read

Aya 54 – 56: Katika Siku Sita

Maana

Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita.

Wafasiri wana kauli zenye kugongana katika Aya hii. Sababu yake ni mambo mawili: Kwanza, kwamba vitendo vya Mwenyezi Mungu havipimwi kwa wakati. Mwenyezi Mungu anasema: Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu kama kupepesa jicho.” (54:50).

Yaani neno moja tu, “Kuwa, ikawa”.

Pili, kwamba wakati unahisabiwa baada ya kumbwa mbingu na ardhi na matukio yanayotokea ndani yake. Kwa hiyo kabla ya ulimwengu hakukuwa na wakati wala siku.
Sasa Je, hiyo si ni sawa na kusema: Nimejenga nyumba kutokana na paa?

Kwa hiyo basi hakuna budi kuleta taawili ya siku kwa maana inayokubalika na inayoingia akilini. Wametofautiana katika kuainisha maana hayo ya majazi. Kuna waliosema kuwa kuna maneno yaliyokadiriwa; yaani katika kipimo cha siku sita.

Wengine wakasema kuwa siku hapo ni fumbo la awamu, na kwamba Mwenyezi Mungu hakuumba huu ulimwengu kwa mkupuo mmoja bali ni kwa awamu sita ili kila kitu kiwe na kiwango na wakati wenye kukadiriwa.

Pia wako waliosema kwamba siku ni fumbo la vipindi na mabadiliko; kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuumba ulimwengu mwanzo kama ulivyo sasa, bali uligeuka umbo mpaka umbo jingine, sawa na nad- haria ya kukua mpaka kufikia umbo la sita na la mwisho, ambalo tunaliona hivi sasa.

Njia zote hizi ni za kufikiri, wala hatuna cha kutuwezesha kuipendekeza zaidi kauli mojawapo; ingawaje tumefuatilia tafsir za zamani na za sasa.

Kwa hiyo tunasema pamoja na yule anayesema: “Siku inawezekana kuwa ni awamu sita; au mambo sita; au siku sita katika siku za Mwenyezi Mungu ambazo hazipimwi kwa kiasi cha kipimo cha wakati wetu. Na inawezekana kuwa ni kitu kingine.

Hivyo basi, haifai kukata kabisa maana yoyote ya idadi hii. Na dhana ni jaribio la suluhu na kushindwa mbele ya kile kinachoitwa elimu – nayo si zaidi ya kudhani na kukadiria.”

Kisha akatawala juu ya Arshi.

Jumla hii inafasiriwa na ile inayofuatia - Fahamuni Kuumba na amri ni yake. Yaani yeye anamilki dunia na kupanga mambo yake. Mfano wake ni Aya isemayo:

Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akatawala juu arshi anapangilia (kila) jambo…” (10:3).

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekuita kumiliki kwake na kupanga kwake mambo, kuwa ni kutawala juu ya kiti cha enzi (arshi). Kwa sababu mfalme hutawala mambo na kuyaendesha akiwa yuko kwenye kiti chake cha enzi (arshi).

Makusudio ya kusema hivyo ni kukurubisha maana, na sio tashbihi, (ukamfananisha Mungu na Mfalme wa duniani). Amesema: “Hakuna chochote kama mfano wake.”

Huufunika usiku kwa mchana, uufuatiao upesi upesi.

Hii ni katika mipango yake Mungu ya mambo ya ulimwengu. Maana yake ni kwamba usiku unafuata mchana na huufuatia haraka haraka na kuushinda ulivyokuwa kwa kufanya giza baada ya kuwa ni mwangaza. Mfano wa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَىٰ {1}

“Naapa kwa usiku unapofunika.” (92:1).

Na vilevile kauli yake:

إِنَّ سَعْيَكُمْ لَشَتَّىٰ {4}

“Na (kwa) usiku unapolifunika.”(91:4)

Yaani unaushinda mwanga wa jua.
Na jua na mwezi na nyota zinatumika kwa amri yake.

Yaani na ameumba sayari hizi zinazo kwenda kwa matakwa yake na kwen- da kwa mujibu wa hekima na masilahi. Mazungumzo kuhusu sayari hizi yanahitajia elimu ya falaki. Nasi hatujui chochote katika elimu hiyo.

Fahamuni! Kuumba na amri ni yake.

Huu ni ubainifu na tafsir ya kauli yake: Kisha akatawala juu ya arshi; kama tulivyotangulia kusema. Kuna Hadith isemayo: “Mwenye kudai kwamba Mwenyezi Mungu amewajaalia waja kuwa na amri, basi amekufuru yaliyoteremshiwa Mitume yake, kutokana na kauli yake: “Fahamuni! Kuumba na amri ni yake.”

Ametukuka Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote kwa umoja wake, ufalme wake na upangaji wake.

Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa uficho.

Maana ya mja kumwomba Mola wake sio kusema ‘Ewe Mwenyezi Mungu naomba rehema zako na maghufira yako’ Hapana! Isipokuwa kuomba kwa haki ni kumwogopa, kumcha na kushikamana na amri zake na kujiepusha na makatazo yake. Na pia sio makusudio ya kunyenyekea kusema: ‘Ewe Mwenyezi Mungu nanyenyekea kwako natubia, na najilinda kwako,’ bali mtu awe mkweli, mwenye ikhlasi katika anayoyasema na anayoyafanya.

Ama maana ya kwa uficho ni kutojifaharisha na kutangaza kwa watu kheri anayoifanya. Kwani hiyo ni aina ya kupetuka mipaka, na Mwenyezi Mungu anasema:

Hakika yeye hawapendi wapetukao mipaka.

Na Mwenyezi Mungu amekataza kujifaharisha kwa ibada na kufanya kheri.

Mwenyezi Mungu Ameitengeneza Vizuri Ardhi Na Binadamu Akaiharibu

Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.

Mwenyezi Mungu aliitengeza vizuri ardhi hii kwa kuweka hazina zisizo na idadi za vitu vizuri na starehe za kiroho na kimaada. Kuanzia maumbile asili ya kupendeza hadi kwenye uzuri wa mwanamke, na kwenye utekelezaji urafiki hadi wema wa watoto; na kuanzia kukua maarifa na utalii hadi sauti za minong’ono na nyimbo mpaka yasiyo na mwisho.

Vitu vizuri vya kimaada katika vyakula ni pamoja na nafaka, mboga, nyama na matunda. Kila jamii katika hivyo ziko aina, rangi na maumbo mbali mbali.

Katika mavazi ni pamoja na sufu, pamba, ngozi na hariri. Kisha binadamu akagundua Nailoni na ataendelea kugundua ambayo tunadhani ni katika mambo yasiyowezekana kama alivyogundua namna ya kupunguza masafa ya ardhini na mbinguni kwa mtu kuweza kusafiri kwa madakika tu.

Ama katika nishati ni kuanzia miti hadi makaa ya mawe, na petroli hadi umeme, nguvu za jua (Solar) na Tonoradi. Miongoni mwa niliyosoma ni kwamba sayansi imevumbua katika petroli vioo visivyovunjika, mabomu ya Napalm, Nailoni, Samadi ya kemikali, sahani na mabomba ya kunyunyizia maji.

Vilevile imetoa vipodozi, kama vile poda, rangi za mdomo, wanja na rangi za kucha. Pia imetoa maua ya bandia, vifunikia meza, dawa za meno, wino na filamu. Na vingine vingi hadi kufikia aina elfu tatu walizozihisabu Wataalamu, bali ni mpaka kufikia isiyo na idadi ila kwa yule ambaye anajua kila kitu:

ۚ وَإِنْ تَعُدُّوا نِعْمَتَ اللَّهِ لَا تُحْصُوهَا ۗ إِنَّ الْإِنْسَانَ لَظَلُومٌ كَفَّارٌ {34}

“Na mkizihesabu neema za Mwenyezi Mungu, hamtaweza kuzidhibiti. Hakika binadamu ni dhalimu mkubwa mwenye kukufuru sana.” (14: 34)

Aya hio ina matamko ya sana na kubwa pamoja na kutilia mkazo usisitizo huo, kwa neno hakika. Ni udhalimu gani mkubwa na utovu mkubwa wa shukran na ufisadi mkubwa kuliko kugeuza riziki njema kuwa mabomu ya Napalm, ya kuua watoto na kuwalemaza wakubwa, na hewa ya sumu inayochoma nyasi mbichi na kavu. Ama hayo mabomu ya Nuklia na Haidrojeni, ndiyo hayabakishi wala hayasazi!

Binadamu ameibadilisha neema kuwa kufuru na kuigeuza neema ya ardhi yake kuwa Jahanamu. Mwisho wa binadamu umefungamanishwa na manuklia. Mwenyezi Mungu ameweka katika ardhi hii starehe na riziki njema kwa waja wake.

Na yule dhalimu mkubwa asiye na shukrani ameweka mabomu ya Nuklia katika maghala yake na kwenye ndege zake zikizunguka angani, anangoja fursa tu aigeuze ardhi na vilivyomo kuwa majivu na mavumbi.

Hiyo ndiyo tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.” Kwa hiyo ni wajibu tumjue yule aliyeharibu ardhi baada ya Mwenyezi Mungu kututengenezea, na tumkatie njia kwa nyenzo zote tulizo nazo; angalau tumtangaze ajulikane na tumwite kwa jina lile alilopewa ‘Adui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu’ ili watu wote wawe na hadhari naye kutokana na vitimbi na hadaa zake.

Na mwombeni kwa kuogopa na kwa kutumai.

Kuwa na roho ya kukata tamaa ni hiyana. Kwa sababu hakuna maisha pamoja na kukata tamaa na kuacha kujihadhari pia ni hiyana kwa sababu ni kughurika. Njia ya kuokoka ni ile ya katika kati. Mwenyezi Mungu anasema:

وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ ۚ {57}

“Na wanatumai rehema zake na wanaogopa adhabu yake” (17:57).

Na amesema tena:

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {49}

وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ {50}

Waambie waja wangu kwamba mimi ni mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu. Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu” (15: 49 – 50).

Mumin mwenye akili anafanya amali hali ya kuwa anamcha Mwenyezi Mungu asijeikataa amali yake kwa makosa katika amali hiyo, na wakati huo huo anataraji kuokoka na kukubaliwa. Na yote hayo mawili, kuhofia na kutarajia yanaleta kujichunga na kufanya amali kwa uzuri.

Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu iko karibu na wanaofanya mema.

Hapo kuna kuashiria kwamba mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na akamtarajia, basi huyo ni katika watu wafanyao wema na kwamba Mwenyezi Mungu anawalipa wema kwa mfano wake.

وَهُوَ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا أَقَلَّتْ سَحَابًا ثِقَالًا سُقْنَاهُ لِبَلَدٍ مَيِّتٍ فَأَنْزَلْنَا بِهِ الْمَاءَ فَأَخْرَجْنَا بِهِ مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ ۚ كَذَٰلِكَ نُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {57}

Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji uliokufa. Kisha tunateremsha hapo maji. Kwa hayo tukaotesha kila matunda. Kama hivi tutawafufua wafu ili mpate kukumbuka.

وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا ۚ كَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَشْكُرُونَ {58}

Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hau- toi ila kwa taabu tu. Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaoshukuru.