read

Aya 46 – 49: Watu Wa A’raf

A’raf

Sisi tunaamini siku ya Kiyama, hisabu na malipo, kwa ujumla, ikiwa ni msingi katika misingi ya dini. Ama ufafanuzi na mafungu yake, hayo ni katika elimu ya ghaibu. Wala hakithibiti kitu chochote katika ulimwengu huo ila kwa Aya iliyo wazi au kwa Hadith wazi iliyothibiti kutoka kwa Ma’sum kwa khabar Mutawatir, na wala sio habari Ahad. Kwa sababu Habari Ahad ni hoja katika matawi tu, si katika misingi.

Khabar Mutawatir ni ile ambayo wanaipokea watu wengi bila ya kutokea mgongano wa uwongo. Kinyume chake ni Khabar Ahad.

Imethibiti kutokana na Wahyi kwamba huko Akhera kutakuwa na mahali, baina ya Pepo na moto, panaitwa A’raf. Hapo si mahali pa Pepo wala moto, lakini kwa undani ni rehema inayofuata Pepo; na kwa dhahiri ni adhabu inayofuatia Moto. Mwenyezi Mungu anasema:

فَضُرِبَ بَيْنَهُمْ بِسُورٍ لَهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِنْ قِبَلِهِ الْعَذَابُ {13}

“… utiwe baina yao ukuta wenye mlango; ndani yake mna rehema na nje kwa upande wake wa mbele kuna adhabu.” (57:13).

Katika mahali hapo paitwapo A’raf kutakuwa na watu wanaowajua watu wote wa Peponi na wa Motoni. Hawawajui kwa majina au hali yao; bali wanawajua kwa alama zinazowatofautisha.

Wao watawaangalia wa Peponi na kuwasalimia wakitumai kuwa pamoja nao wakati fulani. Na jicho lao likiwaangukia watu wa motoni tu, humwomba Mwenyezi Mungu asiwajaalie kuwa pamoja na watu madhalimu walioangamia. Kisha mwisho wa mambo watu wa A’raf wataingia Peponi. Kwa sababu wao ni katika watu wa Lailaha illa Ilah na Mwenyezi Mungu ana usaidizi maalum kwa watu wa aina hiyo.

Hayo ndiyo ujumla wa yaliyoelezwa na Qur’an kuhusu A’raf na watu wake, lakini Wafasiri wengi wamepetuka mpaka katika ufafanuzi huu, sasa tunaingilia kufasiri yanayofahamishwa na Aya:

Na baina yao patakuwa na pazia.

Yaani baina ya Pepo na Moto au baina ya watu wa sehemu hizo mbili. Pazia ni hiyo A’raf iliyoashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na juu ya A’raf watakuwako watu watakaowafahamu wote kwa alama zao.
Yaani watu wa A’raf watawajua wote watu wa Peponi, na watu wa motoni kwa alama zitakazowatambulisha sio mbali kuwa alama hizi ni zile zilizoashiriwa na Aya isemayo:

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ {106}

“Siku ambayo nyuso zitang’aa na nyuso (nyingine) zitasawijika.” (3:106).

Na pia Aya isemayo:

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُسْفِرَةٌ {38}

ضَاحِكَةٌ مُسْتَبْشِرَةٌ {39}

وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ {40}

تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ {41}

أُولَٰئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ {42}

“Nyuso siku hiyo zitanawiri. Zitacheka na kufurahika. Na nyuso nyingine siku hiyo zitakuwa na mavumbi. Zimefunikwa na weusi weusi. Hao ndio makafiri, watendao maovu.” (80:38-42).

Imesemekana kuwa alama hizo ni za ujumla watazijua watu wote; na dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa alama hizo watazijua watu wa A’raf tu.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, mambo ni mepesi sana hakuna taabu, maadamu sisi si wenye kukalifiwa wala hatutaulizwa kuhusu alama hizo zitakavyokuwa na hakika yake au sifa zake maalum au za ujumla.

Utauliza: Ni nani hao watu wa A’raf?

Jibu: Wafasiri wana kauli nyingi, yenye nguvu ni ile waliyoielezea wengi kwamba wao ni wale ambao uzani wao umekuwa sawa sawa; si mema yao yatakayozidi wala maovu yao. Lau mojawapo lingezidi jingine kwa uzani wa tonoradi, basi mwisho wao ungelijulikana, kuwa aidha Peponi au motoni.

Swali la pili: watu wa Peponi watajulikana kwa kuingia humo; vilevile watu wa Motoni. Sasa kuna haja gani ya alama?

Jibu: Huenda ikawa alama hizo ni za kupambanua baina ya makundi mawili kabla ya hisabu na adhabu; kama ambavyo mhalifu anavyotambulika kutokana na hali ya uso wake unavyokuwa anapopelekwa mahakamani.

Na watanadia watu wa Peponi: Salamun Alaykum.

Dhamir ya Watanadi ni ya watu wa A’raf. Maana ni kuwa wao watakapowaangalia watu wa Peponi watawasalimia kwa maamkuzi ya heshima.

Hawajaingia nao wanatumai kuingia Peponi. Kwa sababu wao ni katika watu wa Lailaha illa llah. Na kila anayemwamini Mwenyezi Mungu anatumaini rehema yake na maghufira yake. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِنْ رَوْحِ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ {87}

“Hakika hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri.” (12:87).

Kuna Hadith isemayo kuwa mtu mmoja alisema: “Wallahi Mwenyezi Mungu hatamsamehe fulani.” Mwenyezi Mungu akasema: “Ni nani huyu anayeniapia mimi kuwa nisimsamehe fulani?” Hakika mimi nimekwisha msamehe fulani na nimezishusha amali za mwenye kuapa.”

Na macho yao yanapogeuzwa kuelekea watu wa Motoni, husema: Mola wetu usituweke pamoja na watu waliodhulumu.
Neno ‘Yanapogeuzwa’ linafahamisha kuwa kuangalia kwa watu wa A’raf kwa watu wa motoni si kwa kukusudia.

Makusudio ya dhulma hapa ni ushirikina na kufru. Maana ni kuwa wao wakisadifu kuyaona ya watu wa Motoni huogopa na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu asiwajaalie kuwa pamoja na watu makafiri walioangamia.

Na watu wa A’raf watawanadia watu wanaowafahamu kwa alama zao, waseme: Haukuwasaidia mjumuiko wenu wala mlivyokuwa mkijivuna.

Wale waliokuwa wakijivuna katika ardhi walikuwa wakiwadharau waumini na wakijitukuza kwa yale waliyokuwa wakimiliki miongoni mwa mali na jaha; na wakiwaambia: Hamtapata kamwe rehema ya Mwenyezi Mungu, lakini kitakapofika kiyama na waovu kulipwa matendo yao, basi watu wa A’raf watawakumbusha mambo mawili:

Kwanza, yale waliyokuwa wakiyakusanya na kujivunia nayo, mali na kadhalika. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Haukuwasaidia mjumiko wenu wala mlivyokuwa mkijivunia.’ Pili, Yale waliyokuwa wakiwaambia waumini kuwa hamtaingia Peponi. Hayo yameashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Je, hawa ndio wale mliokuwa mkiwaapia kwamba Mwenyezi Mungu hatawafikishia rehma?

Kwa hiyo neno ‘Hawa’ ni waumini wadhaifu na neno mkiwaapia wanaam- biwa wajivuni.

Ingieni Peponi, hakuna hofu juu yenu wala hamtahuzunika.

Yaani waumini walioambiwa na wajivuni kuwa hawataingia Peponi, ndio sasa wanaambiwa ingieni Peponi.

وَنَادَىٰ أَصْحَابُ النَّارِ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ أَنْ أَفِيضُوا عَلَيْنَا مِنَ الْمَاءِ أَوْ مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ ۚ قَالُوا إِنَّ اللَّهَ حَرَّمَهُمَا عَلَى الْكَافِرِينَ {50}

Watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi: Tumiminieni maji au katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu. Watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameyaharamisha vyote viwili hivyo kwa makafiri.

الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَهْوًا وَلَعِبًا وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۚ فَالْيَوْمَ نَنْسَاهُمْ كَمَا نَسُوا لِقَاءَ يَوْمِهِمْ هَٰذَا وَمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ {51}

Ambao waliifanya dini yao kuwa upuuzi na mchezo na yakawahadaa maisha ya dunia. Basi leo sisi tunawasahau kama walivyosahau kukutana na siku yao hii na kwa sababu walikuwa wakizikataa ishara zetu.

وَلَقَدْ جِئْنَاهُمْ بِكِتَابٍ فَصَّلْنَاهُ عَلَىٰ عِلْمٍ هُدًى وَرَحْمَةً لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {52}

Na hakika tumewaletea Kitab tulichokipambanua kwa ujuzi, ambacho ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.

هَلْ يَنْظُرُونَ إِلَّا تَأْوِيلَهُ ۚ يَوْمَ يَأْتِي تَأْوِيلُهُ يَقُولُ الَّذِينَ نَسُوهُ مِنْ قَبْلُ قَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ فَهَلْ لَنَا مِنْ شُفَعَاءَ فَيَشْفَعُوا لَنَا أَوْ نُرَدُّ فَنَعْمَلَ غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ ۚ قَدْ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ {53}

Hawangojei ila matokeo yake siku yatakapotokea matokeo yake, watasema wale walioisahau hapo zamani: Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki. Je, tunao waombezi watuombee. Au turudishwe ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya? Hakika wamejitia hasarani nafsi zao na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.