasikiliza washirikina na akahalalisha kula nyamafu, kama walivyohalalisha, basi yeye ni mshirikina kama wao, na hukumu hii haihusiki na kula nyamafu peke yake, bali kila anayepinga hukumu ya sharia akijua kuwa imethibiti, basi huyo ni kafiri.

أَوَمَنْ كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَنْ مَثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {122}

Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru, hutembea mbele za watu kwayo, mfano wake ni kama yule aliyegizani asiyeweza kutoka humo? Namna hiyo wamepambiwa makafiri waliyokuwa wakiyafanya.

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا فِي كُلِّ قَرْيَةٍ أَكَابِرَ مُجْرِمِيهَا لِيَمْكُرُوا فِيهَا ۖ وَمَا يَمْكُرُونَ إِلَّا بِأَنْفُسِهِمْ وَمَا يَشْعُرُونَ {123}

Na kama hivyo tumejaalia katika kila mji wakubwa wa wakosefu wake ili wafanye vitimbi humo; wala hawafanyii vitimbi isipokuwa wanajifanyia wenyewe, lakini hawatambui.

وَإِذَا جَاءَتْهُمْ آيَةٌ قَالُوا لَنْ نُؤْمِنَ حَتَّىٰ نُؤْتَىٰ مِثْلَ مَا أُوتِيَ رُسُلُ اللَّهِ ۘ اللَّهُ أَعْلَمُ حَيْثُ يَجْعَلُ رِسَالَتَهُ ۗ سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللَّهِ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ {124}

Na zinapowafikia ishara husema: Hatutaaamini mpaka tupewe sawa na yale waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake. Itawafika wale waliokosea dhila inayotoka kwa Mwenyezi Mungu na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya.