read

Aya 31-34: Chukueni Mapambo Yenu

Maana

Enyi Wanadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti.

Wafasiri wanasema watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakitufu Al- Kaaba wakiwa uchi, wake kwa waume: Na walikuwa hawali mafuta wakati wa Hijja; wala hawali chakula ila kiasi tu cha kuzuia tumbo, kwa ajili ya kuadhimisha Hijja, ndipo ikashuka Aya hii.

Na kwamba Mtume (s.a.w.) alisema: “Baada ya mwaka huu pasihijiwe na mshirikina yeyote wala Al-kaaba haitazungukwa uchi”, basi kauli yake hiyo ikatangazwa kwenye msimu. Miongoni mwa visa vinavavyoingia katika maudhui haya ni kile cha mwanamke mmoja mzuri wa Kiarabu aliyevua nguo na kuweka mkono kwenye tupu yake na akatufu. Macho ya watu yalipompata sana alitunga shairi hili:
Kuona yote au sehemu sihalali kitachoonekana
Kivuli kikubwa adhimu hata akali hamtavuna
Hata mwenye fahamu naye pia hudangana

Akimaanisha kuwa tupu yake ni adhimu pale ilipo, ina haiba na hifadhi, wala hakuna yeyote anayeweza kuifikia; na kwamba yeye anamkemea na kumchukiua anayemwangalia.

Kwa vyovyote itakayokuwa sababu ya kushuka Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kwa mtu kando kuangalia uchi wa mwingine awe mwanamume au mwanamke.
Na amewajibisha kusitiri tupu mbili katika Swala na tawafu.

Makusudio ya kila msikiti ni kama yale tuliyoyaeleza katika Aya iliyotangulia. Maana ni kuhimiza usafi na utwahara kutokana na uchafu na hadath na vilevile kujipamba nguo nzuri katika Swala ya Ijumaa, ya Jamaa, ya Idd au kutufu, ambapo sehemu hizo wanakusanyika watu, ili watu wasimkimbie kwa harufu yake mbaya na mandhari yake. Kujipamba ni vizuri, hata kwa fukara pia ajipambe kwa kiasi cha hali yake. Kuna Hadith isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na hupenda uzuri.”

Na kuleni na kunyweni.

Hii ni kupinga mwenye kuharamisha baadhi ya vyakula na vinywaji.

Wala msifanye ufujaji (israf) katika kula na kunywa na katika kujipamba kwa mavazi.

Hakika yeye hawapendi wafanyao ufujaji (israf).

Katika Aya nyingine anasema Mwenyezi Mungu:

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ {27}

“Hakika wabadhirifu ni ndugu wa mashetani” (17:27).

Na kuna Hadith isemayo: “Tumbo ni nyumba ya kila ugonjwa, na kula kwa makadirio ni msingi wa kila dawa, na uzoesheni kila mwili vile ulivyozoea.” Na Ali Al-Murtadha (a.s.) anasema: “Ni mara ngapi tonge moja imezuia matonge mengi?”

Sema: Ni nani aliyeharamisha pambo la Mwenyezi Mungu ambalo amewatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki?

Dhahiri ya maneno ni swali na maana yake ni kukana sana uharamu wa kujipamba na vilivyo vizuri katika riziki. Na kwamba ni katika wasiwasi wa Shetani na si katika Wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Kutegemeza neno mapambo kwa Mwenyezi Mungu kunafahamisha uhalali, na neno vitu vizuri linajifahamisha hilo lenyewe. Kwa sababu kila lililo haramu ni baya na wala si zuri.

Neno pambo linakusanya aina zake zote, ikiwa na pamoja na nyumba, na neno vitu vizuri linakusanya vyakula, vinywaji, kustarehe kwa mambo mazuri na wanawake, sauti nzuri, mandhari nzuri na kila starehe iliyo nzuri ambayo, sharia haikukataza.

Maulamaa wa Kiislam wameafikiana kwa kauli moja kwamba kila kitu ni halali mpaka uje ukatazo. Wakatoa dalili kwa hukumu ya akili, kwamba hakuna adhabu bila ya ubainifu, na kwa kauli ya Mtume Mtukufu (s.a.w.):

“Watu wako katika wasaa wa wasiyoyajua .” na kauli yake: “Yale ambayo Mwenyezi Mungu amewafunikia waja kuyajua basi yameondolewa kwao.” Amesema tena: “Kila kitu kimeachiwa mpaka uje ukatazo kwenye kitu hicho.”

Sema: Hivyo ni kwa wale walioamini katika maisha ya dunia, ni vyao tu siku ya Kiyama.
Yaani katika maisha haya ya dunia wataneemeka wote waumini na makafiri, lakini kesho watakaoneemeka kwa mapambo ya Mwenyezi Mungu na vitu vizuri katika riziki, ni wale walioamini tu, peke yao bila ya kushirikiana na wale waliokufuru na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Namna hii tunazieleza ishara kwa watu wajuao.

Mwenye kuifuatilia Qur’an ataona kuwa Mwenyezi Mungu anatumia neno Wajuzi (Ulama) kwa yule anayejua hukumu za Mwenyezi Mungu na akazitumia. Vilevile hulitumia kwa yule anayetarajiwa kuzijua na kuzitumia akifafanuliwa.

Kwa hiyo, makusudio ya watu wanaojua hapa ni aina ya pili ambao wanan- ufaika na ubainifu wa hukumu ya mapambo na vitu vizuri na vinginevyo na wanaowarejea maulama wa dini katika kujua hukumu za Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kutoa dalili kwa Aya za Mwenyezi Mungu kwa halali yake na haramu yake.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumkana anayeharamisha mapambo na vitu vizuri, sasa anabainisha misingi ya vilivyo haramu kama ifuatavyo:

Sema: Hakika Mola wangu ameharamisha mambo machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika.

Umetangulia ubainifu wake katika kufasiri Sura 6:151 kifungu cha wasia.

Na dhambi ni kila jambo ambalo anaasiwa kwalo Mwenyezi Mungu, iwe kauli au kitendo. Kuunganisha machafu kwenye dhambi ni katika hali ya kuunganisha mahsus kwenye ujumla; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ {163}

“Kama tulivyompa Wahyi Nuh (a.s.) na Mitume…” (4:163).

Na dhulma bila ya haki.

Kuna hadith inayosema “Lau jabali lingedhulu- mu jabali jingine, basi Mwenyezi Mungu angelifanya lile lililodhulumu lipondekepondeke.” Na Amirul-Muminin anasema: Mwenye kuchomoa upanga wa dhuluma atauwawa nao.”

Na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia dalili.

Hakuna dhambi nyingine baada ya ukafiri na shirk. Shirk ni kinyume cha Tawhid ambayo muhtasari wake ni:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ {11}

“Hakuna chochote kama mfano wake” (42:11).

Umetangulia ufafanuzi katika kufasiri Sura 6:153, kifungu cha ‘Wasia kumi.’

Na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua miongoni mwa hayo ni yale yaliyoashiriwa katika Aya 28 ya Sura hii: “Na wanapofanya machafu husema tumewakuta nayo baba zetu na Mwenyezi Mungu ametuamrisha.” Hakuna uchafu mbaya kama kusema bila ya kujua; na hakuna tofauti katika hukumu baina ya kumzulia Mungu na kumshirikisha. Imam Ali amesema: “Mwenye kuliacha neno ‘sijui’ atakuwa hana salama.”

Kila umma una muda makusudio ya umma hapa ni kundi, kama lilivyotumika neno hilo katika Aya isemayo:

وَلَمَّا وَرَدَ مَاءَ مَدْيَنَ وَجَدَ عَلَيْهِ أُمَّةً مِنَ النَّاسِ يَسْقُونَ {23}

“Alipofikia maji ya Madian alikuta umma wa watu wakinywesha.” (28:23)

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja uovu wa washirikina katika Aya 28; na yale aliyohalalisha katika Aya 31: na aliyoyaharamisha katika Aya 33. Baada ya haya yote anasema kila kundi, ikiwa ni pamoja na washirikina waliomzulia Mwenyezi Mungu, lina muda maalum katika maisha haya; kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu waambiwe yale waliyokuwa wakiyafanya.

Katika haya mna makemeo na kiaga kwa washirikina na wenye kufanya uovu na watu wa dhulma na kila anayesema juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi.

Utakapofika muda wao, hawatakawia (hata) saa moja wala hawatatangulia.

Imepita tafsir yake katika kufasiri Juz. 4 (3:145).

يَا بَنِي آدَمَ إِمَّا يَأْتِيَنَّكُمْ رُسُلٌ مِنْكُمْ يَقُصُّونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِي ۙ فَمَنِ اتَّقَىٰ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ {35}

Enyi: Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu, wakawaeleza ishara zangu, basi watakaoogopa na kufanya mema, haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {36}

Na wale watakaokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِآيَاتِهِ ۚ أُولَٰئِكَ يَنَالُهُمْ نَصِيبُهُمْ مِنَ الْكِتَابِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءَتْهُمْ رُسُلُنَا يَتَوَفَّوْنَهُمْ قَالُوا أَيْنَ مَا كُنْتُمْ تَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ ۖ قَالُوا ضَلُّوا عَنَّا وَشَهِدُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ أَنَّهُمْ كَانُوا كَافِرِينَ {37}

Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo au anayezikadhibisha Aya zake? Hao ndio itawafikia sehemu yao waliyoandikiwa. Mpaka watakapowafikia wajumbe wetu ambao ni Malaika, kuwafisha, watasema: Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema wametupotea. Na watajishuhudia wenyewe kwamba wao walikuwa makafiri.

قَالَ ادْخُلُوا فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِكُمْ مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ فِي النَّارِ ۖ كُلَّمَا دَخَلَتْ أُمَّةٌ لَعَنَتْ أُخْتَهَا ۖ حَتَّىٰ إِذَا ادَّارَكُوا فِيهَا جَمِيعًا قَالَتْ أُخْرَاهُمْ لِأُولَاهُمْ رَبَّنَا هَٰؤُلَاءِ أَضَلُّونَا فَآتِهِمْ عَذَابًا ضِعْفًا مِنَ النَّارِ ۖ قَالَ لِكُلٍّ ضِعْفٌ وَلَٰكِنْ لَا تَعْلَمُونَ {38}

Atasema: Ingieni motoni pamoja na umma zilizopita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapoingia umma utalaani ndugu zake. Mpaka watakapokusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza basi uwape adhabu ya moto maradufu. Hawa ndio waliopoteza. Atasema: Itakuwa maradufu kwenu nyote, lakini hamjui.

وَقَالَتْ أُولَاهُمْ لِأُخْرَاهُمْ فَمَا كَانَ لَكُمْ عَلَيْنَا مِنْ فَضْلٍ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْسِبُونَ {39}

Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao; basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma.