read

Aya 136 – 140: Husema: Hii Ni Sehemu Ya Mwenyezi Mungu

Maana

Na wamemfanyia sehemu Mwenyezi Mungu katika mimea aliyoiumba na katika wanyama na kusema: hii ni ya Mwenyezi Mungu, kwa madai yao, na hii ni ya wale tunaowashirikisha. Basi vile walivyokusudia wale wanaowashirikisha, havifiki kwa Mwenyezi Mungu, na vilivyokuwa vya Mwenyezi Mungu huwafikia wanaowashirikisha. Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu.

Dhamiri katika ‘wamemfanyia’ inawarudia washirikina wa kiarabu.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kubatilisha itikadi ya washirikina, katika Aya zilizotangulia, kwa mantiki ya kiakili na kimaumbile, katika Aya hizi anaonyesha baadhi ya vile ambavyo washirikina walikuwa wakivitenga katika mali zao na watoto wao.

Aya hii tuliyonayo inaonyesha hali zao katika utajiri wao wa mali ambao ni kilimo na mifugo. Walikuwa, kama inavyoelezwa katika vitabu vya tafsiri, wakitenga sehemu katika mimea yao na mifugo kwa ajili ya Mungu na kuitoa kwa watoto na maskini. Na hutenga sehemu kwa ajili ya masana- mu yao, na kuitoa kwa watunzaji na walinzi wa masanamu.

Walikuwa wakijitahidi kuzidisha fungu la masanamu, kuliko la Mwenyezi Mungu, ili litosheleze. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ni tajiri na masanamu ni mafakiri. Ikiwa kitu walichokifanya ni cha Mwenyezi Mungu kinachanganyika na kile walichokifanya cha masanamu, basi hukiachia masanamu. Na ikiwa kile walichokifanya ni cha masanamu kinachanganyika na kile walichokifanya ni cha Mwenyezi Mungu, hukirudisha kwa masanamu. Vilevile wakikumbwa na ukame walikuwa wakila fungu la Mwenyezi Mungu na kuacha fungu la masanamu.

Huu ni ufafanuzi wazi wa “Ni mabaya kabisa wanayoyahukumu” katika kuyatanguliza masanamu yao kuliko Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Namna hivi wanaowashirikisha wamewapambia wengi katika makafiri kuwaua watoto wao.

Yametangulia maelezo kuwa maana ya wanaowashirikisha katika Aya iliyopita kuwa ni masanamu. Ama katika Aya hii inakusudia makuhani na walinzi wa masanamu kulingana na hali ilivyo. Kwa sababu masanamu hayatambui wala hayasemi, basi yatawezeje kuwapambia na kuwahadaa. Maana ni kuwa washirikina kama waliyopiga mafungu mali zao kwa Mwenyezi Mungu na masanamu, vilevile makuhani na watunzaji wamewapambia kuwaua watoto wao.

Unaweza kuuliza: Matumizi ya washirikina katika mali zao na watoto wao, kwa namna iliyotangulia, yalikuwa ni kwa kutokana na desturi ya wakati wa ujahiliya. Inajulikana kuwa desturi huwekwa na watu. Mmoja wao alikuwa anaweza kuua mwanawe kwa kuogopa ufukara, au akimzika binti yake kwa kuogopa aibu; kama ilivyonasibishwa kwa Qais bin Asim aliyeigwa kwa ujinga. Sasa kuna wajihi gani katika kulinasibisha hilo kwa masanamu au wanaosimamia masanamu?

Jibu: Ni kweli kuwa matumizi ya washirikina yalitokana na desturi, lakini Makuhani na viongozi wao walipendekeza na kuipamba desturi hii, nao ndio wasemaji rasmi wa masanamu, kwa hiyo ikafaa kunasibishwa kwenye masanamu.

Ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao.

Yaani Makuhani waliwapambia washirikina amali zao, ikawa natija ya kupambia huku ni kuangamia washirikina na kupotea kwao na haki na dini iliyonyooka.

Na kama Mwenyezi Mungu angependa wasingalifanya hayo.

Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka kuwazuia hilo kwa nguvu wasingelifanya ubaya huo kwa mali zao na watoto wao, lakini amewaacha kama walivoyo baada ya kuwabainishia njia ya kheri na shari.

Basi waache na haya wanayoyazua ya kutegemeza kwa Mwenyezi Mungu yale wanayoyahalalisha na kuyaharamisha.

Amri ya kuwaacha na uzushi wao, imekuja kwa kuwakemea na kuwapa kiaga washirikina na sio kwa njia yake na uhakika wake; kama vile ilivyo amri katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {40}

“Fanyeni mpendavyo, hakika yeye anayaona myafanyayo.” (41:40)

Baada ya hapo Mwenyezi Mungu anataja katika Aya inayofuatia kwamba washirikina waligawanya mavuno yao na mifugo yao mafungu matatu:

1. Fungu la kwanza: Na husema: Wanyama hawa na mimea hii ni mwiko, hawatokula ila wale tuwapendao - kwa madai yao (tu). Yaani washirikina walikuwa wakigawa sehemu ya mazao na mifugo na kukataza kutumiwa ila kwa wanaowachagua. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubainisha hao waliochaguliwa na washirikina. Lakini baadhi ya wafasiri wamesema, ni makuhani na watumishi wa masanamu. Wengine wakasema ni wanaume tu, sio wanawake.

2. Fungu la pili: Na wanyama wengine imeharamishwa migongo yao, hawapandwi wala kubebeshwa mizigo. Rejea maelezo katika Juz.7 (5:103).

3. Fungu la tatu: Na wanyama wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao wakati wa kuchinja, bali wanataja majina ya waungu wao.

Umetangulia ufafanuzi katika kusafiri Sura hii, Aya ya 121, kuwa wao wamemnasibishia Mwenyezi Mungu kugawanya huku kwa uwongo na uzushi na Mwenyezi Mungu atawaadhibu.

Na husema: waliomo matumboni mwa wanyama hawa ni kwa ajili ya wanaume wetu tu, na wameharamishwa kwa wake zetu. Lakini ikiwa ni nyamafu hushirikiana. Atawalipa kwa maelezo yao. Hakika yeye ni mwenye hekima, Mjuzi.

Razi amesema: “Hii ni aina ya nne katika mambo yao maovu. Walikuwa wakisema katika mimba za Bahira na Saiba: “atakayezaliwa hai basi atahusu wanaume tu, hawali wanawake, na atakayezaliwa maiti basi watashirkiana kumla wanaume na wanawake.” Watalipwa maelezo yao.

Na makusudio ya kiaga cha kuwa. Hakika yeye ni mwenye hekima, Mjuzi ni makemeo yawe kwenye hekima na kwa mujibu wa inavyostahiki.”

Hakika wamehasirika wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya elimu.

Kuna upumbavu gani zaidi ya mzazi kumchinja mwanawe kwa mkono wake au kumzika mzima. Kauli yake Mwenyezi Mungu bila ya elimu ni kusisitiza upumbavu wao. Ama hasara yao katika dunia ni kule kuua watoto wao na ufisadi wa maisha yao ya kijamii. Na hasara yao katika akhera ndiyo nzito na chungu.

Na wakaharamisha alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu katika wanyama na mazao ambayo wamedai kuwa ni mwiko. Kwa kumzulia Mwenyezi Mungu. Kwa sababu kuharamisha kunatokana na wao na wala sio kutoka kwake Mwenyezi Mungu.

Hakika wamepotea wala hawakuwa wenye kuongoka kwenye kheri yoyote na uwongofu.

Razi anasema: “Mwenyezi Mungu ametaja mambo saba na kila moja kati hayo ni sababu tosha ya kupatikana shutuma. Nayo ni: Kupata hasara, upumbavu, ujinga, kuharamisha aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu, kumzulia Mungu, upotevu na kuacha kuongoka.”

Kisha akaendelea kusema Razi: “Imethibiti kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewashutumu wanaowaua watoto na kuharamisha aliyohalalisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sifa hizi saba zenye kuwajibisha aina kubwa na ya mwisho ya shutuma, na huo ni ufasaha wa hali ya juu.”

Nasi tunamwambia Razi: Ikiwa Mwenyezi Mungu amewashutumu kwa upotevu kuwa ndiyo aina kubwa na ya mwisho ya shutuma, sasa vipi wewe unadai kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewapoteza? Ni mantiki gani yanayosema kuwa inafaa asiye na hatia kuadhibiwa na kushutumiwa kwa kitendo ambacho amekifanya yule anayeshutumu na kuadhibu?

Hayo Razi ameyasema mara kadhaa katika tafsir yake Al-Kabir, miongoni mwayo ni yale aliyoyasema karibuni katika kufasiri Aya 125 ya Sura hii.

وَهُوَ الَّذِي أَنْشَأَ جَنَّاتٍ مَعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ ۚ كُلُوا مِنْ ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ ۖ وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ {141}

Naye ndiye aliyeumba bustani zenye kutambaa na zisizotambaa na mitende na mimea yenye kutofautiana uliwaji wake. Na mizaituni na mikomamanga. Inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapozaa. Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msifanye ufujaji, hakika Yeye hawapendi wafujaji.

وَمِنَ الْأَنْعَامِ حَمُولَةً وَفَرْشًا ۚ كُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُبِينٌ {142}

Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko. Kuleni katika alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo za Shetani; hakika yeye ni adui yenu dhahiri.

ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۖ مِنَ الضَّأْنِ اثْنَيْنِ وَمِنَ الْمَعْزِ اثْنَيْنِ ۗ قُلْ آلذَّكَرَيْنِ حَرَّمَ أَمِ الْأُنْثَيَيْنِ أَمَّا اشْتَمَلَتْ عَلَيْهِ أَرْحَامُ الْأُنْثَيَيْنِ ۖ نَبِّئُونِي بِعِلْمٍ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {143}

Namna nane za madume na majike: wawili katika kondoo dume na jike na wawili katika mbuzi dume na jike. Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili, niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli.

وَمِنَ الْإِبِلِ اثْنَيْنِ وَمِنَ الْبَقَرِ اثْنَيْنِ ۗ قُلْ آلذَّكَرَيْنِ حَرَّمَ أَمِ الْأُنْثَيَيْنِ أَمَّا اشْتَمَلَتْ عَلَيْهِ أَرْحَامُ الْأُنْثَيَيْنِ ۖ أَمْ كُنْتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ وَصَّاكُمُ اللَّهُ بِهَٰذَا ۚ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا لِيُضِلَّ النَّاسَ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ {144}

Na wawili katika ngamia na wawili katika ng’ombe. Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? Au nyinyi mlikuweko Mwenyezi Mungu alipowausieni haya? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ili kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.