read

Aya 154 – 157: Kisha Tulimpa Musa Kitab

Maana

Kisha tulimpa Musa Kitab.

Wameduwaa wafasiri kuhusu neno ‘Kisha’. Kwa sababu mazungumzo ni ya Qur’an katika Aya zilizotangulia. Na Aya hii inazungumzia Tawrat iliyoshuka kabla ya Qur’an; na ‘Kisha’ inafahamisha kuja nyuma ya kilicho kabla yake kwa wakati. Sasa imekuwaje itajwe Qur’an kisha Tawrat na iliyoanza ni Tawrat?

Razi ametaja njia tatu, na Tabrasi akazidisha ya nne. Sisi hatuoni jambo lolote la kurefusha maneno hapo. Kwa sababu mpangilio hapa ni wa maneno sio wa wakati, na uunganisho ni wa habari kuungana na habari nyingine sio maana kuungana na maana nyingine.

Kumtimizia yule aliyefanya wema.

Yaani tumempa Musa Kitab nacho kinatimiza upungufu wa aliyefanya wema, kunafaika nacho; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ {3}

“Leo nimewakamilishia dini yenu na kuwatimizia neema yangu na nimewapendelea Uislamu kuwa dini.” (5:3)

Na kuwa ni ufafanuzi wa kila kitu.

Hii ni sifa ya pili ya Kitab cha Musa (a.s.) kwamba kimekusanya hukumu zote walizozitaja watu wa wakati ule. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: “Na tukamwandikia katika mbao mawaidha ya kila kitu na ufafanuzi wa kila kitu” (7:144).

Na mwongozo na rehema.

Sifa mbili nyingine za Kitab cha Musa. Kwa mwongozo, watu watajua haki na kheri, na kwa rehema, watu wataishi maisha ya utulivu.

Ili wapate kuamini kukutana na Mola wao.

Dhamiri inawarudia waisrael, kwa maana tumempa Musa Kitab kilichokusanya sifa zilizotajwa, ili watu wake wamwamini Mwenyezi Mungu na thawabu zake na adhabu yake. Lakini wao waling’ang’ania inadi yao, na wakasema miongoni mwa waliloyasema:

يَا مُوسَىٰ لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ نَرَى اللَّهَ جَهْرَةً {55}

“Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mungu waziwazi” Juz.1 (2:55).

Tukadrie kama wangemwona Mwenyezi Mungu waziwazi - na kukadiria muhali si muhali - basi wao wangesema kuwa huyu si Mola, kwa vile yeye si pauni wala dola.

Na hii ni Kitab tulichokiteremsha kilichobarikiwa na baraka.

Hii ni Qur’an tukufu, nayo ni yenye baraka kwa sababu ina kheri na manufaa mengi.

Basi kifuateni na muwe na takua ili mrehemiwe.

Fuateni aliyowaamrisha na muache aliyowakataza ili iwaenee rehma yake duniani na akhera.

Msije mkasema kuwa vitabu viliteremshiwa makundi mawili tu, yaliyokuwa kabla yetu nasi tulikuwa hatuna habari ya yale waliyoyasoma.

Wanaambiwa washirikina wa Kiarabu. Makusudio ya vitabu ni Tawrat na Injil; na makundi mawili ni watu wa Kitab: Mayahudi na Manaswara (Wakristo).

Maana ni kuwa enyi Waarabu, tumewateremshia Qur’an kwa lugha yenu na kwa mtu wenu anayetokana nanyi ili msiwe na udhuru wa shirki yenu, kwamba hakikuteremshwa Kitab kwa lugha yenu na kuwa hamkujua kuk- isoma na kujifundisha mafunzo yake.

Au mkasema: Lau tungeliteremshiwa Kitab bila shaka tungelikuwa woaongofu zaidi kuliko wao.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu anawaondolea udhuru wa lugha, na katika Aya hii anawaondolea udhuru wa kufikiwa na Kitabu chenyewe. Kwa ufupi ni kuwa Aya hii na iliyo kabla yake inafanana na kauli ya asemaye: “Fulani ni tajiri na mimi sina chochote, lau ningekuwa na kitu basi ningelifanya mengi.” Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa jawabu mkataa:
Basi imewafikia hoja kutoka kwa Mola wenu, na uwongofu na rehema.

Makusudio ya hoja ni Qur’an, ndani yake mna dalili na ubainifu wa kumsadikisha Muhammad (s.a.w.). Vilevile mna hukumu na mafunzo yenye kuwatoa watu kwenye giza kwenda kwenye mwanga.

Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezikadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na akajitenga nazo?

Hakuna kabisa dhalimu mkubwa wa nafsi yake na watu kuliko yule anayekana haki na kheri, akahangaika katika dunia kufanya ufisadi na kupinga njia ya Mwenyezi Mungu.

Tutawalipa wale wanaojitenga na ishara zetu adhabu mbaya kwa sababu ya kule kujitenga kwao.

Ishara za Mwenyezi Mungu ni hoja zake na dalili zake. Maana ni kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amesimamisha dalili na hoja mkataa juu ya umoja wake na juu ya utume wa Muhammad na ukweli wa aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake, lakini washirikina walipinga wakakataa kuzingatia vizuri hoja hizo kwa kuifanyia inadi haki na watu wa haki. Kwa hiyo wakastahiki hizaya na adhabu kali.

هَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا أَنْ تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ ۗ يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنْفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِنْ قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ قُلِ انْتَظِرُوا إِنَّا مُنْتَظِرُونَ {158}

Je, wananogoja jingine ila wawafikie Malaika au afike Mola wako au ziwafikie baadhi ya ishara za Mola wako? Siku zitakapofika baadhi ya ishara za Mola wako, basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.Sema: Ngojeni , sisi pia tunangoja.

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُمْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ {159}

Hakika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote. Hakika shauri lao liko kwa Mwenyezi Mungu tu. Kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya.

مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَنْ جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ {160}

Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu. Nao hawatadhulumiwa.