read

Aya 40-43: Ngamia Na Tundu Ya Sindano

Maana

Hakika wale waliokadhibisha ishara zetu na kuzifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbinguni.

Ishara za Mwenyezi Mungu zinakusanya dalili za kuwapo Mwenyezi Mungu, Utume wa Mitume yake na kila walilolieleza kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu: Hawatafunguliwa milango ya mbingu- ni ni fumbo la kukataliwa amali zao na kwamba hazitakubaliwa; kama zikubaliwavyo amali za watu wema.
Mwenyezi Mungu anasema:

لَيْهِ يَصْعَدُ الْكَلِمُ الطَّيِّبُ وَالْعَمَلُ الصَّالِحُ يَرْفَعُهُ ۚ {10}

“Kwake hupanda neno zuri na tendo jema huliinua” (35: 10).

Wala hawataingia Peponi mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano.

Hili ni sharti lisilowezekana; sawa na kusema:

إِنْ كَانَ لِلرَّحْمَٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ {81}

“Kama mwingi wa rehema angelikuwa na mtoto ningekuwa wa kwanza kumwabudu” (43: 81).

Kupatikana sharti la muhali ni muhali. Waarabu hupigia mfano jambo lisilowezekana kwa kusema: “Sitafanya mpaka kunguru aote mvi!” Au “Mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano!”

Na hivi ndiyvo tunavyowalipa wakosefu.

Yaani tunawalipa kwa kuwazuilia Pepo. Pamoja na kuzuiliwa huku watakuwa na matandiko ya Jahanamu na juu yao shuka za kujifunika Yaani Jahanamu itawazunguka pande zote.

Na wale walioamini na wakatenda amali njema; hatukalifishi nafsi yoyote ila uweza wake; hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo.

Mwenyezi Mungu alipowapa kiaga waasi kwa adhabu ya Jahanamu sasa anawaahidi watiifu Pepo yenye neema watakayo starehe nayo bila ya kuwa na mwisho.

Ameishiria kwa kauli yake: “Hatukalifishi nafsi yoyote ila uweza wake,” kwamba Pepo kwa kadiri ya ukubwa wake, lakini mtu anaweza kuifikia bila ya mashaka wala uzito wowote.

Na kwamba atakayeingia Jahanam ataingia kwa kutaka kwake na hiyari yake.

Na tutaondoa chuki vifuani mwao; chini yao itapita mito.

Kwa nini iweko chuki? Duniani kulikuwa na chuki husuda, ria, uwongo na unafiki, kwa sababu kulikuwa na mafukara na matajiri, madhalimu na wenye kudhulumiwa na aliye mashuhuri na asiyejulikana, lakini Peponi hakuna ufukara, dhuluma wala umashuhuri baada ya Mwenyezi Mungu kumuweka kila mmoja katika daraja yake anayostahiki na cheo alichojichumia. Kila mmoja katika watu wa Peponi anahisi raha kwa kuokoka na Moto wa Jahanamu wala hamwangalii kabisa aliye juu yake:

فَمَنْ زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ {185}

“Mwenye kuepushwa na moto akatiwa Peponi, basi huyo amefuzu” Juz.4 (3:185).

Na watasema: Sifa njema zote zinamstahiki Mwenyezi Mungu ambaye ametuongoza kwenye haya Yaani kwenye njia ya neema hii.

Na hatukuwa wenye kuongoka wenyewe kama asingetuongoza Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni shukrani kwa Mwenyezi Mungu juu ya neema zake.

Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki.

Mitume waliwapa habari ya Pepo wakaamini mambo ya ghaibu. Walipoiona kwa macho yao walifurahi ambapo ghaibu imeonekana.
Na watanadiwa kuwa hii ndiyo Pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya.

Neno “Kurithishwa” kwa sababu ya kufanya amali, linafahamisha kwamba Pepo ni haki ya lazima kwa wanaoifanyia amali; sawa na mirathi. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya inafahamisha kwamba thawabu ni haki siyo fadhila.

وَنَادَىٰ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ أَصْحَابَ النَّارِ أَنْ قَدْ وَجَدْنَا مَا وَعَدَنَا رَبُّنَا حَقًّا فَهَلْ وَجَدْتُمْ مَا وَعَدَ رَبُّكُمْ حَقًّا ۖ قَالُوا نَعَمْ ۚ فَأَذَّنَ مُؤَذِّنٌ بَيْنَهُمْ أَنْ لَعْنَةُ اللَّهِ عَلَى الظَّالِمِينَ {44}

Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni kwamba tumekuta aliyotuahidi Mola wetu kuwa ni kweli. Je, nanyi pia mmekuta aliyowaahidi Mola wenu kuwa kweli? Watasema ndio. Basi mtangazaji atatangaza kati yao kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.

الَّذِينَ يَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُمْ بِالْآخِرَةِ كَافِرُونَ {45}

Ambao wanazulia njia ya Mwenyezi Mungu, Na wakataka kuipotosha. Nao hawaiamini Akhera.