read

Aya Ya 73 – 79: Swaleh

Maana

Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, nyinyi hamna Mungu mwingine zaidi yake.

Thamud ni kabila katika Waarabu. Waliitwa kwa jina la babu yao Thamud bin Amir. Makazi yao yalikuwa Hijr, baina ya Hijaz na Sham mpaka Wadil-qura. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ {80}

“Na hakika watu wa Hijr walikadhibisha Mitume (15:80).

Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu aliye ishara kwenu.

Kikundi cha Wafasiri wamesema kuwa watu wa Nabii Swaleh (a.s.) walimwomba awatolee ngamia kutoka kwenye jiwe; na yeye alimwomba Mola wake hilo. Basi jiwe likashikwa na uchungu wa kuzaa kama mwanamke, likazaa ngamia wa kike mchangamfu mwenye manyoya.

Sisi tunaamini kiujumla kwamba ngamia alikuwa ni ubainifu na ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na kwamba hakuja kwa njia ya kawaida; na Mwenyezi Mungu alimtegemeza kwake kwa kumwadhimisha. Tunaamini hivi, bila ya kuongeza chochote ambacho hakikuelezwa na Wahyi au Hadith Mutawatir iliyotoka kwa Maasum.

Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimtie dhara, isije ikawashika adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.

Swaleh (a.s.) aliwaamrisha watu wake wamuache ngamia akae katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, na akawahadharisha na mwisho mbaya ikiwa watamtaaradhi kwa udhia. Kisha akawaambia:

Na kumbukeni alipowafanya makhalifa baada ya Ad.

Mwenyezi Mungu aliangamiza kabila la Ad kwa dhambi zao, akawakumbusha neema hii ya kuwa makhalifa. Vilevile aliendelea kuwakumbusha kwa kuwaambia:

Na kuwakalisha katika ardhi mkajenga makasri kati- ka nyanda zake na mkachonga majumba katika majabali.

Kauli hii inafahamisha kuwa Thamud waliishi katika majengo yaliyoendelea na kwamba walikuwa katika neema na starehe.

Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu, wala msifanye ufisadi katika ardhi.

Baada ya kuwakumbusha neema alizowamiminia Mwenyezi Mungu aliwaamrisha wakumbuke na washukuru neema hizo na kuwakataza wasifanye ufisadi. Hilo ni kuwahadharisha na uovu wa Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Wakasema wakuu wa watu wake waliotakabari kuwaambia wale walio wanyonge walioamini miongoni mwao.

Wale wapenda anasa katika watu wa Swaleh (a.s.) waliendelea na utaghuti na kung’ang’ania kuabudu masanamu. Ama wale wanyonge kuna walioamini katika wao na waliobakia kwenye shirki kwa kuwafuata wapenda anasa. Basi hawa wakawaambia wale walioamini katika mafukara na wanyonge:

Je, mnajua kuwa Swaleh ametumwa na Mola wake?

Waliwauliza wanyonge swali hili kwa kupinga na kutishia au kwa dharau na stihzai.

Wakasema – wale wanyonge – Hakika tunayaamini yale aliyotumwa.

Waliyasema haya bila ya kujali vitisho na stizai. Kwa sababu wao wana yakini na dini yao.

Wakasema wale waliotakabari kuwaambia wale wanyonge: Sisi tunayakataa yale mliyoyaamini.

Pamoja na dalili na ubainifu mkataa juu ya utume wa Swaleh. Kwa sababu masilahi yao ni zaidi kuliko dini za Mwenyezi Mungu na dalili ya kiakili. Razi anasema Aya hii ni miongoni mwa hoja kubwa kuwa kiburi kinatokana na wingi wa mali na jaha. Kwa sababu wingi huo ndio uliowafanya waendele kuasi na kukufuru.

Wakamchinja ngamia na wakaasi amri ya Mola wao.

Hakika yao inadhihirisha uasi huu, na kwamba wao hawajali isipokuwa masilahi yao tu. Wakamchochea Nabii Swaleh (a.s.) kuleta adhabu haraka na wakasema:

Ee Swaleh! : Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwachelewesha kuwalipa inadi hii Ukawanyakua mtetemeko wakawa wameanguka hawajimudu majumbani mwao.1

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya nyingine:

وَفِي ثَمُودَ إِذْ قِيلَ لَهُمْ تَمَتَّعُوا حَتَّىٰ حِينٍ {43}

فَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ وَهُمْ يَنْظُرُونَ {44}

Na katika Thamud walipoambiwa jifurahisheni kwa muda mdogo tu. Wakaasi amri ya Mola wao ikawanyakua rindimo na huku wanaona.” (51: 43-44)

Basi Swaleh akawaacha na akasema: Enyi watu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, lakini hampendi wenye nasaha.

Nabii Swaleh (a.s.) alipoona adhabu iliyowapata watu wake aliachana nao na akijiepusha na mwisho wao huu walioutaka wenyewe kwa uasi na jeuri.

Razi anasema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.): “Ewe Ali! Mwovu zaidi wa kwanza ni mchinja ngamia wa Swaleh, na mwovu zaidi wa mwisho ni muuaji wako”.

Tutarudia habari ya Nabii Swaleh (a.s) mara nyingine inshallah.

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُمْ بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِنَ الْعَالَمِينَ {80}

Na Lut alipowaambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu.

إِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِنْ دُونِ النِّسَاءِ ۚ بَلْ أَنْتُمْ قَوْمٌ مُسْرِفُونَ {81}

Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake! Bali nyinyi ni watu warukao mipaka.

وَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَنْ قَالُوا أَخْرِجُوهُمْ مِنْ قَرْيَتِكُمْ ۖ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ {82}

Na halikuwa jibu la watu wake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu, maana hao ni watu wanaojitakasa.

فَأَنْجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ {83}

Tukamwokoa yeye na jamaa zake isipokuwa mkewe alikuwa miongoni mwa waliobakia.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ مَطَرًا ۖ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُجْرِمِينَ {84}

Na tukawamiminia mvua, basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.
  • 1. Makusudio ya mtetemeko hapa ni rindimo, na kutojimudu ni kuangamia.