Aya 26 – 27: Kivazi Cha Kuonekana Na Kisichoonekana
Maana
Katika Sura 6:141, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja fadhila ya chakula aliyowapa waja wake. Na katika Aya hii tuliyo nayo anataja neema ya kivazi.
Enyi wanadamu! Hakika tumewateremshia vazi lifichalo tupu zenu na vazi la pambo.
Maneno wanaambiwa wanadamu wote. Maana ya kuwateremshia ni kuwapa. Mwenyezi Mungu amewaneemesha waja wake, katika aliyowaneemesha, aina kwa aina za kivazi; kuanzia cha hali ya chini ambacho kinasitiri uchi mpaka cha hali ya juu cha kifahari.
Na vazi la takua ndiyo bora.
Nalo ni kumuogopa Mwenyezi Mungu na kufanya amali njema. Takua imetumiwa kuwa ni vazi kwa sababu imekinga mtu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama vazi linavyomkinga mtu na joto na baridi. Mwenyezi Mungu anasema “Na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto na za kuwakinga na vita vyenu” (16: 81).
Hiyo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.
Yaani Mwenyezi Mungu amewapa kivazi kwa fadhila zake, ili mjue twaa yake na muache kumwasi.
Enyi wanaadamu! Shetani asiwatie katika fitina, kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani (Pepo) akiwavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao.
Asiwatie katika fitina; yaani msighafilike na fitina yake na hadaa yake. Kuwavua nguo zao ni kuwa yeye alikuwa ni sababu ya kuvuliwa nguo.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameashiria uadui wa Shetani kwa Adam na jinsi alivyomfanyia vitimbi mpaka akamtoa yeye pamoja mkewe kwenye maisha ya raha kwenda kwenye maisha ya tabu na mashaka.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anawahadharisha wanaadamu wasiingie katika mtego wa Shetani na fitina yake na kuwateka kwenye maasi ili kuwazuia kuingia Peponi; kama alivyowahadaa wazazi wao, na kuwa ni sababu ya kuwa uchi na kutolewa Peponi.
Ilivyo hasa ni kwamba kuzuia kuingia Peponi ni rahisi zaidi kuliko kutoa. Kwani kumtoa mlowezi ni kuzito sana kuliko kumzuia anayetaka kulowea na kukalia ardhi ya watu. Mmoja wa watoaji waadhi anasema:
“Kosa moja tu lilimtoa Adam Peponi baada ya kuingia akiwa mtulivu, je, watoto wake wataingia vipi na hali makosa yamewajaa?”
Hakika yeye na kabila lake anawaona, na nyinyi hamuwaoni.
Shetani na majeshi yake anatuona, na sisi hatumuoni hata mmoja, kwa mujibu wa habari hizi za Wahyi, nasi tunauamini.
Hakika sisi tumewajaalia mashetani kuwa watawala wa wale ambao hawaamini.
Kifungu hiki kinaashiria jibu la swali la kukadiriwa ambalo ni: Ikiwa Shetani anatuona na sisi hatumuoni, maana yake ni kuwa yeye anatumudu na sisi hatumuwezi na kwamba yeye anaweza kutumaliza wakati wowote akitaka bila kuweza kujikinga naye. Sasa imekuwaje tukaamrishwa kujikinga naye na kutomsikiliza?
Jibu kwa ufafanuzi zaidi, ni kweli kwamba sisi hatumuoni Shetani, lakini tunahisi athari yake ambayo ni wasiwasi wake ukituambia kuwa hakuna Pepo wala moto na mfano wa hayo.
Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho huachana na wasiwasi huu wala hauitikii; na na anijlinda na yule mwenye kumtia wasiwasi. Kwa hiyo Shetani anarudi akiwa amehizika na kupata hasara.
Ama yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho huingiwa na wasiwasi huu na hutawaliwa na Shetani, hivyo humwongoza vile atakavyo na wakati atakao. Ama waumini hawawezi kusimamiwa na Shetani. Kwa sababu wao wamempa uongozi Mwenyezi Mungu peke yake. Hayo ndio maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu:
اللَّهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُمْ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُمْ مِنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ ۗ {257}
Baadhi wafasiri wamesema kuwa mashetani tusiowaona ni viini na virusi vya magonjwa vinavyobebwa na nzi na mbu kumwambukiza mwanadamu. Huzalikana humo na kukua kwa haraka na kusababisha maradhi yasiyoponyeka. Hii ni kufasiri makusudio ya Mwenyezi Mungu kwa kukisia na kubahatisha; na hiyo sio njia yetu kabisa!
وَإِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً قَالُوا وَجَدْنَا عَلَيْهَا آبَاءَنَا وَاللَّهُ أَمَرَنَا بِهَا ۗ قُلْ إِنَّ اللَّهَ لَا يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ ۖ أَتَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {28}
قُلْ أَمَرَ رَبِّي بِالْقِسْطِ ۖ وَأَقِيمُوا وُجُوهَكُمْ عِنْدَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۚ كَمَا بَدَأَكُمْ تَعُودُونَ {29}
فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ ۗ إِنَّهُمُ اتَّخَذُوا الشَّيَاطِينَ أَوْلِيَاءَ مِنْ دُونِ اللَّهِ وَيَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ مُهْتَدُونَ {30}