read

Aya 158 – 160: Haitamfaa Mtu Ila Imani Yake

Maana

Je, wananogoja jingine ila wawafikie Malaika au afike Mola wako au ziwafikie baadhi ya ishara za Mola wako?

Swali hapo si la kuuliza bali ni la kukanusha. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kwamba washirikina wamekana dalili za Qur’an, wakakataa kuzingatia maana yake, sasa anasema katika Aya hii kuwa wao hawataamini isipokuwa mambo matatu: Kuja Malaika, kuja Mola na kuja baadhi ya ishara. Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakubainisha Malaika ambaye anapasa kuwajia ili waamini.

Je, ni Malaika wa mauti au mwingine? Wala pia hakubainisha makusudio ya kuja Mola. Je, ni kuja kwake kwa madai yao au ni kuja amri yake, kama ilivyotokea? Vilevile hakubainisha baadhi ya ishara. Je, ni ishara walizozitaka au ni alama za Kiyama?
Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya Malaika ni Malaika wa mauti. Na makusudio ya kuja Mola ni kuja adhabu na mateso yake. Na baadhi ya ishara, ni ishara za Kiyama.

Tafsir hii ndiyo iliyo karibu zaidi na maana. Kwa sababu, maneno yanayofuatia yanataja mambo haya matatu yakitambulisha kauli ya wafasiri na kuitilia nguvu; nayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Siku zitakapofika baadhi ya ishara za Mola wako, basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchuma kheri kwa imani yake.

Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba toba na imani wakati wa kuja mojawapo ya mambo haya matatu, haifai kitu; isipokuwa inayofaa ni imani na amali njema anayoichuma mumin kabla ya kutokea hayo. Kwani wakati wa kutolewa roho, au ishara za Kiyama au wakati wa kushuka adhabu huwa hakuna taklifa yoyote. Ikiwa hivyo, basi kuweko imani na kutokuweko ni sawa tu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu: Au kuchuma kheri kwa imani yake, inaishiria kuwa kumwamini Mungu kunamwokoa mtu na kukaa milele tu motoni, lakini hakumwokoi na adhabu ya moto. Ama anayemwamini Mwenyezi Mungu na akafanya amali njema, basi hataguswa na moto.

Sema: Ngojeni haya mambo matatu, sisi pia tunangoja.

فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَنْ يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ {39}

“Punde tu mtajua ni nani itakayemjia adhabu ya kufedhehesha” (11:39).

Hakika wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, huna uhusiano nao wowote.

Hapa anaambiwa Mtume (s.a.w.).

Kama ambavyo walihitalifiana wale walioigawa dini yao na wakawa makundi makundi, vilevile wafasiri nao wamekuwa makundi makundi katika kufasiri makusudio ya ‘walioigawa dini yao.’ Baadhi wamesema kuwa hao ni washirikina kwa kuwa baadhi yao wanaabudu masanamu, wengine nyota na baadhi yao mwanga na giza. Wafasiri wengine wamesema kuwa ni watu wa Kitab.

Kwani Mayahudi waligawanyika makundi ya Masadukayo, Mafarisayo na Mahaasid1 Ama Wakristo wao waligawanya kanisa la Mashariki na la Magharibi.

Pia imesemekana kuwa ni makundi ya Kiislamu. Na ikasemekana kuwa ni wote wenye mila na vikundi.

Maelezo bora niliyosoma kuhusu tafsir ya Aya hii ni yale aliyosema mwenye tafsir Al-Manar: “Makusudio ya wale walioigawa dini yao wakawa vikundi ni watu wa Kitab. Na makusudio ya kujitenga nao Mtume ni kuhadharishwa Waislamu wasigawanye dini yao wakawa na vikundi kama watu wa Kitab, ili wajue kwamba wao wakifanya vitendo vya watu wa Kitab, basi Muhammad (s.a.w.) atakuwa mbali nao.”

Hakika shauri lao liko kwa Mwenyezi Mungu tu. Yeye peke yake ndiye anayemiliki hisabu na adhabu ya mwenye kufarikisha waja wake na kuleta uadui na chuki katika dini na penginepo.

Kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya. Kuanzia wale watakaokubali mpaka wale wanaochochea:

وَقَالَتْ أُولَاهُمْ لِأُخْرَاهُمْ فَمَا كَانَ لَكُمْ عَلَيْنَا مِنْ فَضْلٍ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْسِبُونَ {39}

“Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao; basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma.” (7:39)

Mwenye kufanya vizuri atalipwa mfano wake mara kumi. Na mwenye kufanya vibaya hatalipwa ila sawa na hivyo tu. Nao hawatadhulumiwa.

Kila lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na manufaa kwa watu basi ni zuri; na kila lenye machukivu ya Mwenyezi Mungu na ufisadi kwa watu basi ni baya.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mwadilifu, mkarimu. Miongoni mwa uadilifu wake ni kumlipa mwenye kufanya uovu, adhabu inayolingana nao. Na miongoni mwa ukarimu wake ni kusamehe, na kumwongozea mtenda mema ziada inayofikia kumi, au mia saba, au isiyo na idadi kulingana na lengo la mtenda mema, sifa zake na hali yake. Angalia Juz 2. (2:261).

Kuna Hadith ya Mtume (s.a.w.) isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu amesema: “Wema malipo yake ni kumi au zaidi, na uovu ni moja au kusamehewa. Basi ole wake yule ambaye kumi yake imeshindwa na moja yake”.

Anaendelea kusema Mtume: “Mwenyezi Mungu anasema: ‘Mja wangu akikusudia wema mwandikieni jema moja hata kama hatafanya; na akifanya basi mwandikieni kumi mfano wake. Kama atakusudia uovu, msimwandikie kitu; kama ataufanya basi mwandikieni moja.”

قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ {161}

Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza katika njia iliyonyooka, dini yenye msimamo ndiyo mila ya Ibrahim mnyoofu. Wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ {162}

Sema: Hakika Swala yangu na ibada zangu na uhai wangu na mauti yangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ {163}

Hana mshirika. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.

قُلْ أَغَيْرَ اللَّهِ أَبْغِي رَبًّا وَهُوَ رَبُّ كُلِّ شَيْءٍ ۚ وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ مَرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُمْ بِمَا كُنْتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ {164}

Sema: Je, nimtafute Mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Na hali yeye ni Mola wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila (inajichumia) yenyewe. Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu, naye atawaambia yale mliyokuwa mkihitalifiana.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ الْأَرْضِ وَرَفَعَ بَعْضَكُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ لِيَبْلُوَكُمْ فِي مَا آتَاكُمْ ۗ إِنَّ رَبَّكَ سَرِيعُ الْعِقَابِ وَإِنَّهُ لَغَفُورٌ رَحِيمٌ {165}

Naye ndiye aliyewafanya makhalifa wa ardhi na akawainua baadhi yenu juu ya wengine ili awajaribu katika aliyowapa. Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu. Na hakika yeye ni mwingi wa maghufira, mwenye huruma.
  • 1. Miongoni mwa kauli za wa mafarisayo ni kuwa wafu watarudi kwenye dunia hii washiriki katika ufalme wa Masih atakayekuja. Katika kauli za wa masadukayo ni kuwa hakuna uhai kabisa baada ya kufa si duniani wala akhera. Na miongoni mwa kauli za wa Haasid ni usawa baina ya watu. Soma Kitabu kiitwacho Asfar Muqaddasa cha Aliy Abdul Wahid Wafi.