read

Aya 141 – 144: Kuleni Matunda Yake

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kubainisha katika Aya zilizotangulia, waliyoharamisha katika kilimo na mifugo kwa uzushi, amebainisha katika Aya hizi kwamba yeye ameumba mimea na wanyama binadmau anufaike nayo.

Anasema Mtukufu wa Wasemaji:

Naye ndiye aliyeumba bustani zenye kutambaa inayowekwa matawi yake katika chanja na zisizotambaa na mitende na mimea inaungana na Bustani katika upande wa kuunganisha mahsus kutoka ujumla.

Yenye kutofautiana uliwaji wake

Nafaka ziko aina nyingi na kila moja ina aina yake, na kila aina ina ladha yake. Matunda nayo yako aina kwa aina; yenye rangi tofauti, ladha na hata harufu, vilevile mboga.

Na mizaituni na mikomamanga. Hiyo pia inaungana na bustani. Inayofanana na isiyofanana.

Matunda ya mikomamanga yanafanana, lakini kuna yaliyo tamu na yaliyo ugwadu. Vilevile matunda ya jamii ya malimau na mizaituni; kuna mazuri na mabaya.

Kuleni matunda yake inapozaa.
Kwa sababu imeumbwa kwa ajili yenu.

Na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake.

Imesemekana kuwa makusudio ya haki yake ni Zaka. Wengine wakasema kuwa ni sadaka ya Sunna. Lakini, kauli zote mbili ni kinyume na dhahiri.

Linalokuja haraka kwenye akili ni kukusanywa na wala yasiachwe yakaharibika na kupotea.

Wala msifanye ufujaji, hakika Yeye hawapendi wafujaji.

Ufujaji (Israf) ni kupetuka kiwango, na Mwenyezi Mungu amelikataza hilo: ni sawa iwe ni kutumia mtu mwenyewe, au kumpa mwingine.

Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko.

Yaani ameumba katika wanyama wanaowabeba nyinyi na kubeba mizigo yenu; kama vile ngamia. Na wale mnaowachinja na kunufaika kwa nyama yake manyoya na sufi zake.

Kuleni katika alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu,

kama vile wanyama hawa na wengineo na mshukuru neema zake.

Wala msifuate nyayo za Shetani, kwa kuhalalisha aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, na kuharamisha aliyoyahalalisha, na pia kufanya ubadhirifu.

Hakika yeye ni adui yenu dhahiri. Anawaamrisha uovu na kusema kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Namna nane za madume na majike: wawili katika kondoo dume na jike na wawili katika mbuzi dume na jike. Sema je, ameharamisha madume mawili ya kondoo na mbuzi au majike mawili, ya kondoo na mbuzi? Au waliomo matumboni mwa majike mawili ya kondoo na mbuzi?

Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli sio kwa hawa za nafsi na kufuata mnavyoambiwa tu, kwa sababu kuharamisha kunahitajia dalili mkato; sasa je, iko wapi?

Na wawili katika ngamia na wawili katika ng’ombe. Sema je, ameharamisha madume mawili au majike mawili, au waliomo matumboni mwa majike mawili? Au nyinyi mlikuweko Mwenyezi Mungu alipowausieni haya?

Walidai kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaharamishia waliowa- haramisha katika wanyama na mimea. Ndipo akawaambia kuwa jambo halithibitiki ila kwa mojawapo ya hali mbili. Ama kwa kuona au kwa kushuhudia shahidi mkweli. Na nyinyi hamkupata hukumu ya uharamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja au kupitia kwa Mtume wake; basi mmezitoa wapi hukumu hizi?

Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo?

Ikiwa hamkuona, wala hakuna ushahidi wowote, basi nyinyi mtakuwa wazushi. Na mzushi ni dhalimu mwenye dhambi. Bali nyinyi ni madhalimu kuliko dhalimu yeyote, kwa sababu mnamzulia Mwenyezi Mungu uwongo.

Ili kuwapoteza watu bila ya ilimu.

Akiwazuia kufuata njia ya Mwenyezi Mungu na wakati huo huo anadai kuwa yeye ni kiongozi wa dini ya Mwenyezi Mungu; kama walivyo masheikh wengi siku hizi.

Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.
Kwa sababu wao wamekata uhusiano na Mwenyezi Mungu. Isitoshe wameharamisha aliyoyahalalisha na kuhalalisha aliyoyaharamisha.

قُلْ لَا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَنْ يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنْزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّهِ بِهِ ۚ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ رَبَّكَ غَفُورٌ رَحِيمٌ {145}

Sema: Sioni katika niliyopewa wahyi kilichoharamishiwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hivyo ni uchafu; au kwa uharamu, kimetajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, mweye kurehemu.

وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا كُلَّ ذِي ظُفُرٍ ۖ وَمِنَ الْبَقَرِ وَالْغَنَمِ حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ شُحُومَهُمَا إِلَّا مَا حَمَلَتْ ظُهُورُهُمَا أَوِ الْحَوَايَا أَوْ مَا اخْتَلَطَ بِعَظْمٍ ۚ ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُمْ بِبَغْيِهِمْ ۖ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ {146}

Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila mwenye kucha. Na katika ng’ombe na mbuzi na kondoo tukawaharamishia mafuta yao; isipokuwa yale iliyobeba migongo yao, au matumbo, au iliyochanganyika na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na hakika sisi ndio wakweli.

فَإِنْ كَذَّبُوكَ فَقُلْ رَبُّكُمْ ذُو رَحْمَةٍ وَاسِعَةٍ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُهُ عَنِ الْقَوْمِ الْمُجْرِمِينَ {147}

Wakikukadhibisha, basi sema: Mola wenu ana rehema nyingi; wala adhabu yake haizuiliwi kwa watu waovu.