read

Aya 59 – 64: Nuh

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema, katika Aya 35 ya Sura hii: “Enyi: Wanadamu! Watakapowafikia Mitume kutoka miongoni mwenu” Anaashiria, katika Aya hii na zinazofuatia, kisa cha Mitume Nuh, Hud, Swaleh, Nabii Lut, na Shuaib (a.s.).

Mwenyezi Mungu amekifupisha sana hapa kisa cha Nuh, ambapo ametosheka tu na kutaja majibizano kati yake na jamaa zake na namna walivyoepuka mwito na jinsi walivyostaajabu kuchagua Mwenyezi Mungu Mtume kutokana na wao.

Na kwamba yeye (s.w.t.) aliwagharikisha wakadhibishaji na kuwaokoa waumini.

Hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake.

Tabrasi anasema katika Majamaul-Bayan: “Yeye ni Nuh bin Mulk bin Matoshalkh bin Ukhnun, Mtume Idris. Na Nuh ni Mtume wa kwanza baada ya Idris.”

Inasemekana kuwa yeye alikuwa ni seremala na kwamba alizaliwa mwaka aliokufia Adam. Ama sisi, hatujui chimbuko la kusemekana huku.

Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika mimi ninawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu.

Aliufupisha Nuh (a.s.) ujumbe aliouchukua kwa watu wake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa jumla moja tu: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake kwa sababu hakuna Mola mwingine isipokuwa yeye. Na kwam- ba mwito wake huo kwao ni kuwahurumia na adhabu ya siku ya Kiyama.

Wakasema wakuu wa watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio wazi.

Wakamshutumu kwa upotevu na usafihi si kwa jingine ila tu kwa vile amewakataza walioyazoea na kuyarithi ya kuabudu mawe.

Hivi ndiyo alivyo kila safihi na kila mpotevu, humzulia ule ugonjwa wake kila anayekwenda kwenye njia ya uongofu.

Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotevu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu wote. Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu na ninawanasihi; na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Aliwajibu kwa kukanusha upotevu yeye mwenyewe na kujisifu kwa sifa tukufu kwamba yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, amempeleka ili awaokoe na upotevu na kuangamia, na kwamba yeye ni mtoaji nasaha mwaminifu, na anajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu umoja na uadilifu wake. Na mwenye kuwa na sifa hizi hawezi kuwa mpotevu.

Je, mnastaajabu kuwafikia mawaidha kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye na ili muwe na takua na ili mpate kurehemiwa?

Watu wake walimwaambia wewe ni mtu tu kama sisi. Lau Mwenyezi Mungu angelitaka kutuma mjumbe angelimtuma Malaika. Akawajibu kwamba hakuna ajabu kutuma Mwenyezi Mungu mtu kwa watu wake akiwa hana masilahi yoyote au lengo lolote ila kuwaongoza kwenye lile lililo na kheri yao na utengenefu wao, isipokuwa ajabu ni kupuuzwa na kuachwa bila ya mwongozi.

Razi anasema huu ni utaratibu wa lengo zuri, kwani lengo la kutuma ujumbe ni kuonya, na lengo la kuonya ni takua, na lengo la takua ni kufuzu rehema ya Mwenyezi Mungu katika nyumba ya akhera.

Basi walimkadhibisha. Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi, na tukawazamisha waliozikadhibisha ishara zetu. Hakika wao walikuwa watu vipofu.

Milango ya mbinguni ilifunguka ikatoa maji na ardhi ikachimbuka chem-chemi. Hapo Mwenyezi Mungu akawaangamiza madhalimu wenye kukad- hibisha na akaokoka Nuh (a.s.) na waumini aliokuwa pamoja nao. Yatakuja maelezo kwa ufafanuzi kuhusu Nuh (a.s.) na watu wake katika Sura iliyoitwa kwa jina lake (71) inshaallah.

وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۚ أَفَلَا تَتَّقُونَ {65}

Na kwa Adi (tulimpeleka) ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake. Basi hamwogopi?

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَوْمِهِ إِنَّا لَنَرَاكَ فِي سَفَاهَةٍ وَإِنَّا لَنَظُنُّكَ مِنَ الْكَاذِبِينَ {66}

Wakasema wakuu waliokufuru katika watu wake: Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu na tunakudhania ni katika waongo.

قَالَ يَا قَوْمِ لَيْسَ بِي سَفَاهَةٌ وَلَٰكِنِّي رَسُولٌ مِنْ رَبِّ الْعَالَمِينَ {67}

Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.

أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ {68}


Nawafikishi


a


ujumb


e


wa


Mola wangu na mimi kwenu nimtoanasaha,mwaminifu.

أَوَعَجِبْتُمْ أَنْ جَاءَكُمْ ذِكْرٌ مِنْ رَبِّكُمْ عَلَىٰ رَجُلٍ مِنْكُمْ لِيُنْذِرَكُمْ ۚ وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِنْ بَعْدِ قَوْمِ نُوحٍ وَزَادَكُمْ فِي الْخَلْقِ بَسْطَةً ۖ فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّهِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ {69}

Je, mnastaajabu kuwafikia ukumbusho kutoka kwa Mola wenu kupitia mtu anayetokana na nyinyi ili awaonye. Na kumbukeni alivyowafanya makhalifa baada ya watu wa Nuh. Na akawazidisha nguvu katika umbo. Basi kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.

قَالُوا أَجِئْتَنَا لِنَعْبُدَ اللَّهَ وَحْدَهُ وَنَذَرَ مَا كَانَ يَعْبُدُ آبَاؤُنَا ۖ فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِنْ كُنْتَ مِنَ الصَّادِقِينَ {70}

Wakasema: Je, umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ قَدْ وَقَعَ عَلَيْكُمْ مِنْ رَبِّكُمْ رِجْسٌ وَغَضَبٌ ۖ أَتُجَادِلُونَنِي فِي أَسْمَاءٍ سَمَّيْتُمُوهَا أَنْتُمْ وَآبَاؤُكُمْ مَا نَزَّلَ اللَّهُ بِهَا مِنْ سُلْطَانٍ ۚ فَانْتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُنْتَظِرِينَ {71}

Akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishawaangukia kutoka kwa Mola wenu. Je, mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote? Basi ngojeni; mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.

فَأَنْجَيْنَاهُ وَالَّذِينَ مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِنَّا وَقَطَعْنَا دَابِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۖ وَمَا كَانُوا مُؤْمِنِينَ {72}

Basi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.