read

Aya 161 – 165: Sema Mola Wangu Ameniongoza

Maana

Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu ameniongoza katika njia iliy- onyooka.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwataja wale walioigawanya dini yao wakawa vikundi, alimwamrisha Mtume wake kuwatangazia washirikina, watu wa Kitab na wengineo kuwa Mwenyezi Mungu amemwongoza Mtume kwa umbile safi, akili kamili na kwa wahyi utokao kwake, kwenye njia inayomweka mbali na batili na kumfikisha kwenye dini yenye msimamo ndiyo mila ya Ibrahim mnyoofu. Yaani njia ambayo Mwenyezi Mungu amemuongoza nayo Mtume wake Muhammad ndiyo dini ya Nabii Ibrahim (a.s.) kipenzi cha Mwenyezi Mungu ambayo wanaitukuza watu wa dini zote.

Wala hakuwa miongoni mwa washirikina .

Bali ni katika maadui wakubwa wa ushirikina na watu wake. Hili ni jibu la Washirikina wa Kiquraish ambao wanadai kwamba wao wako kwenye dini ya Nabii Ibrahim (a.s.).

Sema: Hakika Swala yangu na ibada zangu na uhai wangu na mauti yangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.

Maudhui ya Aya iliyotangulia ni misingi ya dini na itikadi kwa kulinganisha na neno: ‘Wala hakuwa miongoni mwa washirikina’ na maudhui ya Aya hii ni matawi ya dini na sharia, kwa kulinganisha Swala na ibada.

Kuunganisha ibada kwenye Swala ni katika hali ya kuunganisha ujumla kwenye mahsusi; kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَالنَّبِيُّونَ مِنْ رَبِّهِمْ {84}

“Na waliyopewa Musa na Isa na Mitume kutoka kwa Mola wao” (3:84)

Uhai na mauti hapa ni fumbo la uthabiti na kuendelea. Maana ni kuwa ibada za Muhammad (s.a.w.) na maisha yake yote ya kiitikadi, nia na amali, yanaekelea kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala hakengeuki nayo mpaka kufa.

Hana mshirika. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.

Aya hii ni ufafanuzi na usisitizo wa yaliyo katika Aya iliyotangulia – Tawhid na ikhlasi. Na Muhaammad ni Mwislamu wa kwanza katika umma wake kwa sababu yeye ndiye mwenye wito huo.

Sema: Je, nimtafute Mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?

فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّهِ ۚ {115}

Atakayemtafuta Mola huyo atampata wapi, na hali: “Mahala popote mnakoelekea ndiko kwenye uelekeo wa Mwenyezi Mungu?”Juz. 1 (2:115)

Na hali yeye ni Mola wa kila kitu?

Na Mola wa kila kitu ni mmoja tu, hana wa kinyume chake.

Kila Mtu Na Mzigo Wake

Na kila nafsi haichumii ila (inajichumia) yenyewe.

Kila alifanyalo mtu liwe kheri au shari basi ni mazao ya silika yake na hali yake kwa ujumla. Anayenasibisha matendo ya mtu kwa mwingine, ni sawa na anayemnasibisha mtoto kwa asiyekuwa mama yake, na matunda kwa usiokuwa mti wake.

Wala mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine.

Makusudio ya mzigo hapa ni dhambi. Jumla hii inatilia mkazo jumla iliyo kabla yake, na maana yake ni kwamba:

لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ {286}

“Faida ya yale iliyoyachuma ni yake na hasara iliyochuma ni yake.” Juz. 2 (2:286).

Sio yaliyochumwa na nafsi nyingine.

Hii ndiyo asili ya kidini na kiakili; haiwezekani kuifuta au kuigeuza. Maulama wa lugha na fasaha wametoa masuala mengi na hukumu kwenye asili hii.

Utauliza: Aya hii inaonyesha kuwa kila mtu na lake tu, sasa uko wapi wajibu wa Jihadi, kutoa nasaha na kusaidiana katika wema na takua.

Jibu: Maadhui ya Aya hii yanahusiana na adhabu tu, na kwamba mtu hataadhibiwa kwa kosa la mwingine; wala haina uhusiano wowote na jihadi na nasaha na mengineyo, kwa umbali au karibu. Kwa sababu kuadhibiwa kwa kosa la mwingine ni jambo mbali na wajibu wa jihadi na kurekebisha ufisadi ni jambo jengine.

Swali la pili: watu wamezoea kutoa sadaka ya mali na chakula kwa ajili ya roho za maiti wao; wakasoma Qur’an na kuwapelekea thawabu; je, hii inajuzu kisharia? Na je, maiti wananufaika nayo. Kama ni hivyo, itakuwaje na ilivyo ni kuwa wafu hawaadhibiwi kwa maovu ya walio hai, basi iwe pia wasineemeke na mema yao?

Jibu: Tumesema kuwa akili na sharia inakataa kuadhibiwa mtu kwa kosa la mtu mwingine na kushirikishwa kwenye kosa hilo. Kuhusu thawabu, katika mtazamo wa akili, hakuna kizuizi kwa aliyefanya wema kumshirikisha asiyefanya wema ule katika thawabu anazostahiki kwa amali yake.

Na sharia imelieleza hilo, hivyo imepasa kulisadiki. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) anasema: “Mwanadamu akifa, hukatika amali yake isipokuwa mambo matatu: Sadaka inayoendelea, au elimu inayopatiwa manufaa, au mtoto mwema atakayemwombea, dua?” Akaendelea kusema: “Atakayekufa na ana saumu anayodaiwa basi na amfungie walii wake”.

Akasema tena: “Mwenye kuingia makaburini akasoma Sura ya Yasin huwahafifishia waliozikwa hapo siku hiyo. Na anapata wema kwa idadi ya waliomo makaburi.” Imam Jafar As-sadiq (a.s.) naye anasema: “Ni jambo gani linalomzuia mtu kuwafanyia wema wazazi wake mara kwa mara?”

Kwa hiyo Hadith hizi na nyinginezo zinafahamisha kwamba maiti ananufaika kwa kupelekewa thawabu kwa amali ya kheri. Na akili hailikatai hilo kabisa. Kwa sababu hilo linaafikiana na fadhila za Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.

Lakini watu wamezidisha mno na kupetuka mipaka ya ilivyoelezwa. Na mafakihi wameafikiana kuwa kila mwenye kufanya ambalo halikuelezewa kwa makusudio ya kuwa linatiliwa mkazo na sharia basi amefanya uzushi (bid’a) katika dini na amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa hiyo ni bora ampelekee thawabu maiti kwa kutarajia anufaike nazo, bila ya kukusudia kuwa hilo llimependekezwa na dini na sharia.

Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu, naye atawaambia yale mliyokuwa mkihitalifiana.

Bila ya kutegemea akili au Wahyi; mkakubali yale mliyoyazoea na sio haki, na mkayakana yale yanayochukiwa na mapenzi yenu na matamanio yenu.

Ardhi Na Nyumba

Naye ndiye aliyewafanya makhalifa wa ardhi na akawainua baadhi yenu juu ya wengine ili awajaribu katika aliyowapa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameiumba ardhi hii akaifanya ni mahali pema panapofaa kwa maisha ya binadamu kutokana na mazingira yake, mpangilio wake, umbo lake na kuwa mbali kwake na jua na mwezi. Akaiandalia yote anayoyahitaji mtu mpaka nyenzo za kujipumbaza na kujistarehesha; sawa na nyumba iliyokamilika kila kitu. Kisha akamweka mtu, ndani ya hiyo ardhi baada ya kumwandalia nyenzo zote za kunufaika na kheri zake na baraka zake.

Na hekima yake ikataka watu watofautiane katika nyenzo hizo na kwamba baadhi yao wawe zaidi ya wengine katika akili, elimu na nguvu za mwili. Na akawawekea njia iliyo sawasawa ili awajaribu wenye nguvu kuwa je wataishukuru neema hii na kuzielekeza nguvu zao kwenye masilahi yao na maslahi ya ndugu zao wanaadamu; au watazifanya ni nyezo za kudhulumu, kunyang’anya, kujiadhimisha na kujifaharisha?

Aya hii imefahamisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemleta mtu katika ardhi hii kwa ajili ya elimu na matendo yenye kunufaisha.

Utauliza: Utaiunganishaje Aya hii na Aya isemayo:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ {56}

“Na sikuumba majini na watu ila waniabudu?” (51:56)

Jibu: Hazipingani Aya hizi mbili. Kwa sababu elimu na kazi yenye kunufaisha ni ibada ya Mwenyezi Mungu, bali ni katika ibada bora, na twaa iliyo kamili.

Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu.

Anawajaribu waja wake ili ampambanue mwovu na mwema, amwadhibu huyu na kumpa thawabu yule.

Na hakika yeye ni mwingi wa maghufira, mwenye huruma.

Huruma yake haina mpaka, wala msamaha wake hauna kifungu chochote. Ndio! Toba inajaalia msamaha ndio malipo yake yenye kulingana na unabaki msamaha wa ukarimu na kutoa kwa aombaye, hana wa kumlazimisha, isipokuwa yeye mwenyewe mtukufu. Hii ndiyo dalili ya kauli yake:

وَمَا أَصَابَكُمْ مِنْ مُصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَنْ كَثِيرٍ {30}

“Na masaibu yanayowasibu ni kwa sababu ya yaliyochumwa na mikono yenu; na Mwenyezi Mungu husamehe mengi.” (42:30).

Yaani mengi yaliyochumwa na mikono yetu.

Mola! tuokoe na yanayotokana na sisi wenyewe na tunakuomba utusamehe mizigo yetu wenyewe!