read

Aya 85 – 87: Shuaib

Maana

Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake.

Umepita mfano wake katika Aya 59 ya Sura hii.

Nabii Shuaib ni miongoni mwa Mitume waarabu; kama vile nabii Hud (a.s.) na Nabii Swaleh. Watu wa Madian ni waarabu walikuwa wakikaa katika ardhi ya Maa’n viungani mwa mji wa Sham.

Hakika umewafikia ubainifu kutoka kwa Mola wenu.

Ubainifu ni kila linalobainishiwa haki, ni sawa liwe ni dalili ya akili, au muujiza. Hakuna mwenye shaka kwamba Nabii Suhaib aliwaletea muujiza watu wake unaofahamisha utume wake; vinginevyo angelikuwa ni mtabiri sio Mtume. Hakuna nukuu ya Qur’an inayofahamisha aina ya muujiza huu. Kuuelezea ulivyokuwa, kama ilivyo katika baadhi ya Tafsir, ni kusema juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ujuzi.

Basi kamilisheni kipimo na mizani wala msiwapunje watu vitu vyao.

hii inashiria kwamba wao walikuwa wanafanyiana vibaya katika biashara, na kwamba hilo lilikuwa limeenea kwao. Kwa hivyo aliwaamrisha kukamilisha kipimo cha ujazo na mizani baada ya kuwaamrisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Tawhid). Kisha akawaamrisha uadilifu na kuacha kupunja katika haki zote za kimaada, kama vile elimu na maadili; wasimsifu mjinga kwa elimu wala kwa mhaini kwa uaminifu.

Wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya kutengenea kwake.

Imepita tafsir yake katika Aya 56 ya Sura hii kifungu ‘Mwenyezi Mungu aliitengeneza ardhi na mtu akaiharibu’
Hayo ndiyo bora kwenu ikiwa nyinyi mmeamini.

Hayo, ni ishara ya hayo matano yaliyotangulia: Kumwabudu Mwenyezi Mungu, kukamilisha vipimo na mizani, na kuacha kupunja na ufisadi.

Wala msikalie kila njia kumuogopesha na kumzuilia njia ya Mwenyezi Mungu mwenye kumwamini na kutaka kuipotosha.

Huu ni ubainifu na tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Wala msifanye uharibufu katika ardhi. Kwa sababu maana yake ni: Msiwatie shaka na kuwatisha ikiwa wanataka kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msimzuie Muumin kusimamisha nembo za dini, msije mkamzuia na njia ya Mwenyezi Mungu iliyo sawa na kujaribu kuwapeleka watu kufuata njia ya kombo mnayoifuata nyinyi.

Ufafanuzi zaidi na ufupi wa tafsir ya Aya hii ni yale yaliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba wao walikuwa wakikaa njiani kuwahofisha watu wasimwendee Nabii Shuaib (a.s.) na kuwaambia kuwa yeye ni mwongo atawafitini na dini yenu.

Na kumbukeni mlipokuwa wachache akawafanya kuwa wengi.

Mwenyezi Mungu amewajalia kuwa matajiri baada ya kuwa mafukara, wenye nguvu baada ya kuwa wanyonge, na wengi baada ya kuwa wachache. Na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa waharibifu.

Yaani yasije yakawapata yaliyowapata waliofanya uharibifu katika nchi; mfano watu wa Nuh , Hud, Swaleh na Lut (a.s).

Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini yale niliyotumwa kwayo na kundi (jingine) haliamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu.

Kundi moja lilimwamini Nabii Shuaib (a.s.) na jingine likamkanusha. Akayataka makundi yote yaishi kwa amani na kila kundi liachane na jingine bila ya kumtaaradhi yeyote kwa kukumuudhi; ni sawa awe amechagua ukafiri au imani, kisha yote mawili yataongoja mpaka Mwenyezi Mungu awahukumu.

Naye ndiye mbora wa wenye kuhukumu.

Wala hakuna wa kupinga mantiki hii. Utampinga na nini anayekuambia: ‘Ngoja Mungu atakuhukumu?’.