read

Aya 128 – 132: Siku Atakapowakusanya Wote

Maana

Na siku atakapowakusanya wote, yaani majini na watu, na awaambie Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika watu. Yaani kuwapoteza na kuwahadaa.

Na marafiki wao katika watu waseme; yaani wanadamu ambao wamemtawalisha shetani na kumtii, watasema kumwambia Mwenyezi Mungu: Mola wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Yaani walinufaisha watu na watu wao wakawanufaisha majini. Razi amebainisha wajihi wa kunufaishana huko kwa kusema: “Watu walikuwa wakiwatii majini, kwa hiyo majini wakawa kama viongozi. Huku ndiko kunufaika majini. Ama kunufaika watu, ni kuwa majini walikuwa wakiwafahamisha watu aina za matamanio na kuwafanyia sahali.”

Na tumefikia muda wetu uliotuwekea.

Bado maneno yanaendelea ya watu waliowatii majini. Maana ni kuwa kunufaishana kwetu sisi kwa sisi kulikuwa kwa muda maalum na wakati uliopangwa – nao ni siku ile tulipouacha uhai wa dunia. Sasa tuko mbele yako tukikiri dhambi zetu, basi tuhukumu unavyotaka.

Atasema: Moto ndio makazi yenu, mtadumu humo, ila apende Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo hukumu ya sawa na malipo yenye kulingana.
Hakika Mola wako ndiye mwenye hekima, Mjuzi.

Hupitisha hukumu yake kwenye misingi ya hekima na ujuzi.

Na kama hivi tunawatia mapenzi baadhi wao kwa wao, kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaja katika Aya iliyotangulia (127) kuwa Yeye ndiye walii wa waumini, hapa anataja kuwa makafiri katika majini na watu baadhi yao ni marafiki wa wengine kwa sababu wao wanashirikiana katika kufuru na dhuluma, na siku ya Kiyama watakuwa washirika katika adhabu vilevile.

Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakuwafikia Mitume mion- goni mwenu kuwasomea Aya zangu na kuwaonya kukutana na siku yenu hii?

Swali hili atalielekeza kesho Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa waovu katika majini na watu; nalo ni kulaumu na kukemea; sio kuwa Mwenyezi Mungu anataka kujua. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anajua na wao wanajua kuwa Mwenyezi Mungu amewatumia Mitume watoaji bishara na waonyaji.

وَإِنْ مِنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ {24}

“Na hakuna umma wowote ila alipita humo muonyaji.” (35:24)

Watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu.

Kwa vile hakuna nafasi ya kukanusha hapa. Na mahali pengine aliwapa nafasi wakakadhibisha. Wakasema: “Wallahi, Mola wetu! Hatukuwa washirikina” kama ilivyoelezwa katika Aya 23 ya Sura hii.

Na yaliwadanganya maisha ya dunia.

Kwa sababu dunia haikuficha chochote katika mawaidha yake na mageuzi yake.

Nao watajishuhudia wenyewe kwamba wao walikuwa makafiri.

Kwanza Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja kuwa wao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu, kisha akafuatishia kwa kusema kuwa wao watajishuhudia wenyewe.

Makusudio ya msisitizo huu ni makaripio ya ukafiri na maasia. Kwa sababu mwenye kujaribu kufanya dhambi akiwa na yakini kwamba yeye atalazimika kukiri, basi ataacha, ikiwa ana akili.

Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako hakuwa ni mwenye kuiangamiza miji kwa dhulma na hali wenyewe wameghafilika.

Hayo, ni hayo ya kupeleka Mitume. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ni mwadilifu, hamdhulumu yeyote wala hamwadhibu ila baada ya kutuma Mitume watakaoamrisha mema na kukataza maovu. Kama mja hakuamri- ka na akakoma, basi ataambiwa na Mtume yatakayompata ikiwa hatatubu na kuacha. Akiendelea ataadhibiwa na Mwenyezi Mungu yale anayostahiki.

Na wote wana daraja mbalimbali kutokana na yale waliyoyatenda.

Waovu wana daraja kulingana na dhara zao, kunyonya jasho la wananchi na kutupa mabomu ya Atomic kwa maelfu ya watu. Na wema nao wana daraja kulingana na matendo yao, kuanzia mamkuzi mpaka kufa shahid katika njia ya haki na maslahi ya umma.

Na Mola wako si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.

Kila kitu kimesajiliwa, kiwe kikubwa au kidogo, kizuri au kibaya. Si vibaya kurudia yale tuliyoyaeleza mara kwa mara, kwamba sisi tunaamini kiujumla kuweko majini, kwa sababu wahyi umethibtisha hilo na akili hailikanushi; sawa na kuhusu Malaika. Ama kuhusu ufafanuzi wao bado uko kwa Mwenyezi Mungu Mjuzi wa ghaibu.

وَرَبُّكَ الْغَنِيُّ ذُو الرَّحْمَةِ ۚ إِنْ يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ وَيَسْتَخْلِفْ مِنْ بَعْدِكُمْ مَا يَشَاءُ كَمَا أَنْشَأَكُمْ مِنْ ذُرِّيَّةِ قَوْمٍ آخَرِينَ {133}

Na Mola wako ndiye Mkwasi, mwenye rehema. Akipenda atawaaondoa, na kuweka wengine awapendao baada yenu. Kama alivyowaanzisha kutokana na uzao wa watu wengine.

إِنَّ مَا تُوعَدُونَ لَآتٍ ۖ وَمَا أَنْتُمْ بِمُعْجِزِينَ {134}

Hakika mnayoahidiwa yatafika tu. Wala hamtaweza (kuepuka)

قُلْ يَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ ۖ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَنْ تَكُونُ لَهُ عَاقِبَةُ الدَّارِ ۗ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ {135}

Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni vile muwezavyo; na mimi nafanya. Mtakujajua ni nani atakuwa na makazi mema mwishoni. Hakika madhalimu hawafaulu.