read

Aya 125 – 127: Humfungulia Kifua Chake Uislam

Maana

Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumwongoza humfungulia kifua chake Uislam; na yule anayetaka apotee hufanya kifua chake kinadhiki kimebana.

Anasema Razi: “Wameshikilia masahibu zetu -yaani Sunni Ashaira - Aya hii katika kubainisha kuwa upotevu na uongofu unatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Ama masahibu zetu sisi- Shia - wanasema lau ingelikuwa upotevu na uongofu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, basi kusingelikuwa na taklifu zozote na ingebatilika hisabu na malipo. Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwadilifu, hawezi kufanya jambo na kisha amhisabu mwingine kwalo. Itakuwaje hivyo na hali yeye ndiye aliyesema:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ{164}

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.” (6:164)

Ama Aya hii tuliyonayo haifahamishi madai ya Razi na masahibu zake; wa haikuja kubainisha chimbuko la upotevu na uongofu, au kwamba unatoka kwa Mwenyezi Mungu au mwinginewe; isipokuwa imekuja kubainisha kuwa watu ni makundi mawili:

Kundi la kwanza, ni wale ambao vifua vyao vitakunjukia haki, wataitumia na kuitegemea, kwa sababu ya mwamko wao, kujiepusha kwao na malengo ya kiutu na kujikomboa na kuiga na hawaa. Hao ndio wanaokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ {18}

“Ambao husikia maneno wakafuata yaliyo mazuri yao. Hao ndio aliowaongowa Mwenyezi Mungu na hao ndio wenye akili” (39: 18).

Alipojua Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kheri kutoka katika kundi hili aliwazidishia uongofu na akawasaidia kwa tawfiki yake, akasema:

وَيَزِيدُ اللَّهُ الَّذِينَ اهْتَدَوْا هُدًى ۗ {76}

“Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uowongofu wale walioongoka…” (19:76).

Akasema tena:

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ {17}

“Na wale wanaofuata uongofu anawazidishia uongofu na huwapa takua yao.” (47:17).

Vilevile mwalimu humshughulikia na kumshujaisha mwanafunzi wake atakapojua kuwa ni mwerevu na mchangamfu.

Kundi la pili: Ni wale ambao vifua vyao haviikunjukii haki kwa ujinga wao na kuwa finyu fikra zao, au kwa kuwa haki inapingana na manufaa yao na faida zao au desturi zao na takilidi zao. Hawa ndio waliokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَوَيْلٌ لِلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ مِنْ ذِكْرِ اللَّهِ ۚ {22}

“Basi ole wao wale wenye nyoyo ngumu kumkumbuka Mwenyezi Mungu …” (39:22).

Na kauli yake:

مَا يَأْتِيهِمْ مِنْ ذِكْرٍ مِنْ رَبِّهِمْ مُحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ{2}

“Hayawafikii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao ila huyasikiza, na hali wanafanya mchezo.” (21:2).

Na pia kauli yake:

وَلَوْ عَلِمَ اللَّهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَأَسْمَعَهُمْ ۖ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوْا وَهُمْ مُعْرِضُونَ {23}

“Na Mwenyezi Mungu angelijaalia wema wowote kwao angeliwasikilizisha, na lau angeliwasikilizisha wangelikengeuka wakapuuza.” (8:23).

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaachana na mja na kumwacha ajitegemee mwenyewe, ikiwa haoni kheri yoyote kwake; kama ambavyo mwalimu anampuuza mwanafunzi wake baada ya kukata tamaa na kufaulu kwake. Angalia Juz.5 (4:88).

Kama kwamba anapanda mbinguni.

Zamani watu walikuwa wakipigia mfano wa mtu aliyelemewa kwa kupanda mbinguni, ambapo hakuna wasila wa kufika huko kwa hali yoyote. Mfananisho katika Aya unaafikiana na wakati ilipoteremka. Makusudio yake ni kwamba kundi la watu, ambalo ni kundi la pili tulilolielezea, linapata dhiki na uzito wakikalifishwa kufuata haki, sawa na kuamrishwa kupanda mbinguni.

Namna hii anajaalia Mwenyezi Mungu adhabu juu ya wale wasioamini.

Neno Rijsi hapa lina maana ya adhabu. Maana ni kuwa wale wanaoona dhiki na tabu kufuata haki katika dunia, vilevile kesho wataingia katika adhabu ambayo ni kali na kubwa kuliko kufuata haki.

وَقَالُوا لَا تَنْفِرُوا فِي الْحَرِّ ۗ قُلْ نَارُ جَهَنَّمَ أَشَدُّ حَرًّا ۚ {81}

“…. Wakasema msiende katika joto hili. Sema: Moto wa Jahanamu una joto zaidi …” (9:81)

Na huu (Uislamu) ndio njia ya Mola wako iliyonyooka.

Huu, ni ishara ya Uislam ambao hukunjua nyoyo za wale wanaosikiliza kauli wakafuata mazuri yake. Na Uislamu ndio njia isiyo kombo.

Hakika tumezipambanua ishara kwa watu wenye kukumbuka.

Yaani, tumesimamisha dalili na hoja zilizo wazi zenye kutosheleza, juu ya kuswihi Uislamu na ukweli wake katika Qur’an na Aya zake. Kwa hoja hizo watanufaika wale ambao wanajua dalili za haki na kuzitumia.

Watapata nyumba ya salama kwa Mola wao.

Watakaokaa katika nyumba hii ya Mwenyezi Mungu hawatapatwa na uovu wowote wala hawatahuzunika, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye anayewatunza naye ndiye walii wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyatenda miongoni mwa mambo ya kheri na twaa.

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُمْ مِنَ الْإِنْسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُمْ مِنَ الْإِنْسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ {128}

Na siku atakapowakusanya wote, (awaambie): Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika watu. Na marafiki wao katika watu waseme: Mola wetu tulinufaishana sisi na wao, na tumefikia muda wetu uliotuwekea. Atasema: Moto ndio makazi yenu, mtadumu humo, ila apende Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.

وَكَذَٰلِكَ نُوَلِّي بَعْضَ الظَّالِمِينَ بَعْضًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ {129}

Na kama hivi tunawatia mapenzi baadhi, wao kwa wao, kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي وَيُنْذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَٰذَا ۚ قَالُوا شَهِدْنَا عَلَىٰ أَنْفُسِنَا ۖ وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَشَهِدُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ أَنَّهُمْ كَانُوا كَافِرِينَ {130}

Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakuwafikia Mitume miongoni mwenu kuwasomea Aya zangu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii? Watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe kwamba wao walikuwa Makafiri.

ذَٰلِكَ أَنْ لَمْ يَكُنْ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ بِظُلْمٍ وَأَهْلُهَا غَافِلُونَ {131}

Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako hakuwa ni mwenye kuiangamiza miji kwa dhulma na hali wenyewe wameghafilika.

وَلِكُلٍّ دَرَجَاتٌ مِمَّا عَمِلُوا ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ {132}

Na wote wana daraja mbali mbali kutokana na yale waliyoyatenda. Na Mola wako si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.