read

Aya 145 – 147: Sioni Katika Niliyopewa Wahyi

Maana

Sema: Sioni katika niliyopewa wahyi kilichoharamishiwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni mzoga au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe, kwani hivyo ni uchafu; au kwa uharamu, kimetajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kubainisha uzushi wa washirikina kwa Mwenyezi Mungu, katika vyakula walivyoharamisha na kuhalalisha, kati- ka Aya hii anabainisha vilivyoharamishwa na Mwenyezi Mungu kuliwa.

Navyo ni vinne: Mfu, damu yenye kutirizika, nyama ya nguruwe na kilichotajiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu; yaani aliyechinjwa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Haifai kwa yeyote kula chochote katika hivyo ila akiwa amelazimika; katika hali hiyo anaruhusiwa kula kiasi kile kitakachoweza kuzuia madhara ya nafsi yake tu. Umetangulia ufafanuzi wa hayo katika kufasiri Juz.2 (2: 173.) Huko tumejibu swali la mwenye kuuliza, kuwa inaonyesha vilivyo haramu ni hivi vinne tu, lakini tunaelezewa vingi. Vilevile umetangulia ufafanuzi zaidi katika Juz.6 (5:3).

Na kwa wale walio Mayahudi tuliharamisha kila mwenye kucha.

Katika Aya iliyotangulia, Mwenyezi Mungu ameharamisha aina zilizotajwa kwa watu wote, Mayahudi na wasiokuwa Mayahudi. Ama vilivyoharamishwa, katika Aya hii, vinawahusu Mayahudi tu, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kwa wale walio Mayahudi tuliharamisha:

Kwanza ni, kila mwenye kucha; yaani wote wenye kucha bila ya kuacha wengine. Tabari katika Tafsir yake anasema: “Mwenye kucha katika wanyama na ndege ni ambaye vidole vyake havikuachana; kama vile ngamia, mbuni na bata.”
Pili, Na katika ng’ombe na mbuzi na kondoo tukawaharmishia mafuta yao.

Mwenyezi Mungu hakuwaharamishia sehemu yote ya nyama ya ng’ombe na mbuzi na kondoo,ispokuwa nyama nyeupe tu sio nyekundu. Na pia katika hiyo amevua kwa kusema:

Isipokuwa yale iliyobeba migongo yao. Yaani mafuta yaliyogandana na mgongo.

Au matumbo yaani mafuta yanayogandamana na utumbo.

Au iliyochanganyika na mifupa nayo ni mafuta ya mkia kulingana na wafasiri wote waliokuwako wakati wa Razi. Na mfupa uliochanganyika na na mafuta ya mkia ni kifandugu.

Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na hakika sisi ndio wakweli.

Hii ni kubainisha sababu ya kuharamishiwa mayahudi vitu hivi vizuri, na kwamba hivyo ni malipo ya makosa yao yasiyo na idadi, yakiwemo kuua mitume, kula mali za watu kwa batili, kusema kwao mikono ya Mwenyezi Mungu imefumba na mengineyo. Tazama Juz.4 (3:93).

Wakikukadhibisha, basi sema: Mola wenu ana rehema nyingi; na adhabu yake haizuiliwi (kuwafikia) watu waovu.

Yaani wakikukadhibisha Ewe Muhammad, basi usiwakatishe tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na uwaambie kuwa mkitubia, basi Mwenyezi Mungu atawakubali na atawasamehe; kama ambavyo atawaadhibu mkiendelea na mliyo nayo.

Katika Aya hii kuna ahadi na kiaga kikali. vilevile radhi ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake: Radhi yake ni kwa atakayekimbilia kwake akitaka msamaha na ghadhabu yake ni kwa atakayeendelea na uasi. Mwenyezi Mungu anasema:

لَئِنْ شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِنْ كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ {7}

“Mkishukuru, nitawazidishia; na mkikufuru (jueni) kuwa adhabu yangu ni kali” (14:7)

سَيَقُولُ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِنْ شَيْءٍ ۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ حَتَّىٰ ذَاقُوا بَأْسَنَا ۗ قُلْ هَلْ عِنْدَكُمْ مِنْ عِلْمٍ فَتُخْرِجُوهُ لَنَا ۖ إِنْ تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ أَنْتُمْ إِلَّا تَخْرُصُونَ {148}

Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelimshirikisha sisi wala baba zetu; wala tusingeliharamisha chochote. Kama hivi walikadhibisha waliokuwa kabla yao mpaka wakaonja adhabu yetu. Je, mnayo elimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana tu, na hamsemi ila uwongo tu.

قُلْ فَلِلَّهِ الْحُجَّةُ الْبَالِغَةُ ۖ فَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ {149}

Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye mwenye hoja ikomeshayo. Na kama angelitaka angeliwaongoza nyote.

قُلْ هَلُمَّ شُهَدَاءَكُمُ الَّذِينَ يَشْهَدُونَ أَنَّ اللَّهَ حَرَّمَ هَٰذَا ۖ فَإِنْ شَهِدُوا فَلَا تَشْهَدْ مَعَهُمْ ۚ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ وَهُمْ بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ {150}

Sema: Leteni mashahidi wenu wanaoweza kushuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameharamisha haya. Basi wakitoa ushahidi, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala usifuate matamanio ya wale waliozikadhibisha ishara zetu na wale wasioamini Akhera, na ambao humlinganisha Mola wao.