read

Aya 50 – 53: Watu Wa Peponi Na Wa Motoni

Maana

Imeelezwa katika Hadith kwamba furaha ya watu wa Peponi kwa kuokoka na Moto itawazidishia neema na kwamba masikitiko ya watu wa Motoni kwa kukosa neema yatawazidisha adhabu; nao watajua kuwa watu wa Peponi wako kwenye neema. Ndio maana: watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi: Tumiminieni maji au katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu.

Nao watu wa Peponi watawajibu:

Hakika Mwenyezi Mungu ameyaharamisha vyote viwili hivyo kwa makafiri.

Baada kukata tamaa na watu wa Peponi, watataka waokolewe na walinzi wa Motoni; kama anavyosema Mwenyezi Mungu: Na wale waliomo Motoni watawaambia walinzi wa Jahanamu: “Muombeni Mola Wenu atupunguzie siku moja ya adhabu.” Na (walinzi) watasema: “Je, hawakuwawajia Mitume wenu kwa hoja zilizo wazi? Waseme: Kwa nini? Watasema: Basi ombeni, na dua ya makafiri haiwi ila ni ya kupotea bure.” (40: 49-50).

Baada ya kukata tamaa na walinzi watataka kujiokoa kwa Mwenyezi Mungu Mola wa ulimwengu, jambo ambalo lilikuwa rahisi wakati wa raha.

Watasema: “Mola wetu tulizidiwa na ubaya wetu na tukawa watu wenye kupotea. Mola wetu, tutuoe humu na tukirudia tena hakika tutakuwa wenye kudhulumu. Na (Mwenyezi Mungu) atasema: Hizikieni humo wala msinisemeshe.” (23: 106 - 108).

Ambao waliifanya dini yao kuwa upuuzi na mchezo na yakawahadaa maisha ya dunia.

Imepita tafsir yake katika Juz.7 (6: 70).

Basi leo sisi tunawasahau kama walivyosahau kukutana na siku yao hii na kwa sababu walikuwa wakizikataa ishara zetu.

Makusudio ya kusahau hapa ni kupuuza, kwani:

وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا {64}

“Mola wako si Mwenye kusahau.” (19: 64).

Na hakika tumewaletea Kitab tulichokipambanua kwa ujuzi, ambacho ni mwongozo na rehema kwa watu wanaoamini.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja watu wa Peponi, wa Motoni na wa A’raf . Na Aya hii na inayofuatia zinahusika na watu wa motoni tu, ambao wameghurika na maisha ya dunia.

Mwenyezi Mungu anasema kuwa tumewaletea hawa Qur’an inayoongoza kwenye uongofu na inayobainisha kwa ujuzi yake wanayoyahitajia watu katika maisha yao na marejeo yao na imemdhaminia – yule anayeamini na akayatumia mafunzo yake – uongofu wa kheri katika dunia na rehema ya Mwenyezi Mungu na thawabu katika Akhera. Ama mwenye kuachana nayo akafuata matamanio yake, basi marejeo yake ni Jahanamu.

Hawangojei ila matokeo yake.

Dhamir ya ‘yake’ inarudia Kitab; yaani kila linalotamkwa na Qur’an litatokea tu hapana budi.

Siku yatakapofika matokeo yake.

Kwa kutokea yale iliyoyatolea habari na uwabainikie makafiri kwa macho ukweli wake.

Watasema wale walioisahau hapo zamani: Hakika Mitume wa Mola wetu walileta haki.

Watayasema haya baada ya kuona adhabu. Na kabla yake waliwaambia Mitume kuwa ni wachawi na wazushi. Vilevile wataendelea kusema baada ya kuona adhabu:

Je, tunao waombezi watuombee kwa Mwenyezi Mungu atusamehe makosa yetu na asitufanyie hizaya na adhabu kama tunayvostahiki?

Au turudishwe ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya?

Lau Mwenyezi Mungu ataitikia maombi yao haya, misimamo yote ingelibatilika, na mwovu, ambaye haamini mpaka awekewe upanga kichwani mwake, asingekuwa ana tofuati na mwema ambaye anaamini haki bila kulazimishwa na kujitolea mhanga katika njia ya haki kwa pumzi zake zote.

Hakika wamejitia hasarani na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.

Hivi ndivyo zinavyokwenda bure amali za wabatilifu na hupotelewa na waombezi na wasimamizi waliokuwa wakiwafanyia amali.

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ {54}

Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Arshi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatiao upesi upesi, Na jua na mwezi na nyota zinatumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ {55}

Mwombieni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa uficho. Hakika yeye hawapendi wapetukao mipaka.

وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّهِ قَرِيبٌ مِنَ الْمُحْسِنِينَ {56}

Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake. Na mwombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema.