read

Aya 148 – 150: Angelitaka Mwenyezi Mungu Tusingelishirikisha

Maana

Watasema walioshirikisha: Lau angelitaka Mwenyezi Mungu tusingelimshirikisha sisi wala baba zetu; wala tusingeliharamisha chochote.

Wanaokubali nasaha na kufuata kauli nzuri ni wachache sana; na wanaokubali makosa yao ni wachache zaidi. Kwani wengi wanaona makosa yao ndiyo mambo bora na maovu yao kuwa ni mema.

كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْمُسْرِفِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {12}

“… Namna hii wamepambiwa wale wapitao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda,” (10:12).

Wanaposhindwa kuboresha uovu wao wanajivua na kusema kuwa ni matakwa ya Mwenyezi Mungu au sababu yoyote nyingine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametakata na hayo wanayomsifu nayo. Yeye anawaamrisha na kuwakataza, na kuwafanya wawe na hiyari katika wanayoyafanya na kuyaacha. Ili aangamie mwenye kuangamia kwa dalili zilizo dhahiri na apone yule atakayepona kwa dalili zilizo dhahiri. Wala hakuna yeyote mwenye mamlaka kwa mwingine; hata shetani atasema siku itakapokatwa hukumu:

إِنَّ اللَّهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدْتُكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ ۖ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُمْ مِنْ سُلْطَانٍ إِلَّا أَنْ دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي ۖ فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوا أَنْفُسَكُمْ ۖ {22}

“Hakika Mwenyezi Mungu aliwaahidi ahadi ya kweli, nami nikawaahidi, lakini sikuwatimizia. Wala sikuwa na mamlaka juu yenu isipokuwa niliwaita tu, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu, bali jilaumuni wenyewe … (14:22).

Katika Aya hii tuliyonayo, Mwenyezi Mungu anasimulia madai ya washirikina kuwa shirki yao na shirk ya mababa zao na kuharamisha kwao mimea na wanyama, ilitokana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na amri yake. Lau angelitaka wasishirikishe angeliwazuia na shirk.

Kama hivi walikadhibisha waliokuwa kabla yao mpaka wakaonja adhabu yetu.

Yaani washirikina wa Kiarabu walimkadhibisha Muhammad (s.a.w.), aliyewakataza ushirikina na kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo; sawa na walivyokadhabisha Mitume wale waliokuwa kabla yao; na hawakuwasadiki mpaka baada ya kuteremshiwa adhabu ya malipo ya kukadhibisha kwao.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusimulia madai ya washirikina, na mababu zao, alimwamrisha Mtume wake kuwajibu kwa swali litakalowazima na kubatilisha madai yao nalo ni:

Je, mnayo elimu mtutolee?

Makusudio ya elimu hapa ni dalili. Hiyo ni katika kutumia chenye kus- ababisha kuwa ndio sababu. Kwa sababu dalili ndiyo sababu ya kupatikana elimu.

Makusudio ya swali hili ni kudhihirisha uwongo wao na kushindwa kwao.

Kwa sababu maana yake ni kuwa nyinyi washirikina! Mmedai shirk ilikuwa ni kwa kuridhia kwake Mwenyezi Mungu; sasa ni nani basi aliyewaambia haya?

Kutoka wapi mmejua matakwa yake Mwenyezi Mungu Mtukufu? Hiyo ni katika siri zake Mwenyezi Mungu wala hamdihirishii siri yake ila Mtume wake aliyemridhia. Na Mtume hakuwaambia haya nyinyi wala wengineo. Kwa hiyo vipi mnafanyia hila Mwenyezi Mungu?

Nyinyi hamfuati ila dhana tu, na hamsemi ila uwongo tu.

Sisi hatuna shaka kwamba wakubwa wa waasi wanajua kuwa wao ni waongo katika wanayoyasema; isipokuwa wanaysema kwa kuifanyia inadi haki ambayo inaipomosha batili yao na kumaliza malengo yao na matendo yao ya uadui.

Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye mwenye hoja ikomeshayo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amebainisha katika Aya iliyotangulia kuwa washirikina hawana hoja ya madai yao isipokuwa dhana na uwongo. Katika Aya hii amebainisha kuwa hoja inayokomesha ni ya Mwenyezi Mungu pekee yake, juu yao na juu ya wengine. Maana ya kuwa inakomesha ni kwamba ina nguvu ya kukomesha nyudhuru zote.

Na kama angelitaka angeliwaongoza nyote.

Katika kufasiri Juz.1 (2: 26), tumetaja kuwa Mwenyezi Mungu ana matakwa mawili: Matakwa ya kuumba ambayo yanakuwa katika ibara yake “Kuwa na ikawa” (kun fayakun) na Matakwa ya kuweka sharia, ambayo ni amri zake na makatazo yake.

Na Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaumba ulimwengu kwa matakwa yake ya kuumba na hajiingizikama sikosei - katika matakwa haya kwenye mambo ya watu ya kijamii; bali huweka sharia na mwongozo.

Maelezo haya ndiyo yanatufafanulia maana ya kauli yake. ‘Na kama angelitaka angeliwaongoza nyote’. Yaani lau angelitaka kujiingiza katika mambo yenu ya kijamii kwa matakwa ya neno “Kuwa ikawa” (ya kuumba), basi mngeliamini nyote. Lakini yeye hafanyi hivyo. Kwa sababu lau angelifanya hivyo ingelibatilika taklifu na kusingekuwapo thawabu na adhabu.

Tunarudia kusema tena kuwa washirikina walidai kuwa shirki yao ilikuwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aka- batilisha madai yao haya kuwa ni madai yasiyo na dalili. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hajiingizi katika mambo ya watu kwa matakwa ya kuumba.

Lau tukichukulia kuwa Mwenyezi Mungu anajiingiza katika mambo hayo, basi kwa hali ilivyo angeliwaelekeza kwenye imani ya umoja wake na sio kwenye uasi, ukafiri na ushirikina.

Sema: Leteni mashahidi wenu wanaoweza kushuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameharamisha haya.

Washirikina walimzulia Mwenyezi Mungu uwongo katika kuharamisha waliyoyaharamisha katika mimea na wanyama; vilevile walimzulia katika kunasibisha shirki yao kwake. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha Mtume wake Muhammad, katika Aya ya kwanza, kuwambia kuwa kama wanayo dalili waitoe.

Katika Aya ya pili akamwamrisha kuuwaambia kuwa dalili mkataa ni ya Mwenyezi Mungu tu, si yenu. Kisha katika Aya hii amemwamrisha kuwaambia nionyesheni anayeshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu amewapa wahyi moja kwa moja au kupitia kwa Mtume miongoni mwa Mitume yake kuwa yeye ameharamisha mliyoyaharamisha. Kwa sababu kushuhudia haki kuna sharti la kuweko elimu yenye kuondoa shaka na dhana. Wala hakuna nyenzo ya kujua yaliyoharamishwa na yaliyohalalishwa ila Wahyi tu; basi mleteni atakeyelishuhudia hilo.

Basi wakitoa ushahidi, wewe ushishuhudie pamoja nao.

Katazo hili ni fumbo la uwongo wao katika ushahidi wao. Kwa sababu ni muhali mtume kushuhudia pamoja na washirikina. Na fumbo ni fasaha zaidi kuliko ufafanuzi.

Wala usifuate matamanio ya wale waliozikadhibisha ishara zetu na wale wasioamini Akhera, na ambao humlinganisha Mola wao.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwahukumia uwongo na uzushi, anabainisha sababu ya hukumu yake hiyo kwa mambo matatu: Kwanza, kuwa wao wanafuata hawaa na matamanio. Hilo ameliletea ibara ya:

Wala usifuate matamanio ya wale waliokadhibisha ishara zetu, kwa sababu ni muhali kwa Mtume kumfuata anayekadhibisha utume wake.

Pili, kwamba wao ni wale wasioamini Akhera; na asiyeamini Akhera hao- gopi mwisho wa uwongo.

Tatu, kwamba wao Humlinganisha Mola wao. Yaani wanamfanya kuwa ana wa kulingana naye katika kuumba. Na yeyote anayemshirikisha Mwenyezi Mungu haukubaliwi ushahidi wake, sababu yeye amefanya madhambi mabaya zaidi.

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ مِنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {151}

Sema: Njooni niwasomee aliyowaharamishia Mola wenu: Kwamba msimshirikishe na chohote. Na kuwafanyia wema wazazi wawili. Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa sisi tutawaruzuku nyinyi na wao. Wala msikurubie mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika; wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha (kuiua), ila kwa haki. Hayo amewausia Mwenyezi Mungu ili mpate kutia akili.

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {152}

Wala msiikurubie mali ya yatima isipokuwa kwa njia bora zaidi. Mpaka afikie kukomaa kwake. Na kamilisheni vipimo vya ujazo na uzani kwa uadilifu. Hatuikalifishi nafsi ila kwa uweza wake Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa. Na tekelezenim ahadi ya Mwenyezi Mungu. Haya ameusiwa ili mpate kukumbuka.

وَأَنَّ هَٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَنْ سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ {153}

Na kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni wala msifuate njia nyingine zikawatenga mbali na njia yake (Mwenyezi Mungu). Hayo amewausia ili muwe na takua.