read

Aya 122 – 124: Kumhuisha Maiti

Maana

Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru, hutem- bea mbele za watu kwayo, mfano wake ni kama yule gizani asiyeweza kutoka humo?

Huu ni mfano alioupiga Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kulinganisha baina ya mumin na kafiri. Ufafanuzi wake ni kuwa, kuwalinganisha wawili hao ni sawa na kulinganisha mauti na uhai. Na mwanga na giza. Kafiri ni maiti akiamini hufufuliwa upya na kurudiwa na uhai na imani yake ni nuru anayokwenda nayo katika uhai wake.

Anayebakia kwenye ukafiri na shirki ni kama anajikokota gizani, anakwenda bila ya uongozi na haimfikii kheri yoyote katika maisha yake yote.

Mwenye Kuulizwa Na Muulizaji Mkuu

Mtu anaweza kusema kuwa Aya imefananisha imani na uhai; na ukafiri na mauti; ingawaje makafiri na walahidi, katika zama hizi, wanaishi maisha ya anasa na wenye utajiri zaidi kuliko waumini na wenye kuabudu?

Jibu: Makusudio ya uhai katika Aya hii sio kuishi mtu katika neema na anasa, akawa anakula vizuri, kuvaa nguo za thamani na kunywa vinywaji vitamu. Hakika anasa hazihusiani na ukafiri wala imani. Kama ni hivyo waumini wa Mashariki na Magharibi wangelikuwa sawa katika maendeleo na uchumi mzuri, vilevile walahidi na makafiri.

Hali nzuri ya maisha ina sababu na mambo yanayoambatana nayo ambayo hayafungamani na chochote katika imani au ukafiri. Isipokuwa makusudio ya uhai, katika Aya hii, ni imani na hisia za kidini zinazompa mtu msukumo wa kutekeleza wajibu, akiwa ni mtu atakayeulizwa kuhusu mwenendo wake, atahisabiwa na kulipwa thawabu kwa wema wake, na adhabu kwa uovu wake.

Lau mtu angelikuwa si mwenye kuulizwa chochote, ingelikuwa sharia na kanuni ni maneno tu, yasiyokuwa na maana yoyote. Na tukipitisha kuwa mtu ataulizwa wala hataachwa bure bure, basi itatulazimu tupitishe kwam- ba yeye ataulizwa mbele ya yule ambaye

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ {23}

“Haulizwi anayoyafanya, na wao ndio wanaoulizwa” (21:23).

Lau muulizaji huyu anaulizwa, basi ingelipaswa kupatikana atakayemuuliza, na kuendelea hivyo hivyo bila mwisho.

Mwenye kukanusha kuweko muulizaji mkuu kabisa ambaye huuliza na haulizwi, basi atakuwa amekanusha maulizo. Kwa sababu hakuna maulizo bila ya muulizaji. Na mwenye kukanusha maulizo amekanusha maisha ya kijamii.

Unaweza kusema: Ndio mtu ataulizwa, lakini si lazima muulizaji awe Mwenyezi Mungu; watu wanaweza kuchagua kundi (kamati) ambalo litauliza watu.

Nasi tutauliza je kundi hilo likikosea, liulizwe na lihukumiwe na nani? Ikijibwa ni dhamir. Tutasema: Kwanza, dhamir ni jambo la kimaana si la kidhati. Pili, dhamiri anayo kila mtu, kwanini huyu aache dhamiri yake afuate ya mwingine?

Kwa hiyo, basi hakuna muulizaji asiyeulizwa ila Mwenyezi Mungu peke yake. Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu akailazimisha nafsi yake kufuata sharia za Mwenyezi Mungu na hukumu zake, basi atakuwa na busara ya mambo yake, itikadi yake na tabia zake. Vinginevyo atakuwa kama aliye gizani asiyeweza kutoka.

Namna hiyo wamepambiwa makafiri waliyokuwa wakiyafanya.

Yaani kama waliyvopambiwa waumini amali zao, vilevile washirikina wamepambiwa amali zao. Tofauti ni kuwa wao wamepambiwa kinyume na hali halisi, wamepambiwa, kimawazo na kinjozi tu.

Na kama hivyo tumeajaalia katika kila mji wakubwa wa wakosefu wake.

Makusudio ya mji ni kila jamii (mkusanyiko) wa watu, wachache au wengi. Maana ni kuwa: Ewe Muhammad kama ambavyo wanapatikana katika jamii yako viongozi wa waovu wanaofanya vitimbi na kuifanyia uadui dini ya Mwenyezi Mungu, vilevile katika jamii zilizotangulia walikuwapo; na hivi sasa pia wako viongozi wanaowafanyia vitimbi watu wao na kuwa katika msimamo wa kuifanyia uadui haki na wenye haki.

Unaweza kuuliza: Dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye aliyewafanya wakubwa kuwa waovu kwa watu wa haki, na tunajua kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hukataza vitimbi na uovu; je, kuna taawili gani hapa?

Jibu: Makusudio ya kunasibishwa kwake huku Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kuashiria kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu yamepitisha kuwa desturi ya jamii iwe kwenye misingi ya kupingana baina ya wenye haki na wenye batili, baina ya viongozi wenye kufanya uadui na wenye kufanyiwa uadui.

Hakuna kimbilio la kuepuka mgongano huu ila kumalizwa waovu; na hapana budi kutimia hilo na kutukuka neno la haki mikononi mwa wanaolingania uadilifu na utengenevu; hata kama batili itakuwa kubwa kiasi gani. Hilo amelisajili Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Kitabu chake, aliposema:

وَلَا يَحِيقُ الْمَكْرُ السَّيِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ ۚ فَهَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِينَ ۚ فَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَبْدِيلًا ۖ وَلَنْ تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّهِ تَحْوِيلًا {43}

“Na vitimbi vibaya havimpati ila yule aliyevifanya. Basi hawangoji ila desturi iliyokuwa kwa watu wa zamani, wala hutakuta mabadiiko katika desturi ya Mwenyezi Mungu, wala hutakuta mageuko katika desturi ya Mwenyezi Mungu.” (35:43)

Kukaririka huku ni kutilia mkazo kwamba mwisho ni wa wanaomcha Mwenyezi Mungu; kadiri zitakavyorefuka zama. Hivi ndivyo tunapata tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Ili wafanye vitimbi humo; wala hawafanyii vitimbi isipokuwa wanajifanyia wenyewe, lakini hawatambui.

Na zinapowafikia ishara husema: Hatutaaamini mpaka tupewe sawa na yale waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Wametofautiana wafasiri katika maana ya Aya hii kwa kauli mbili: Kwanza, kwamba wakubwa waovu katika Waarabu walimtaka Muhammad (s.a.w.) awaletee muujiza kama aliopewa Musa, wa kupasua bahari; na wa Isa, wa kufufua wafu.

Kauli ya pili, ni kuwa wao walimwambia hatutakuamini mpaka utushushie wahyi kama ulivyowashukia Mitume. Razi akasema: “Hii ndio kauli mashuhuri baina ya wafasiri.”

Nasi tunaipa uzito kuliko ya kwanza. Kwa sababu mfumo wa Aya unafahamisha hivyo, ambapo Mwenyezi Mungu anawajibu wakubwa waovu kwa kauli yake:

Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake.

Kuongezea kuwa kutaka kwao Mwenyezi Mungu awateremshie Wahyi kunaafikiana na hasadi yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amesema:

أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ ۖ {54}

“Au wanawahusudu watu kwa alichowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake?” Juz.5 (4:54)

Katika Majmaul-bayan na kwengine, imeelezwa kuwa Walid bin Mughira alimwambia Mtume (s.a.w.): “Lau Utume ungelikuwa ni kweli mimi ningelistahiki zaidi kuliko wewe, kwa sababu mimi ni mkubwa kuliko wewe, na nina mali nyingi kushinda wewe.”

Maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa kujua mahali anapoweka ujumbe wake’, ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anauchagulia ujumbe wake mtu atakayefaa katika viumbe vyake, na Muhammad ni Mtukufu zaidi wa viumbe vya Mwenyezi Mungu na aheshimiwaye zaidi kwao.

Itawafika wale waliokosea dhila inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu walijifanya wakubwa wakajiadhimisha. Ndipo wakastahiki malipo ya udhalilifu na fedheha. Kuna Hadith isemayo kuwa wenye kutakabari watafufuliwa katika Sura ya chembe (kama sisimizi) watakanyagwa na watu kwa nyayo zao, ikiwa ni malipo ya kujifanya kwao wakubwa katika dunia.

Na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya.

Udhalili ni malipo ya kiburi, na adhabu ni malipo ya vitimbi na hadaa. Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawafanyia wale wenye nia mbaya na malengo ya ufisadi kinyume cha wanavyokusudia na wanavyolenga.

فَمَنْ يُرِدِ اللَّهُ أَنْ يَهْدِيَهُ يَشْرَحْ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ ۖ وَمَنْ يُرِدْ أَنْ يُضِلَّهُ يَجْعَلْ صَدْرَهُ ضَيِّقًا حَرَجًا كَأَنَّمَا يَصَّعَّدُ فِي السَّمَاءِ ۚ كَذَٰلِكَ يَجْعَلُ اللَّهُ الرِّجْسَ عَلَى الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ {125}

Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumwongoza humfungulia kifua chake Uislam; na yule anayetaka apotee hufanya kifua chake kina dhiki kimebana. Kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hii anajaalia Mwenyezi Mungu adhabu juu ya wale wasioamini.

وَهَٰذَا صِرَاطُ رَبِّكَ مُسْتَقِيمًا ۗ قَدْ فَصَّلْنَا الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَذَّكَّرُونَ {126}

Na huu (Uislamu) ndio njia ya Mola wako iliyonyooka. Hakika tumezipambanua ishara kwa watu wenye kukumbuka.

لَهُمْ دَارُ السَّلَامِ عِنْدَ رَبِّهِمْ ۖ وَهُوَ وَلِيُّهُمْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {127}

Watapata nyumba ya salama kwa Mola wao naye ndiye walii wao, kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyatenda.