read

Aya 35-39: Wanaoogopa Na Kufanya Mema

Maana

Enyi: Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu, wakawaeleza ishara zangu, basi watakaoogopa na kufanya mema, haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
Mwenyezi Mungu alimuumba Adamu na kizazi chake na akawawekea njia ya kufuata, akawapelekea Mitume wa kuwafahamisha njia hiyo. Akawafanya Mitume ni jinsi ya wale wanaopelekewa Mitume hao. Kwa sababu hilo lina athari zaidi na ni hoja zaidi. Basi atakayesikia na akatii atasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Na wale watakaokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.

Mwalimu wetu- Mungu awe radhi naye - alikuwa akiwasomea wanafunzi wake sehemu za Kitab anachofundisha na kuwafafanulia kwa maneno wanayoyafahamu wote. Ikiwa sehemu iko wazi na inaeleweka kwa wote, basi husema “Kufafanua ufafanuzi ni mushkeli zaidi ya mishikeli!”. Hapo huiacha sehemu hiyo na kuendelea.

Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uwongo au anayezikadhibisha Aya zake?

Yametangulia maelezo katika Juz. 7 (6:21).

Hao ndio itawafikia sehemu yao waliyoandikiwa.

Hao ni wale waliotangulia kutajwa-ambao wamezusha yasiyokuwapo na wakakanusha yaliyopo. Makusudio ya waliyoandikiwa ni ajali na riziki. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anawaacha wakadhibishaji wamalize umri na riziki waliyoandikiwa.

Mpaka watakapowafikia wajumbe wetu ambao ni Malaika, kuwafisha, watasema: Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema wametupotea hatujui wako wapi wala hawaji kutuokoa na adhabu.

Na watajishuhudia wenyewe kwamba wao walikuwa makafiri.

Kukiri dhambi kunafaa pale inapowezekana kuificha na kukimbia malipo yake. Lakini baada ya kudhihiri kama jua na wakati wa kutekelezwa adhabu yake, hapo kukiri hakufai chochote.

Baada ya makafiri kujishuhudia wenyewe mahakama itafungwa na kutolewa hukumu ya adhabu ya moto.

Atasema: Ingieni motoni pamoja na umma zilizopita kabla yenu za majini na watu.

Makusudio ya uma ni wale wenye mila za kikafiri. Yaani Mwenyezi Mungu atawaambia wale waliokufuru Utume wa Muhammad (s.a.w.): Ingieni motoni ikiwa ni malipo ya kukufuru kwenu; kama walivyoingia waliokadhibisha Mitume kabla yenu.

Kila utakapoingia umma utalaani ndugu zake.

Watalaaniana nao walikuwa ndugu katika dini, nasaba na ukwe. Hivi ndivyo wafanyavyo watu wa hawaa na upotevu, wanapendana wakati wa utulivu na siku ya mutumaini, na kuchukiana na kulaaniana wakati ambapo hakuna matumaini wala matarajio yoyote.

Mpaka watakapokusanyika wote humo.

Yaani wakikutana humo, utaanza ugomvi na malumbano wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza basi uwape adhabu ya moto maradufu.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa makusudio ya wa mwanzo wao ni wa kwanza kuingia motoni, na wa nyuma ni wa nyuma kuingia. Wengine wakasema kuwa makusudio ya wa mwanzo ni viongozi na wa nyuma ni wafuasi. Kauli hii ndiyo iliyo sahihi kutokana na kusema: ‘Hawa ndio waliotupoteza.’

Kwa sababu mwenye kupoteza hufuatwa, na mwenye kupotezwa hufuata. Wenye kufuata wanataka kuongezewa adhabu wale waliofuatwa. Kwa vile wao ndio sababu ya kupotea kwao.

Atasema: Itakuwa maradufu kwenu nyote, lakini hamjui.

Yaani nyote mtapata adhabu maradufu, lakini kila kundi halijui kiasi cha adhabu ya kundi jingine.

Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi.

Wafuasi wanataka wazidishiwe adhabu viongozi. Kwa hiyo viongozi nao wanasema: Kwa nini mnataka hayo, nasi sote tuna malipo sawa wala hatutofautiana na chochote, kwa nini basi Mwenyezi Mungu atuongezee sisi adhabu zaidi ya nyinyi? Kisha wataendelea kusema ikiwa ni majibu ya maombi ya kuzidishiwa adhabu:

Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma sisi hatukuwalazimisha mlikuwa na hiyari.

إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلَا يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ {40}

Hakika wale waliokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbinguni. Wala hawataingia Peponi mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyowalipa wakosefu.

لَهُمْ مِنْ جَهَنَّمَ مِهَادٌ وَمِنْ فَوْقِهِمْ غَوَاشٍ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ {41}

Watakuwa na matandiko ya Jahanamu na juu yao shuka za kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ {42}

Na wale walioamini na wakatenda amali njema; hatukalifishi nafsi yoyote ila uweza wake; hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo.

وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِمْ مِنْ غِلٍّ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ ۖ وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّهُ ۖ لَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ ۖ وَنُودُوا أَنْ تِلْكُمُ الْجَنَّةُ أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنْتُمْ تَعْمَلُونَ {43}

Na tutaondoa chuki vifuani mwao; chini yao itapita mito. Na watasema: Sifa njema zote zinamstahiki Mwenyezi Mungu ambaye ametuongoza kwenye haya. Na hatukuwa wenye kuongoka wenyewe kama asingetuongoza Mwenyezi Mungu. Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki. Na watanadiwa kuwa hii ndiyo Pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya.