read

Aya 80 – 84: Lut

Maana

Na Lut alipowaambia watu wake: Je, mnafanya uchafu.

Amenukuu Mwenye Tafsir Al-Manar kutoka Kitabu Ansabul Arabiya ya kwamba Nabii Lut ni mwana wa ndugu wa Nabii Ibrahim Khalili (a.s.). Na kwamba yeye alizaliwa kaldayo (Chaldeans)

Hiyo ni sehemu iliyo upande wa Mashariki ya kati kusini mwa Iraq upande wa Magharibi katika jimbo la Basra. Sehemu hiyo wakati huo ikiitwa nchi ya Babel. Kisha Nabii Lut akasafiri na Nabii Ibrahim (a.s.) ami yake hadi sehemu iliyo baina ya mito miwili, sehemu inayozungukwa na Dijla, mamlaka ya Ashwar. Kisha Nabii Ibrahim (a.s.) akamweka mashariki mwa Jordan.

Ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu.

Inafahamisha kuwa watu wa Nabii Lut (a.s) ndio wa kwanza kuzusha aina hii ya ufisadi.

Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake.

Hii ni tafsir ya uchafu; na makusudio yake ni ulawiti ambao kisasa unaitwa kinyume na maumbile au kitendo kibaya.

Bali nyinyi ni watu warukao mipaka.

Mmepetuka mpaka katika kila kitu, mpaka mmefikilia kiasi hiki cha upotofu ambao unakataliwa na maumbile na kuhalifu desturi ya maisha.

Na halikuwa jibu la kaumu yake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu,maana hao ni watu wanaojitakasa.

Ndio! Utakatifu na kujistahi ni dhambi kwa mzinzi mchafu; na uaminifu ni kosa kwa mhaini kibaraka. Watoeni, maana hao ni watakatifu. Hivi ndivyo jamii chafu hukataaa wasafi na wema, si kwa lolote ila kwamba wao ni wasafi. Usawa ni kinyume cha hivyo.

Tukamwokoa yeye na jamaa yake isipokuwa mkewe alikuwa miongoni mwa waliobaki.

Makusudio ya jamaa yake ni kila aliyeamini, ni sawa awe ni katika familia yake au la. Kubaki ni kwamba mke wa Nabii Lut alibakia pamoja na walioangamia, na hakufuatana naye wakati alipoondoka usiku kukimbia adhabu, kwa sababu alikuwa mnafiki akila njama pamoja na washirikina dhidi ya mumewe. Inasemekana kuwa jina lake ni Wahila.
Mwenyezi Mungu ametumia dhamir ya wanaume “waliokuwa nyuma” kwa vile waume walikuwa wengi zaidi.

Yalimpata mke wa Nabii Lut yale yaliyowapata washirikina kwa sababu yeye ni katika wao, wala haukumfaa uhusiano wake na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuwa naye. Kuna Hadith isemayo: “Mtu yu pamoja na kipenzi chake.”

Na tukawamiminia mvua.

Amebainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) adhabu aliyowateremshia kuwa ni aina ya mvua, lakini ni ya mawe sio ya maji, kama ilivyoelezwa katika Aya isemayo:

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ {82}

Tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mkavu. (11:82).

Utakuja ufafanuzi huko mbele inshallah.

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.

Ni adhabu iumizayo, na mwenye akili ni yule anayepata funzo kwa wengine.

Utauliza: manabii Nuh, Hud na Swaleh (a.s.) kila mmoja aliwalingania watu wake kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake; kama ilivyoelezwa katika Aya zilizotangulia.

Lakini Nabii Lut aliwalingania watu wake kujizuia na uchafu; kama inavyoelezwa katika Aya hizi. Je, hii inamaanisha kuwa watu wa Nabii Lut walikuwa ni watu wa Tawhid, lakini walikuwa waovu kwa kitendo chao hiki kibaya?

Jibu: watu wa Nabii Lut walikuwa makafiri, na aliwalingania kwa Mwenyezi Mungu mmoja, na kuwakataza na shirk na ukafiri, kama alivyowakataza ulawiti; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ {162}

فَاتَّقُوا اللَّهَ وَأَطِيعُونِ {163}

“Hakika mimi kwenu ni Mtume Mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini”
(26: 162-163).

Isipokuwa alijishughulisha sana na uchafu huu, kwa vile ulikuwa umeenea sana kwao, na kuwafanya kuwa waasi wenye kuipinga haki na kuthubutu kuwakadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Yamekongamana madhehebu ya Kiislamu kwa kauli moja kuharamisha ulawiti, na kwamba ni katika madhambi makubwa. Wametofautiana katika adhabu yake.

Hanafi anasema ni kuaziriwa kwa aonavyo hakimu. Na madhehebu mengine yaliyobaki wamesema ni kuuliwa; kwa Hadith isemayo: “Mtakayempata anafanya vitendo vya watu wa Lut, basi muueni mfanyaji na mfanywa.”

Serikali ya Uingereza imehalalisha ulawiti na kupitishwa na bunge la Britania mnamo mwaka 1967. Gazeti la Al-Ahram la 6.9.1974 likinakili gazeti la Times la London linasema kwamba watu wakubwa wa Uingereza walifanya hafla kusherehekea kuhalalishwa huku kwa ulawiti.

Na wakajionyesha mbele ya mamia ya watazamaji. Hakuna mwenye shaka kwamba kuweko mabibi na wapenzi katika starehe hii kuliongeza shangwe na furaha!

وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُمْ مِنْ إِلَٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُمْ بَيِّنَةٌ مِنْ رَبِّكُمْ ۖ فَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {85}

Na kwa wa Madian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake. Hakika umewajia ubainifu kutoka kwa Mola wenu. Basi kamilisheni kipimo na mizani wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika ardhi baada ya kutengenea kwake. Hayo ndiyo bora kwenu ikiwa nyinyi mmeamini.

وَلَا تَقْعُدُوا بِكُلِّ صِرَاطٍ تُوعِدُونَ وَتَصُدُّونَ عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ مَنْ آمَنَ بِهِ وَتَبْغُونَهَا عِوَجًا ۚ وَاذْكُرُوا إِذْ كُنْتُمْ قَلِيلًا فَكَثَّرَكُمْ ۖ وَانْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ {86}

Wala msikalie kila njia kumwogopesha na kumzuilia njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kumuamini na kutaka kuipotosha. Na kumbukeni mlipokuwa wachache Akawafanya kuwa wengi, na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

وَإِنْ كَانَ طَائِفَةٌ مِنْكُمْ آمَنُوا بِالَّذِي أُرْسِلْتُ بِهِ وَطَائِفَةٌ لَمْ يُؤْمِنُوا فَاصْبِرُوا حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّهُ بَيْنَنَا ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ {87}

Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini yale niliyotumwa kwayo, na kundi (jingine) halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu; naye ndiye mbora wa wenye kuhukumu.