read

Aya 133 – 135: Na Mola Wako Ndiye Mkwasi

Maana

Na Mola wako ndiye mkwasi, mwenye rehema.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja kwamba atawahisabu watu kulingana na matendo yao. Ameashiria kuwa yeye ni mkwasi (mwenye kujitosheleza), hawahitajii viumbe.

Haimnufaishi twaa ya mwenye kumtii, wala hayamdhuru maasi ya mwenye kuasi; na kwamba ulimwengu wote una haja ya rehema yake. Kwa sababu, yeye ndiye sababu ya kwanza ya kupatikana huo ulimwengu.

Akipenda atawaaondoa kwa sababu ni Mkwasi, hawahitajii, na kuweka wengine awapendao baada yenu awabadili wengine wawe watiifu zaidi kuliko nyinyi. Lakini amewaacha na kuwapa muda kutokana na fadhila na ukarimu kutoka kwake.

Kama alivyowaanzisha kutokana na uzao wa watu wengine.

Yaani kama ambavyo imekuwa wepesi kwake kuwaleta nyinyi kutokana na kizazi kilichopita, vilevile ni wepesi kwake kuleta kizazi kipya kutokana na nyinyi na wengineo.

Makusudio ya Aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaonya makafiri, wenye inadi, na maangamivu, kama ilivyokuwa kwa kaumu ya Nuh (a.s.), A’d na Thamud.

Hakika mnayoahidiwa yatafika tu.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwahofisha na adhabu ya dunia, sasa anawahofisha na Kiyama na adhabu yake; kwamba Kiyama kitakuja bila ya shaka yoyote, wala hapana pa kukikimbia ila kwake yeye tu, peke yake.

Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni vile muwezavyo; na mimi nafanya. Mtakujajua ni nani atakuwa na makazi mema mwishoni.

Baada ya Mtume (s.a.w.) kuwalingania kwenye Uislamu waarabu wa ujahiliya na wakaitikia mwito wake walioitikia na kupinga waliopinga, Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwamrisha kuwaambia wenye inadi: Kuweni kama mlivyo na mimi ninafanya kulingana na uongozi wa Mola wangu.
Baada ya muda mtajua mwisho mwema utakuwa wa nani; sawa na kumwambia yule anayepinga nasaha zako: Haya endelea tu utaona!

Hakika madhalimu hawafaulu.

Wale wanaojidhulumu wenyewe au wengineo kwa uadui. Lau angefaulu dhalimu, basi mwadilifu angelikuwa na hali mbaya kuliko dhalimu. Na maneno ya msimamo wa usawa yangelikuwa ni misamiati ya unafiki na ria.

وَجَعَلُوا لِلَّهِ مِمَّا ذَرَأَ مِنَ الْحَرْثِ وَالْأَنْعَامِ نَصِيبًا فَقَالُوا هَٰذَا لِلَّهِ بِزَعْمِهِمْ وَهَٰذَا لِشُرَكَائِنَا ۖ فَمَا كَانَ لِشُرَكَائِهِمْ فَلَا يَصِلُ إِلَى اللَّهِ ۖ وَمَا كَانَ لِلَّهِ فَهُوَ يَصِلُ إِلَىٰ شُرَكَائِهِمْ ۗ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ {136}

Na wamemfanyia sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea aliyoiumba na katika wanyama na kusema: hii ni ya Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, na hii ni ya wale tunaowashirikisha. Basi vile walivyokusudia wale wanaowashirikisha, havifiki kwa Mwenyezi Mungu, na vilivyokuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia wanaowashirikisha. Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu.

وَكَذَٰلِكَ زَيَّنَ لِكَثِيرٍ مِنَ الْمُشْرِكِينَ قَتْلَ أَوْلَادِهِمْ شُرَكَاؤُهُمْ لِيُرْدُوهُمْ وَلِيَلْبِسُوا عَلَيْهِمْ دِينَهُمْ ۖ وَلَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ {137}

Namna hivi wanaowashrik- isha wamewapambia wengi katika makafiri kuwaua watoto wao. Ili kuwaangamiza na kuwavu- rugia dini yao. Na kama Mwenyezi Mungu angependa wasingalifanya hayo. Basi waache na haya wanayoyazua.

وَقَالُوا هَٰذِهِ أَنْعَامٌ وَحَرْثٌ حِجْرٌ لَا يَطْعَمُهَا إِلَّا مَنْ نَشَاءُ بِزَعْمِهِمْ وَأَنْعَامٌ حُرِّمَتْ ظُهُورُهَا وَأَنْعَامٌ لَا يَذْكُرُونَ اسْمَ اللَّهِ عَلَيْهَا افْتِرَاءً عَلَيْهِ ۚ سَيَجْزِيهِمْ بِمَا كَانُوا يَفْتَرُونَ {138}

Na husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko, hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao (tu). Na wanyama wengine imeharamishwa migongo yao, Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao. Wanamzulia tu. Atawapa kwa hayo wanayomzulia.

وَقَالُوا مَا فِي بُطُونِ هَٰذِهِ الْأَنْعَامِ خَالِصَةٌ لِذُكُورِنَا وَمُحَرَّمٌ عَلَىٰ أَزْوَاجِنَا ۖ وَإِنْ يَكُنْ مَيْتَةً فَهُمْ فِيهِ شُرَكَاءُ ۚ سَيَجْزِيهِمْ وَصْفَهُمْ ۚ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ {139}

Na husema: waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharamishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa ni nyamafu hushirikiana. Atawalipa kwa maelezo yao. Hakika Yeye ni mwenye hekima, Mjuzi

قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ قَتَلُوا أَوْلَادَهُمْ سَفَهًا بِغَيْرِ عِلْمٍ وَحَرَّمُوا مَا رَزَقَهُمُ اللَّهُ افْتِرَاءً عَلَى اللَّهِ ۚ قَدْ ضَلُّوا وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ {140}

Hakika wamehasirika wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya elimu. Na wakaharamisha alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu Kwa kumzulia Mwenyezi Mungu. Hakika wamepotea wala hawakuwa wenye kuongoka.