Aya 65 – 72: Hud
Maana
Imesemwa katika Tafsir Al-Manar kwa kunukuliwa kutoka kwa Is-haq bin Bashar na Ibn Asakir: “Nabii Hud (a.s.) ndiye wa kwanza kuzungumza Kiarabu, alikuwa na watoto wane: Qahtan, Muq-hit, Qahit na Faligh ambaye ni baba wa Mudhar. (Abu Mudhar) Na Qahtan ni baba wa Yemen (Abul-Yaman). Ama Qahit na Muqhit hawana kizazi.”
Wafasiri wamesema: Watu wa Hud (a.s.) walikuwa ni katika kizazi cha Nuh (a.s.) na walikuwa kwenye dini yake. Baada ya muda kuwa mrefu, shetani aliwachezea, wakaabudu masanamu na wakafanya ufisadi katika ardhi.
Katika Tafsir Tabari imeelezwa kuwa Imam Ali alimwambia mtu mmoja kutoka Yemen: “Je, umeona katika ardhi ya Hadharamauti chungu ya tifu-tifu jekundu iliyochanganyika na madongo mekundu, ina mipilipili na mikunazi mingi sehemu kadha wa kadha?” Akasema: “Ndio Ewe Amirul Muminin, wallah unapasifu sifa ya mtu aliyepaona.” Akasema Amirul-Muminina: “Hapana, nimehadithiwa”. Yule mtu akasema: “Kwani pana nini Ewe Amirul-Muminin?” Akasema: “Pana kaburi ya Nabii Hud (a.s.) ”
Ikiwa ni sahih Riwaya hii, basi itabidi iondolewe sehemu iliyoandikwa kwenye kaburi ya Imam Ali, isemayo: Amani ishuke juu yako na juu ya jirani zako Hud na Swaleh , ila ikiwa ujirani wenyewe ni katika akhera sio hapa duniani, au iwe mwili wa Hud ulihamishwa baada ya kufa Imam.
Aya hizi zilizoshuka kuhusu kisa cha Hud (a.s.) zinaafikiana na Aya zilizotangulia, ambazo zimeshuka kuhusu kisa cha Nuh (a.s.) kimaneno na kimaana isipokuwa katika mambo yafuatavyo:-
Nuh (a.s.) aliwaambia watu wake: “Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iliyo kuu”. Na Hud (a.s.) akawaambia watu wake: Basi hamwogopi? Hiyo ni kwa sababu kabla ya Nuh (a.s.) hakukuwahi kutokea mfano wa adhabu hiyo, ambayo ni tufani. Na watu wa Hud (a.s.) walikuwa wakijua, ndipo akawahadharisha na akawaamrisha kumwogopa Mwenyezi Mungu, kwa kuacha kumshirikisha na kumthibitishia umoja.
Nuh (a.s.) aliambiwa na watu wake: ‘Hakika sisi tunakuona umo katika upotofu ulio dhahiri.’ Na watu wa Hud (a.s.) walimwambia:
Hakika sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakudhania ni katika waongo.
Kwa sababu Nuh (a.s.) alikuwa akitengeneza safina mahali pasipo na bahari wala mito. Na kazi hii ukitazama kwa dhahiri ni ujinga na upotevu.
Ama Hud (a.s.) hakufanya namna hii, isipokuwa aliwafanya wapumbavu watu wake kwa kuabudu masanamu. Kwa hiyo nao wakamrudishia na kumnasibishia upumbavu.
Nuh (a.s.) aliwaambia watu wake: ‘Ili mpate kurehemiwa.’ Na Hud (a.s.) aliwaambia watu wake:
Ili mpate kufaulu.
Nuh (a.s.) alikusudia rehema, na kuondolewa adhabu na Hud (a.s.) naye akakusudia kufaulu na kuongoka kwenye njia iliyo sawa. Maana zote mbili zinaungana, haziachani.
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja katika Aya hizi mambo ambayo watu wa Hud (a.s.) walimwambia mtume wao, lakini hakutaja kama watu wa Nuh (a.s.) walimwambia Mtume wao nayo ni:
Wakasema: Je, Umetujia ili tumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu?
Ibara inayotumiwa na kila jahili na mwenye kufuata. Basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.”
Likaja jawabu la mkato na la haraka kutoka kwa Mtume akasema: Hakika adhabu na ghadhabu zimekwishwaangukia kutoka kwa Mola Wenu. Maana ya kuwaangukia hapa ni kuwawajibikia, na makusudio ya adhabu ni sababu yenye kuwajibisha adhabu.
Je, Mnanijadili katika majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote?
Waungu mnaowaabudu hawako, na kila kisichokuweko hakina athari wala dalili. Kwa hali hii majina waliyopewa yanakuwa ni maneno matupu yasiyokuwa na maana.
Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojao.
Hili ni jibu la kauli yao: “Basi tuletee unayotuahidi ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.”
Basi tukamwokoa na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu na tukakata mizizi ya wale waliokadhibisha ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.
Kukatwa mizizi, ni kuangamizwa mpaka wa mwisho wao. Amebainisha Mwenyezi Mungu mahali pengine aina ya adhabu aliyowaangamizia watu wa Hud (a.s.), aliposema:
وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ {6}
سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَىٰ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ {7}
فَهَلْ تَرَىٰ لَهُمْ مِنْ بَاقِيَةٍ {8}
Inshallah yatakuja maelezo zaidi kuhusu Hud (a.s.) na watu wake katika Sura (11) iliyoitwa kwa jina lake.
وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُمْ بَيِّنَةٌ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ هَٰذِهِ نَاقَةُ اللَّهِ لَكُمْ آيَةً ۖ فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّهِ ۖ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ {73}
وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِنْ بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكُمْ فِي الْأَرْضِ تَتَّخِذُونَ مِنْ سُهُولِهَا قُصُورًا وَتَنْحِتُونَ الْجِبَالَ بُيُوتًا ۖ فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ {74}
قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِنْ قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُرْسَلٌ مِنْ رَبِّهِ ۚ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ {75}
قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا بِالَّذِي آمَنْتُمْ بِهِ كَافِرُونَ {76}
فَعَقَرُوا النَّاقَةَ وَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُوا يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِنْ كُنْتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ {77}
فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ {78}
فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَٰكِنْ لَا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ {79}