read

Aya 57 – 58: Apelekaye Pepo Kuwa Bishara

Maana

Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji uliokufa. Kisha tunateremsha hapo maji. Kwa hayo tukaotesha kila matunda.

Makusudio ya rehema hapa ni mvua. Makusudio ya mawingu mazito ni yaliyotiwa uzito na mvuke wa maji. Na mji uliokufa ni ule usio na mimea.

Na kila matunda, makusudio yake ni ujumla wa kidesturi, sio wa kihalisi. Kwa ajili ya mji uliokufa ni kwa kukadiria, yaani kwa ajili ya uhai wa mji uliokufa.

Upepo huvuma, jua huyatia mvuke maji ya bahari na pepo hupandisha mvuke huu hadi juu; kisha ardhi huuvuta na kuanguka juu yake matone yenye kufuatana, yote haya na mfano wa hayo huja kwa mujibu wa desturi ya maumbile. Hilo halina shaka.

Lakini ni nani huyo aliyeweka maumbile haya na kuyapa utaratibu unaok- wenda nayo kwa jinsi moja katika mamilioni ya karne bila kugeuka au kubadilika? Je, maumbile yamepatikana kibahati tu. Je, kanuni, na desturi zimesimamiwa na sadfa tangu mwanzo hadi mwisho bila ya sababu yoyote? Vipi kisicho na nidhamu kizalishe nidhamu? Na kisicho na utambuzi kizalishe utambuzi?

Isitoshe je, maswali haya yana majibu ya kuingilika akilini na kukubalika zaidi ya kuwako muumbaji mwenye hekima, Aliyeyaleta maumbile na akayapa utaratibu na kanuni. Na kwake yeye kinaishia kila kitu na kuhitajia kila kitu, wala yeye hahitaji chochote?

Kwa hiyo upepo, mvua na kuhuyishwa mji uliokufa hunasibishwa kwenye desturi ya maumbile moja kwa moja na kupitia kwa muumbaji wa maumbile.

Kama hivi tutawafufua wafu, ili mpate kukumbuka.

Wakanushaji husema: Vipi tutaamini ufufuo na hatujaona yeyote aliyerudiwa na uhai baada ya kufa kwake? Wanasema hivi na wao wanaona kwa macho ardhi baada ya kufa inavyopata uhai, lakini wao wamesahau kuwa sababu ni moja na kwamba hakuna tofauti ila katika sura tu, ndipo Mwenyezi Mungu akawakumbusha hilo ili wao wanufaike kwa ukumbusho au iwalazimu hoja.

Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hautoi ila kwa taabu tu.

Kwa idhini ya Mola wake ni fumbo la kutoa kingi kutokana na uchache na kwa wepesi, na kidogo ni fumbo la kutoa kichache kwa uzito na ugumu.

Wafasiri wengi wanafananisha moyo wa mumin na kafiri, na mwema na mwovu na ardhi ambayo wote wameumbwa kutokana nayo. Wajihi wa kufananisha ni kwamba ardhi yote ingawaje ni jinsi moja, lakini kuna ile iliyo nzuri ambayo ikinywa maji husisimka na kututumka na kumea kila namna ya mimea mizuri.

Na kuna nyingine iliyosusuwaa imefungika inapinga kheri na utengenefu, inapojiwa na kheri yoyote ni kama kwamba inapelekwa kufa.

Namna hii tunazipambanua ishara kwa watu wanaoshukuru.

Mwenyezi Mungu hupiga mifano hii na mengineyo kwa wote kwa mwovu na mwema, lakini wema ndio wanufaikao nayo na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ama kwa mnasaba wa waovu. Basi ni hoja juu yao inayokata nyudhuru na sababu zao.

لَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ {59}

Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.

قَالَ الْمَلَأُ مِنْ قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {60}

Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.

قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي ضَلَالَةٌ وَلَٰكِنِّي رَسُولٌ مِنْ رَبِّ الْعَالَمِينَ {61}

Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote.

أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنْصَحُ لَكُمْ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ {62}

Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na nawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

أَوَعَجِبْتُمْ أَنْ جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِنْ رَبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِنْكُمْ لِيُنْذِرَكُمْ وَلِتَتَّقُوا وَلَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {63}

Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua, na ili mpate kurehemiwa?

فَكَذَّبُوهُ فَأَنْجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ فِي الْفُلْكِ وَأَغْرَقْنَا الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا عَمِينَ {64}

Basi walimkadhibisha. Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu. Hakika wao walikuwa watu vipofu.