read

Aya 143: Umma Wa Wastani

Lugha

Neno Wast lina maana ya kati kati na neno Wasat lina maana ya ubora, Mtume anasema Bora ya mambo ni wastani. Linakuja neno wasata. Kwa maana ya kulingana sawa (wastani). Neno wastani na ubora yanakurubiana.

Makusudio ya Wasat hapa ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameijaalia dini ya Waislamu ni ya wastani; yaani ni ya kati na kati katika itikadi na maadili. Kwa upande wa itikadi hakuna ushirikina wala ulahidi, bali ni Tawhid tu, na kwa upande wa maadili sio ya kimaada wala kiroho, bali ni pande zote mbili kwa sharti ya kulingana sawa na kukamilika.

Neno ‘kurudi nyuma’ ni istiara yaani kueleza mtu anayemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa sababu mwenye kuacha imani yake yuko katika daraja ya asiyeendelea mbele.

Tumewafanya kuwa umma wa wastani.

Jumla hii ni ubainifu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.): Humwongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka.” (2:213).

Njia ya kubainisha hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaneemesha wafuasi wa Muhammad (s.a.w.w) kwa uongofu. Linalodhihirisha zaidi uongofu huu ni kuwa Yeye amewajaalia wao kuwa katikati; yaani hawakuzidisha, kama vile kuwazidisha waungu, wala hawakupunguza; kama vile ulahidi (kumkana Mungu). Hayo ni upande wa kiitikadi. Ama upande wa kimadili wastani wake ni, kwa kuwa amewachanganyia mambo ya kiroho na ya kimwili katika mafunzo yake na maelekezo yake - sio ubahili wa kiroho wala ubadhirifu wa kimaada, bali kuna uwiano kati yao.

Baadhi wameifanya kauli hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.Tumewajaalia ni umma wa wastani”, kuwa ni dalili ya hoja ya Ijmai. Lakini hiyo ni kutoa dalili mahali pasipokuwa pake. Kwa sababu haikuja kubainisha Ijmai, kwamba ni hoja au sio hoja.

Wengine wamesema kwamba kauli hii ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) inafahamisha kuwa kila Mwislamu ni mwadilifu kwa tabia. Hii pia nayo ni batil kabisa. Kwa sababu uadilifu hauthibiti isipokuwa kwa kujua au kwa ushahidi.

Ukamilifu Na Uwiano Katika Uislamu.

Binadamu ni mwili uliotokana na mchanga unaokwisha na ni roho inayo- dumu inayotokana na siri ya Mwenyezi Mungu, kama alivyosema: “Na wanakuuliza kuhusu roho. Sema: Roho ni katika mambo ya mola wangu.” (17:85). Kwa vile vitu viwili hivyo (mwili na roho) vina mahitaji na matakwa ndipo ikaletwa sharia ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa maelekezo ya msingi na nidhamu ili visizidiane. Kwa maneno mengine binadamu ni sehemu mbili, kupuuza moja wapo ni kumpuuza binadamu mwenyewe.

Uislamu umekataza utawa na kuiepusha nafsi na maumbile ya kawaida, kama ambavyo umehalalisha starehe za maisha, kama kula, kuvaa vizuri nk.

Atakayeziangalia Aya za Qur’an atakuta kwamba dunia yote imeumbwa kwa ajili ya uhai wa mtu kwa namna inayokubalika kwa wote, lakini wakati huo huo kuipupia kuifanyia hiyana na kuwazuia watu wengine na hiyo dunia ni ufisadi na hatari kwa usalama wa jamii. Riziki bora kabisa katika Uislamu ni ile iliyotolewa jasho.

Anas anasema: Siku moja tulikuwa na Mtume (saww) safarini wengine wakawa wamefunga na wengine hawakufunga. Tukashuka sehemu fulani ilikuwa ni wakati wa joto. Basi waliofunga wakaanguka wote, ikawa wasiofunga wanawahudumia waliofunga. Mtume (s.a.w.w) akasema.: Wasiofunga leo wamechukua malipo yote.

Huu ndio msingi wa uwiano katika Uislamu. Sio ibada itayozuia kuhangai- ka wala sio ulafi utakayozuia kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Ili muwe mashahidi juu ya watu na Mtume awe shahidi juu yenu.

Maana ya matamko haya yako wazi na maana ya kiujumla pia iko wazi. Lakini tatizo liko kwenye kuelezea sisi Waislamu ni mashahidi juu ya akina nani? Mtume (s.a.w.w) atakuwa shahidi kesho dhidi ya yule aliyehalifu miongoni mwetu, je sisi tutakuwa mashahidi dhidi ya wasiokuwa Waislamu ambao wamehalifu Kitabu na Sunna?

Kauli zimekuwa nyingi na kugongana juu ya hilo; nami sikupata ya kunituliza. Nionavyo mimi ni kwamba Ulama wa Kislamu wanawajibu wa kuufikisha ujumbe wa Muhammad (s.a.w.w) kwa watu wawe ni Waislamu au si Waislamu wasiojua au wawe wanajua. Mwenye kutekeleza wajib huu Mtukufu, basi atakuwa shahidi dhidi ya yule aliyemfikishia kuwa hakuyatumia mafunzo. Na, atakayepuuza wajib huu na asiufikishe, basi Muhammad (s.a.w.w) atakuwa shahidi dhidi yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba yeye amefanya hiyana.

Kwa ufafanuzi zaidi tupige mfano huu: Mtu ana mali na mtoto mdogo, alipohisi kifo chake kiko karibu akamuusia mtu anaye mtegemea kwa dini yake amlee mtoto wake kutokana na mali atakayoiacha. Akitekeleza yule aliyeusiwa na mtoto akafaulu, basi nisawa, lakini mtoto akifanya uasi na akakataa mfunzo, basi aliyeusiwa atakuwa shahidi dhidi ya mtoto na kama aliyeusiwa ndiye aliyezembea, basi mzazi atakuwa shahidi dhidi ya aliyeusiwa.

Vilevile sisi Ulama tuna majukumu makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ya kufikisha mwito wa Kiislamu kwa watu wenye dini mbali mbali kwa hekima na mawaidha mazuri. Na atakayezembea wajib huu kesho atashuhudiwa na bwana wa viumbe na atahukumiwa. Hii ni ikiwa amepuuza, sikwambii ikiwa yeye ndiye sababu ya kupatikana shaka katika watu wake?

Na hatukukifanya Qibla ulichokuwa nacho ila tupate kumjua yule anayemfuata Mtume na yule atakayegeuka akarudi nyuma.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwamrisha Mtume wake kugeuza Qibla baadhi ya watu walianza kutia shaka na kusema: mara huku na kesho kule. Na Mayahudi nao wakachukua fursa ya kuwatia shaka wajinga kuhusu Mtume. Hao Mayahudi walikuwa wamekuwa na wataendelea kuwa ni watu wa fitina na uvunjaji; wenye vitimbi na hadaha. Wanatengeneza matatizo na kumwekea vikwazo kila mwenye Ikhlas na wanajaribu kuzigeuza jamii kuzipeleka kwenye matatizo. Ndio tabia na maumbile yao.

Ndivyo ilivyo, mara nyingi maadui wa haki wanawatumia wadhaifu wa akili na kuwafanya ni chombo cha kufanya vitimbi, uharibifu na vurugu.

Imam Ali amewaelezea kwa ufasaha zaidi aliposema: Ni wanyama wasiokuwa na mchungaji wanamfuata kila atakayewapigia kelele ni (bendera) wanafuata upepo, hawakupata mwanga wa elimu wala hawana cha kutegemea.”
Mwenyezi Mungu alimpa habari Mtume wake Mtukufu kwamba wale wanaotia shaka si waumini halisi na tumewapatia mtihani huu ili ufichuke ukweli kwako na kwa wengine.

Na kwa hakika lilikuwa ni jambo gumu, ispokuwa kwa wale aliowaongoza Mwenyezi Mungu.

Ambao ni wenye imani halisi sio imani ya kuazima. Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua kila kitu kabla ya kutokea, sasa kuna wajihi gani kusema: ili tumjue anayemfuata Mtume?

Jibu: Lengo hapa ni kumdhihirisha mtiifu na asiyekua mtiifu na libainike hilo mbele za watu.

Wafasiri wengi wamesema kwamba Mwenyezi Mungu ana elimu mbili ya kujua kitu kabla ya kuwa ambayo ni elimu ya ghaib na elimu baada ya kuwa, ambayo ni elimu ya ushahidi na ndiyo iliyokusudiwa katika Aya hii, yaani Mwenyezi Mungu ametaka kujua baada ya kuwa, kama alivyo jua kabla ya kuwa.

Huku ni kucheza na maneno tu. Elimu ya Mwenyezi Mungu ni moja, elimu ya ghaib ndiyo hiyo hiyo elimu ya ushahidi .

Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kupoteza imani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu kwa watu ni mpole mwenye kurehemu

Hii ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa wale wenye uthabiti katika imani yao kwa Mtume (s.a.w.w) kwa shida na raha. Wanafuata amri yake na wanaacha makatazo yake.

Wafasiri wengi wamesema kuwa sababu ya kushuka Aya hii ni kwamba baadhi ya masahaba waliswali na Mtume kibla cha kwanza na wakafa kabla ya kugeuzwa kibla cha pili, akaulizwa Mtume kuhusu swala yao, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo.

Sisi hatutegemei mapokezi ya sababu za kushuka Aya isipokuwa machache tuliyo na yakini nayo. Kwa sababu maulamaa hawakujishughulisha sana na usahihi wake, kama walivyofanya kwa mapokezi ya hukumu.

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ ۖ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا ۚ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ ۚ وَحَيْثُ مَا كُنْتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ ۗ وَإِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِنْ رَبِّهِمْ ۗ وَمَا اللَّهُ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ {144}


Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni; basi tutakuelekeza Qibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu (Al-Ka’aba). Na popote mlipo geuzeni nyuso zenu upande huo. Na hakika wale waliopewa Kitabu wanajua kwamba huo ni haki itokayo kwa Mola wao; na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.

وَلَئِنْ أَتَيْتَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ بِكُلِّ آيَةٍ مَا تَبِعُوا قِبْلَتَكَ ۚ وَمَا أَنْتَ بِتَابِعٍ قِبْلَتَهُمْ ۚ وَمَا بَعْضُهُمْ بِتَابِعٍ قِبْلَةَ بَعْضٍ ۚ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُمْ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ ۙ إِنَّكَ إِذًا لَمِنَ الظَّالِمِينَ {145}


Na hao waliopewa Kitabu hata ukawaletea hoja za kila namna, hawatafuata Qibla chako; na wala wewe si mwenye kufuata Qibla chao, wala baadhi yao si wenye kufuata Qibla cha wengine. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya kuku- fikia elimu, utakuwa miongoni mwa madhalimu.