read

Aya 144-145: Hakika Tunakuona Unavyogeuza Uso Wako

Maana

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Imepokewa kutoka kwa Imam Jaffar Sadiq (a.s.) kwamba: Kiligeuka Qibla baada ya kuswali Mtume (s.a.w.w), Makka kwa muda wa miaka 13 akielekea Baitul Maqdis. Na baada ya kuhamia Madina, aliswali miezi saba, kisha Mwenyezi Mungu akamwelekeza Al Ka’aba.”

Sababu hiyo ni kwamba Mayahudi walikuwa wakimkejeli Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumwambia: “Wewe unatufuata sisi, unaswali kwenye Qibla chetu.” Mtume akaingiwa na majonzi makubwa, akatoka usiku akawaana angalia pambizoni mwa mbingu, akingojea amri ya Mwenyezi Mungu kuhusu jambo hilo.

Kulipokucha akaswali swala ya Adhuhuri katika msikiti wa Bani Salim, alipomaliza rakaa mbili alishukiwa na Jibril akamshika na kumgeuza upande wa Al-Ka’aba, akamteremshia Aya hii: “Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni”, Mtume akaswali rakaa mbili kuelekea Baitul Maqdis na rakaa mbili kuelekea Al- Ka’aba.

Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti mtakatifu (Al Ka’aba).

Ameusifu Msikiti kwa utakatifu, ambapo ni wajibu kuutakasa na ni hara- mu kuuvunjia heshima. Al-Ka’aba ni sehemu ya Masjidul Haram (Msikiti Mtakatifu) nao ni sehemu ya Haram ambayo inakusanya Makka na mipaka yake, kama ilivyoelezwa katika vitabu vya Fiqh, katika mlango wa Hijja, katika masuala ya Ihram na kuwinda katika Haram.

Yanayojulikana katika Qur’an ni kwamba amri ya wajib yoyote ya kisharia inayoelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu inawahusu watu wote, mfano: “Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na mwanzo wa usiku.” (11:114).

Haiwezekani kuwa amri ya wajib inahusika na yeye Mtume tu, ila kama kuna kitu kinachofahamisha hilo; kama Aya hii: “Na katika usiku swali Tahajjud.1Hiyo ni Sunna kwa ajili yako...” (17:79).

Neno ‘kwa ajili yako’ linafahamisha kwamba taklifa hii haimuhusu mtu mwingine isipokuwa yeye.

Vile vile njia ya Qur’an ni kwamba taklifa zenye kuelekezwa kwa watu na Muhammad (s.a.w.w) pia huwamo, bila ya kuwako na tofauti hata ndogo ya mwelekezo huo kati yake na mwingine. Kwa hivyo umma unaingia katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtukufu (Al-Ka’aba).

Na popote mlipo geuzeni nyuso zenu upande huo.

Yaani popote mnapokuwa baharini au bara, kwenye tambarare au majabalini, Mashariki au Magharibi, ni juu yenu kuelekea Msikiti Mtukufu kwa sehemu ya mbele ya mwili, wala haijuzu kuupa mgongo katika swala au kuuelekea kwa upande wa kuume au kushoto, nk.

Kutokana na hali hiyo Qibla kinahitalifiana kwa kuhitalifiana miji. Kwa ajili hii Waislamu wamejishughulisha sana na suala la Qibla na wakaweka elimu mahsus kwa jina la elimu ya “Qibla”, Kinyume na Wakristo ambao wanalazimiana na upande wa Mashariki daima na Mayahudi nao ni upande wa Magharibi popote walipo, hata kama hilo litalazimisha kuipa mgongo Baitul Maqdis.

Unaweza kuuliza: Ikiwa Umma unaingia katika msemo unaoelekezwa kwa Mtume na msemo unaolekezwa kwa Umma unamhusu Mtume; sasa kwa nini kukusanyika misemo inayoelekea sehemu mbili katika Aya moja na maudhui moja tena bila ya kuwako kitenganisho.

Yaani Mwenyezi Mungu anasema elekeza uso wakoewe Muhammad - upande wa Msikiti Mtakatifu, na popote mtakapokuwa - enyi Waislamu - elekezeni nyuso zenu upande uliko Msikiti Mtakatifu.

Jibu: Kugeuka Qibla ni tukio kubwa katika Uislamu na kulikuja kutokana na raghba ya Mtume (s.a.w.w). Kwa hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akataka kumbainishia hilo, na kulitilia mkazo kwa kulikariri.

Zaidi ya hayo ni kuwa kwa asili taklifa hiyo ni ya Muhammad (s.a.w.w), kwa sababu imekuja kwa raghba yake na kufuatilia umma wake.

Ni Wajib Wakati Gani Kuelekea Qibla?

Al Ka’aba ni Qibla kwa aliye ndani ya Msikiti Mtakatifu ambao Al Ka’aba imo ndani yake, Msikiti ni Qibla kwa watu wa Haram; yaani watu wa Makka na pembeni mwake na Haram au upande wake ni Qibla kwa watu wa Mashariki na Magharibi.

Ni wajibu kuelekea Qibla katika swala za kila siku, swala ya ihitiyat, mafungu yaliyosahauliwa katika swala na sijda mbili za kusahau. Vile vile ni wajibu kuelekea Qibla kwa ajili ya swala yoyote ya wajibu, ikiwemo Swala ya tawaf, na Swala ya kumswalia maiti. Pia ni wajibu kumwelekeza Qibla mtu aliye katika hali ya kukata roho na wakati wa kumzika, na wakati wa kumchinja mnyama.

Ama katika swala za sunna ni wajibu kuelekea Qibla katika hali ya utulivu tu, na wala sio wajibu katika hali ya kutembea na kupanda chombo cha kusafiria.

Watu Wa Qibla

Watu wa Qibla, watu wa Qur’an, watu wa shahada mbili na Waislamu, yote hiyo ni misamiati iliyo katika maana moja. Ama lile jina la ‘Wafuasi wa Muhammad’ (Mohammedan), ni jina tulilobandikwa na maadui wa Uislamu, wakiwa na maana kwamba sisi ni wafuasi wa mtu na wala sio wa dini ya Mwenyezi Mungu; kama Mabudha ambao ni wafuasi wa Budha na Wazaradashti ambao ni wafuasi wa Zaradasht.

Kwa vyovyote vile lengo la kifungu hiki ni kuzindua kwamba umma wa Kiislamu, pamoja na kutofautiana miji yake, rangi na lugha, lakini unakusanywa na kuwa pamoja na misingi ya aina moja, ambayo ni ghali na yenye thamani zaidi kuliko uhai.

Kwa sababu Waislamu wanadharau maisha kwa ajili ya misingi hiyo na wala hawawezi kuidharau misingi hiyo kwa ajili ya maisha. Misingi hiyo ni pamoja kumwamini Mwenyezi Mungu na kitabu chake, kumwamini Muhammad (s.a.w.w) na sera yake na kuswali kwa kuelekea Qibla. Basi mwenye kumkufurisha mwenye kuswali kwa kuelekea Qibla na akamtoa katika idadi ya Waislamu, atakuwa amei- dhoofisha nguvu ya Uislamu na atakuwa amelichana jina la Waislamu, na kusaidia maadui wa dini, atake asitake.

Na hakika wale waliopewa kitabu wanajua kwamba huo ni haki itokayo kwa Mola wao.

Makusudio ya waliopewa kitabu ni Mayahudi na Wakristo, na wala sio Mayahudi peke yao, kama ilivyosemwa. Kwa sababu neno linaenea, na wala hakuna dalili ya kuhusisha.

Wafasiri wametofautiana katika dhamiri ya neno Annahul-haqq kwamba je ni huo Msikiti au ni huyo Mtume? Sababu ya kutofautiana ni kwamba Mwenyezi Mungu nyuma amemtaja Mtume kwa kusema: “Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako” na vile vile ametaja Msikiti Mtakatifu.

Sisi tuko katika upande wa wanaosema kuwa dhamiri inarudia Msikiti kwa sababu ndilo tamko la karibu zaidi, na dhamiri inarudia tamko la karibu zaidi.

Kwa hiyo maana yanakuwa, watu waliopewa kitabu wanajua kabisa kwamba Ibrahim (a.s.) ni baba wa Mitume na ni mkubwa wao ambaye alijenga Nyumba Tukufu (Al Ka’aba), lakini wao wameikataa kwa vile tu, iko mikononi mwa Waarabu ambao wanaitumikia na kuihami. Lau isingelikuwa mikononi mwa Waarabu, Mayahudi wangelikuwa wa kwanza kuitukuza na wangeliiheshimu sana.

Na hao waliopewa kitabu hata ukiwaletea hoja za kila namna hawata- fuata Qibla chako.

Yaani hawafuati mila yako, sembuse kufuata Qibla chao. Nao hawana hoja yoyote isipokuwa ujinga na ukaidi.

Na wala wewe si mwenye kufuata Qibla chao.

Huenda baadhi ya watu wa Kitab walitaraji kuwa Mtume (s.a.w.w) ataru- dia Qibla alichokielekea kwanza, ndipo Mwenyezi Mungu akawakatisha tamaa kabisa kwa kauli yake hiyo; kama alivyomkatisha tamaa Muhammad (s.a.w.w) kuwa wao hawatafuata Qibla chake.

Wala baadhi yao si wenye kufuata Qibla cha wengine.

Mayahudi wanaswali kuelekea Magharibi na Wakristo wanaelekea Mashariki, wala kundi moja haliwezi kulifuata kundi jingine, vipi wataweza kufuata Qibla chako ewe Muhammad? Bali hata hao Mayahudi wanatofautiana; kama walivyo Wakristo. Mauaji yaliyotokea kati ya Wakatoliki na Waprotestant, hayana mfano wa fedheha yake katika zama zote.

Na kama ukifuata matamanio yao baada ya kukufikia elimu, utakuwa miongoni mwa madhalimu.

Ni muhali kuwa Mtume afuate matamanio yao, kwa sababu yeye ni masum (mwenye kuhifadhiwa na madhambi), lakini lengo la makatazo haya ni kumpa nguvu Mtume katika kuamiliana kwake na Mayahudi na kusimama nao imara, na kwamba hakuna heri yoyote ya kupatana nao wala hakuna,tumaini lolote kwao. Haliwezi kufaa jaribio lolote la kuwazuia na vitimbi na ufisadi wao. Kwa sababu wao wana maumbile ya shari.

Kupinga haki na kumfanyia uovu anayewafanyia wema. Yamekwishaelezwa maelezo zaidi katika kufasiri Aya ya 120.

Uislamu Na Watu Wenye Upendeleo Na Dini Zao

Ni jambo lenye kuingia akilini kwamba wataalamu wanaweza kuhitilafi- ana katika aina yoyote ya masuala yasiyokuwa ya kidini. Baada ya kukumbushana na kudurusi, huafikiana katika lile walilohitilafiana. Hilo limekwishatokea.

Ama wakihitalifiana katika masuala ya dini mbali mbali, basi kuafikiana kwao ni muhali, hata kama zitakuwepo dalili elfu. Imethibiti kwa wataalamu wa elimu ya saikolojia, kwamba watu kubadili tabia yao ni rahisi zaidi tena sana kuliko kubadili dini yao. Hilo ni kwamba watu wengi hutegemea dini za mababa na mababu. Hakuna dini iliyojulikana kukataza kufuata mababu isipokuwa Uislamu ambao umetegemea akili peke yake katika kuthibitisha misingi yake.

Mwenye kuangalia Aya za Qur’an na Hadith za Mtume ataziona zimetilia umuhimu kufuatilia akili kwa kiasi kile kile zinavyoitilia umuhimu kumwamini Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Imani hiyo haiepukani kabisa na nuru ya akili timamu katika kuongoka kwake.

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّ فَرِيقًا مِنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ {146}


W


ale tuliowapa Kitabu wanamjua yeye kama wanavyowajua watoto wao. Na hakika kundi katika wao wanaificha haki na hali wanaijua.

الْحَقُّ مِنْ رَبِّكَ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ {147}


HakiniiliyotokakwaMola wako. Basi usiwe miongoni mwawanaofanyashaka.

  • 1. Swala za Sunna za usiku wa manane.