read

Aya 19 – 25: Na Wewe Adam Kaa Peponi Pamoja Na Mkeo

Maana

Na Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani (Pepo); na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, wala msiukurubie mti huu; msije mkawa miongoni mwa waliodhulumu (nafsi zao).

Imepita tafsir yake kwa ufafanuzi katika Juz.1 (2:35).

Basi shetani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizofichiwa.

Maana ya walizofichiwa ni kuwa kila mmoja hakuweza kuona tupu yake wala ya mwenziwe. Hatujui wasiwasi wa shetani ulikuwaje, lakini tunaamini kuwa mawazo yoyote, kauli au kitendo chochote kinachokikingama katika njia ya uhai basi kinatokana na mawazo ya shetani.

Vyovyote iwavyo ni kwamba shetani alidhihirisha nasaha kwa Adam na Hawa na akaficha uwongo. Na dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Iblisi alikuwa akijua kwamba mwenye kula mti huu basi atakuwa uchi na kwamba mwenye kuwa uchi hufukuuzwa Peponi; na ndio akafanya hila hiyo ya kuwatoa Peponi na akasema:

Mola wenu hakuwakataza mti huu ila msije mkawa Malaika au kuwa miongoni mwa wakaao milele. Na akaawapia: Kwa hakika mimi ni miongoni mwa watoa nasaha kwenu.

Mlaanifu alibadilisha mambo kichwa chini miguu juu, aliapa kwamba yeye anawanasihi, na hali yeye ni adui mhasimu. Akaapa kuwa wao wakila mti watakuwa katika watakaokaa milele, naye anajua wazi kuwa mwisho wa kula huko ni kufukuzwa na mauti. Hivi ndivyo wafanyavyo mashetani wa kibinadamu, huwatia mawazo wenye akili ndogo, wakaona mangati ni maji na maji ni mangati.

Basi akawatelezesha kwa hadaa.

Yaani, baada ya Shetani kuwapia Adam na Hawa kwamba yeye ni mtoaji nasaha aliye mwaminifu walimwitikia hadaa zake wakidhani kuwa hakuna yeyote anayeweza kuapa kwa Mungu uwongo. Kwa sababu mlaanifu huyu ndiye wa mwanzo kuthubutu kula kiapo cha uwongo; kama ambavyo yeye ndiye wa kwanza kujinaki kwa asili yake na ndiye wa kwanza kukisia kwa rai yake.

Walipouonja mti ule, tupu zao ziliwadhihirikia, wakaanza kujibandika majani ya kwenye Bustani (Pepo).

Yaani walipokula mti kila mmoja akaiona tupu ya mwenziwe, ambapo mwanzo zilikuwa zimesitiriwa, wakatahayari na wakaona iko haja ya kujisitiri. Wakaanza kukusanya majani ya mti wa Peponi na kuyaweka kwenye tupu zao.

Na Mola wao akawaita: Je, sikuwakataza mti huo na kuwaambia kwamba Shetani ni adui yenu wa dhahiri?
Hii ni lawama kwa Adam na mkewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kughurika kwao na kauli ya Iblisi, na udhaifu wa kukabiliana na upotevu wake; wakati huo huo akitanabahisha wajibu wa kutubia na kurejea.

Kwa hiyo ndio wakaharakisha kukiri dhambi na kuomba maghufira, wakasema:

Mola wetu! Tumedhulumu nafsi zetu; na kama hutatughufiria na kuturehemu tutakuwa miongoni mwa waliohasirika.

Na Mwenyezi Mungu alighufiria na kurehemu, kwa dalili ya Aya isemayo:

فَتَلَقَّىٰ آدَمُ مِنْ رَبِّهِ كَلِمَاتٍ فَتَابَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ {37}

“Akapokea Adam maneno kutoka kwa Mola wake na Mola wake akapokea toba yake; hakika Yeye ni Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu.” Juz. 1 (2:37).

Akasema (Mwenyezi Mungu): Shukeni, nyinyi kwa nyinyi ni maadui.

Maneno haya anaambiwa Adam, mkewe na Iblisi. Makusudio ya nyinyi ya kwanza ni Iblis na kabila yake, na ya pili ni Adam na kizazi chake. Sababu ya uadui huu ni kuwa Iblisi alikusudia kumpoteza mtu na kumharibu kwa kuchukua kisasi cha maafa yake.

Ama mtu hamwoni Iblisi kuweza kumpa udhia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ ۗ {27}

“Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni.” (7:27)

Na akasema tena:

إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ {6}

“Kwa hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni adui” (35:6).

Na makao yenu na starehe yatakuwa katika ardhi kwa muda. Akasema mtaishi humo na mtafia humo na mtatolewa kutoka humo.

Hivi ndivyo alivyotuandikia Mwenyezi Mungu, baada ya kutokea yaliyotokea kwa Adam, kwamba tuishi na tufe katika ardhi hii, kisha tutolewe humu kwa ajili ya hisabu na malipo baada ya kupata taabu na mashaka.

Kisa Cha Adam Kama Kilivyo Katika Qur’an

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja kisa cha Adam. Katika Juz.1 (2:33) na Aya zinazofuatia, Juz.8. (7:18) na Aya zinazofuatia, na katika Juz.16 (20: 116) na Aya zinazofoutia.

Muhtasari wa kisa chenyewe, kama kilivyoelezwa katika Aya hizo, ni huu ufuatao:

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwafahamisha Malaika wake kwamba yeye ataumba viumbe katika ardhi hii, watakaotembea katika pande zake zote na kula riziki yake. Na Malaika wakamwambia: Vipi unataka kuweka katika ardhi atakayefanya ufisadi na kumwaga damu kwa kushindania matunda yake; na sisi hapa tuko, tukikuabudu wewe milele? Mwenyezi Mungu akawapa jibu la kutuliza nyoyo zao na kuwataka wamsujudie Adam alipomkamilisha kuwa mtu.

Baada ya kwisha kumuumba kutokana na mchanga na kumweka sura ya mwisho, Malaika walimuadhimisha na kumsujudia, isipokuwa Iblisi akadhihirisha uasi na akatangaza jeuri.

Mwenyezi Mungu alipomuuliza akasema: “Mimi ni bora kuliko yeye.” Mwenyezi Mungu akampa malipo ya kumfukuza na laana.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimfundisha Adam majina ya viumbe vyote, ambapo Malaika walikuwa hawayajui. Mwenyezi Mungu akaamwamuru Adam awaambie, ili kubainisha ubora wake na kudhihirishaa hekima yake Mungu, ya kumweka Adamu kuwa khalifa katika Ardhi.

Mwenyezi Mungu akamfanyia Adam mke kutokana jinsi yake. Akawakalisha kwenye Bustani (Pepo) ya neema zake, akawaruhusu kula matunda yote na akawakataza mti mmoja katika miti yake. Akawapa dhamana, kama wakifuata amri, hawatakuwa na njaa wala kiu au kuwa uchi. Kisha akawatahadharisha na Iblisi na hadaa zake.

Mlanifu Iblisi aliona uchungu yeye kuwa mwovu na kuneemeka yule aliyekuwa ni sababu ya uovu wake na kufukuuzwa kwake kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu. Akawafitini kwa kuwapambia maneno na kuwahadaa.

Walikuwa na kivazi cha kuwasitiri tupu zao, hawajioni wala hawaonani uchi, lakini walipomaliza kula tunda hilo tu, sitara iliwaondoka wakawa uchi. Ndipo wakaharakisha kujifunika kwa majani ya Peponi.

Mwenyezi Mungu, Mtukufu akawalingania huku akiwalaumu, kwa kughafilika na nasaha yake na kusahau hadhari aliyowapa juu ya Iblisi.

Hapo wakanyenyekea kwake kwa kukiri na kujuta huku wakitaka rehema na maghufira. Lakini aliwatoa kwenye neema waliyokuwa nayo na akawakalisha kwenye ardhi hii aliyowafanyia njia mbili: Uongofu na upotevu.

Na akamwahidi Pepo yule atakayefuata uongozi wake; na kumpa kiaga cha moto yule atakayepotea. Akamfahamisha Adam na kizazi chake kwamba uadui baina yao na Iblisi utaendelea mpaka siku ya mwisho na kuwatahadharisha na fitina yake.

Huu ndio muhtasari wa yaliyo katika Qur’an kuhusu kisa cha Adam na mkewe. Kuhusu kisa hiki, watu wana kauli mbili: wale wanaopinga Wahyi na wale wanaouamini. Na hawa nao wako makundi mawili: Kuna kundi lilipetuka dhahiri ya Qur’an, wakategemea ngano za Kiyahudi katika kufasiri Bustani (Pepo) ya Adam na mengineyo.

Kwamba bustani hiyo ilikuwa duniani ikiitwa Bustani ya Aden; na mti aliokula Adam na Hawa ni ngano, na wao walijisitiri na majani ya mti wa Tini; na kwamba Iblisi aliingia kwenye Bustani akiwa ndani ya nyoka na mengineyo yasiyokuwa na asili yoyote ya Hadith wala Qur’an.

Kundi jingine likakimbilia kwenye mambo yasiyohisiwa. Wakafasiri mti kuwa ni mtihani, shetani kuwa ni matamanio, uchi kuwa uchafu na mengineyo katika fahamu za kisufi.

Sisi tuko katikati, tunaamini kiujumla yale yaliyotolewa Wahyi na dhahir ya Qur’an kwamba mti, uchi na majani, yote hayo yalikuwa ni vitu hasa vya kuhisiwa. Kwa sababu ndio ufahamisho wa kihakika wa tamko, wala hakuna la kuwajibisha kuleta taawili, maadam akili inakubali maana ya dhahiri wala haikatai.

Hatuwezi kuzungumzia hakika ya Bustani ya Adam, kwamba ilikuwa hapa duniani au penginepo; wala aina ya majani aliyojisitiria Adam na Hawa, aina ya mti, wala jinsi alivyonyapa Iblisi na kujipenyeza Peponi. Kwa sababu ufafanuzi wa haya ni katika ilimu ya ghaibu wala haukuteremshiwa wahyi na akili inashindwa kufahamu.

Imepokewa kutoka kwa Imam Ahmad amesema: “Mambo matatu hayana asili: Tafsir, mapigano na vita.” Anakusudia Tafsir ya Maneno ya Mwenyezi Mungu kwa yasiyokuwa maana ya dhahiri. Kwa sababu yeye ni katika ambao wanatoa dalili kwa dhahiri hii katika msingi na matawi.

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنْزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ ۚ ذَٰلِكَ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ {26}

Enyi wanadamu! Hakika tumewateremshia vazi lifichalo tupu zenu na vazi la pambo. Na vazi la takua ndiyo bora. Hiyo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.

يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُمْ مِنَ الْجَنَّةِ يَنْزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا ۗ إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ ۗ إِنَّا جَعَلْنَا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ {27}

Enyi wanaadamu! shetani asiwatie katika fitina, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo) akiwavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni. Hakika sisi tumewajaalia mashetani kuwa watawala wa wale ambao hawaamini.