read

Aya 4-10: Na Miji Mingapi Tuliiangamiza

Maana

Na miji mingapi tuliiangamiza; ikafikia adhabu yetu usiku au katika wakati wa kailula1.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kumwamrisha Mtume wake Mtukufu kuonya kwa Qur’an na kuamrisha watu kuifuata, katika Aya hii, anataja maangamizo ya waliopita ambao aliwaangamiza kwa sababu ya kupinga kwao Mwenyezi Mungu na kukadhibisha Mitume yake, na kwamba yeye Mwenyezi Mungu aliwateremshia adhabu usiku au wakati wa kailula, mchana, ambao ni wakati wa raha na amani, ili adhabu iwaumize zaidi.

Wafasiri wengi wanasema kuwa kaumu ya Nabii Lut walijiwa na adhabu usiku. Nami nashangaa sijui wameyatoa wapi haya, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:

إِنَّ مَوْعِدَهُمُ الصُّبْحُ ۚ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ {81}

“Hakika miadi yao ni asubuhi, Je, asubuhi si karibu” (11:81).

Kuna kikundi cha wafasiri waliosema kuwa kuna mageuzi ya kutanguliza maneo katika Aya hii tunayoifasiri. Kwa sababu kuangamia kunakuja baada adhabu. Kwamba isomeke hivi: Ni miji mingapi ilifikiwa na dhabu yetu tuliiangamiza? Razi ametaja njia tatu za kuawili Aya hii na Tabrasi akazidisha ya nne.

Ilivyo hasa ni kuwa hakuna wajibu wowote wa kupangilia maneno kulingana na maana ya hali halisi, ikiwa utaratibu wa hali halisi uko wazi na unajulikana na wote; kama ilivyo katika Aya. Na herufi “Fa’, kama ambavyo inakuja kwa maana ya kufuatisha, vilevile inakuja ikiwa ni ya ziada na ya kufasiri. Hapa, herufi ‘Fa’ inafasiri aina ya maangamivu waliyoyapata washirikina.

Basi hakikuwa kilio chao, ilipowafikia adhabu yetu, ila kusema: Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

Washirikina walikuwa wakitambika kwa majina ya masanamu wakiwa wameamini kabisa. Lakini walipoona adhabu walijitenga na waungu wao na wakaelekea kwa Mwenyezi Mungu wakikiri ukafiri na ushirikina wao, lakini ni baada ya kukatika taklifa zote na kufungwa mlango wa toba.

Kwa hakika tutawauliza wale waliopelekewa (Mitume) na pia kwa hakika tutawauliza (Mitume) waliopelekwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuelezea maangamivu yao duniani anaelezea kuwa wao wataulizwa huko akhera na wataulizwa Mitume pia, wawatolee ushahidi.

Tena kwa hakika tutawasimulia kwa ujuzi, wala hatukuwa mbali.

Mwenyezi Mungu hatatosheka na kuwauliza tu na kuwauliza Mitume, bali yeye pia atawasomea kila kitu walichokisema na kukifanya:

يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُمْ بِمَا عَمِلُوا ۚ أَحْصَاهُ اللَّهُ وَنَسُوهُ ۚ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ {6}

“Siku Mwenyezi Mungu atakapowafufua wote, awaambie yale waliyoya- tenda; Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau; na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.” (58:6)

Mkusudio yake ni kuwatia msukosuko watambue nakama ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake kwao, yakiwa ni malipo ya uasi na ukaidi wao.

Mizani Ya Matendo

Na kipimo siku hiyo kitakuwa haki.

Maneno yamekuwa mengi kuhusu hakika ya mizani ambayo atapimia Mwenyezi Mungu matendo ya watu; mpaka baadhi ya watu wakasema kuwa mizani hiyo itakuwa na mikono miwili.

Tunavyofahamu sisi kuhusu mizani hii – na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi – ni kuwa ni kipimo ambacho kitampambanua mtiifu na mwasi na mwema na mwuovu. Kipimo chenyewe ni amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake.

Ukifika wakati wa Hisabu, huangaliwa aliyoyafanya na aliyoyaacha mwanaadamu, na hulinganisha kati ya aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kuyafanya na aliyoyaacha. Vitendo vyake vikifuatana na amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake, basi atakuwa ni katika waliofaulu, na kama si hivyo atakuwa ni katika wale ambao uzani waao umekua hafifu na kuwa katika madhalimu waliojihasiri wenyewe na adhabu ya moto.

Kwa maneno mengine ni kwamba kila kitu katika maisha haya kina msingi na udhibiti wake, iwe ni sayansi, fasihi au fani yoyote nyingine. Na kwayo hutofautiana na kingine, bali uzuri wake na ubaya wake unajulikana kutokana na misingi hiyo.

Misingi hiyo na udhibiti huo inaitwa mizani, makisio, njia na mwamuzi. Basi hivyo hivyo hisabu katika akhera ina misingi na udhibiti ambao Qur’an imeipa jina la Mizan na Swirat.

Kwa hiyo misingi hii au Mizani hii ya matendo ya watu ni amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake. Kazi yake katika kumhukumu mtu kesho, ni kama kazi ya fiqhi na kanuni katika kuhukumiwa mshitakiwa katika maisha ya hapa duniani.

Basi ambao uzani wao utakuwa mzito.

Nao ni wale ambao matendo yao yamelingana na misingi ya amri za Qur’an na makatazo yake yakawa makamilifu.

Hao ndio wenye kufaulu.

Kwa sababu hawakuanguka mtihani.

Na ambao uzani wao utakuwa hafifu.

Nao ni wale ambao umedhihirika umbali baina ya matendo yao na hukumu za Mwenyezi Mungu na mafunzo yake.

Basi hao ndio waliozitia hasara nafsi zao kwa sababu ya kuzidhulumu
Aya zetu.

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya kuzidhulimu hapa ni kuzikufuru, lakini sawa ni kukadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu kwa hali yoyote, kama inavyoonyesha Aya yenyewe, ni sawa Aya hizo ziwe zinafahamisha umoja wa Mwenyezi Mungu, ujumbe wa Mitume yake, ufufuo au halali yake na haramu yake.

Na hakika tumewamakinisha katika ardhi na tukawawekea humo mahitaji ya maisha. Ni shukrani ndogo mnazotoa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwamrisha washirikina kufuata waliyoteremshiwa, na kuwahofisha na adhabu ya dunia na akhera, sasa anawakumbusha neema yake kwao; na kwamba yeye ndiye aliyewaweka katika ardhi hii akawapa uwezo wa kuitumia kwa maslahi yao.

Mmoja wa wafasiri wa kisasa anasema: “Lau si Mwenyezi Mungu kumakinisha mtu katika ardhi hii, asingeliweza kiumbe huyu dhaifu kuyamudu maumbile”.

وَلَقَدْ خَلَقْنَاكُمْ ثُمَّ صَوَّرْنَاكُمْ ثُمَّ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ لَمْ يَكُنْ مِنَ السَّاجِدِينَ {11}

Na hakika tuliwaumba, kisha tukawatia sura. Kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam. Basi waka- sujudu wote isipokuwa Iblisi hakuwa miongoni mwa walio- sujudu.

قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِنْهُ خَلَقْتَنِي مِنْ نَارٍ وَخَلَقْتَهُ مِنْ طِينٍ {12}

Akasema (Mwenyezi mungu): Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, umeniumba kwa moto naye umemuumba kwa udongo.

قَالَ فَاهْبِطْ مِنْهَا فَمَا يَكُونُ لَكَ أَنْ تَتَكَبَّرَ فِيهَا فَاخْرُجْ إِنَّكَ مِنَ الصَّاغِرِينَ {13}

Akasema: Basi shuka kutoka huko, haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka, hakika wewe ni miongoni mwa walio duni.

قَالَ أَنْظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ {14}

Akasema: Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.

قَالَ إِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ {15}

Akasema (Mwenyezi mungu): Utakuwa katika waliopewa muda.

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ {16}

Akasema: Kwa kuwa umenipoteza, basi hakika nitawakalia katika njia yako

ثُمَّ لَآتِيَنَّهُمْ مِنْ بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَنْ شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ {17}

Kisha hakika nitawaendea kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru.

قَالَ اخْرُجْ مِنْهَا مَذْءُومًا مَدْحُورًا ۖ لَمَنْ تَبِعَكَ مِنْهُمْ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنْكُمْ أَجْمَعِينَ {18}

Akasema: Toka humo, hali ya kuwa ni mwenye kufedheheka na mwenye kufukuzwa. Atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.
  • 1. Kulala wakati wa mchana, nyakati za adhuhuri