read

Aya 183-185: Mmelazimishwa Kufunga

Maana

Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kufunga kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu.

Saumu ni miongoni mwa ibada muhimu, na ni katika dharura za dini, kama ilivyo wajibu Swala na Zaka. Katika Hadith imesemwa: “Uislamu umejengwa katika mambo matano: Kushuhudia kuwa hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wake (shahada), kusimamisha swala, kutoa zaka, kufunga mwezi wa Ramadhan na kuhiji Makka kwa anayeweza.

Mafaqihi wametoa fatwa kwamba yeyote mwenye kukana wajibu wa saumu, basi amekuwa murtadi (si Mwislamu tena) na ni wajibu kumuua. Na mwenye kuamini kuwa saumu ni wajib, lakini akaiacha kwa kupuuza ataaziriwa kutokana na vile anavyoona hakimu wa sharia. Kama akirudia ataaziriwa mara ya pili. Akirudia tena atauawa, wengine wamesema atauawa mara ya nne.

Saumu ni ibada ya zamani aliyoifaradhisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa watu waliotangulia, kwa namna inayotofautiana na yetu sisi Waislamu, kwa kiasi chake namna yake na wakati wake. Kufananishwa hapa kumekuja kwa uwajibu tu, bila ya kuangalia sifa, idadi ya siku na wakati wake. Na kufananisha kitu sio lazima kiwe sawa kwa njia zote.

Ili mpate kuwa na takua.

Wafasiri wengi wamesema kuwa jumla hii inaonyesha hekima ya saumu ambayo ni mazoezi ya mwenye kufunga kuweza kuthibiti nafsi, kuacha matamanio ya haramu na kuwa na subira (uvumilivu). Hadith inasema: “Saumu ni nusu ya subira.” Imam Amirul Mumini (a.s.) anasema: “Kila kitu kina zaka (utakaso) na zaka ya mwili ni kufunga.” Amesema tena: “Mwenyezi Mungu amefaradhisha saumu kwa majaribio ya ikhlasi ya viumbe...”

Kimsingi, ni kwamba kila maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake ni majaribio ya ikhlasi ya viumbe, lakini saumu ina taklifa kubwa, kwa sababu kuna kushindana na nafsi na kupambana, kuweza kuidhibiti na mambo inayoyapendelea ambayo ni chakula, kinywaji na matamanio ya kimwili.

Kwa siku maalum za kuhisabika

Hizo ni siku za Ramadhan, kwa sababu Mwenyezi Mungui hakutufaradhishia zaidi ya Ramadhan.

Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi, au yuko safarini, basi atimize idadi katika siku nyingine. Na wale wanaoweza kwa shida, watoe fidia kwa kumlisha maskini.

Mwenyezi Mungu ametaja katika Aya hii mambo matatu ya kuruhusiwa kufungua Ramadhan ambayo ni Maradhi, Safari na Uzee.

Maradhi anayoruhusiwa mtu kufungua ni kuwa mtu ni mgonjwa ambaye kama atafunga maradhi yake yatazidi, au kuzidi siku za ugonjwa. Au pengine ni mzima, lakini anaogopa kama atafunga atazukiwa na maradhi mapya. Ama udhaifu tu, hauwezi kumruhusu mtu kufungua, madamu anaweza kustahmili na mwili wake uko salama.

Ikiwa mgonjwa atang’ang’ania kufunga pamoja na kuthibitika madhara, basi saumu yake itakuwa batili na ni wajibu kwake kulipa sawa na aliyefungua bila udhuru.

Imethibiti kwa upande wa Sunni na Shia kwamba Mtume (s.a.w.w) amesema; “Si wema kufunga safarini”, Katika Tafsir Al-Manar imekuja Hadith mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Mtume mtukufu: “Mwenye kufunga safarini ni kama mwenye kufungua akiwa nyumbani.”

Katika waliotaja Hadith hii ni Ibn Maja na Tabari. Razi anasema: “Wanavyuoni wa kisahaba wamesema kuwa ni wajibu kufungua kwa mgonjwa na msafiri kwa hali yoyote ile kutokana na kutokuwepo amri ya kufunga. Na hiyo ndiyo kauli ya Ibn Abbas na Ibn Umar. Vile vile Daud bin Ali Al-Asfahani.

Kutokana na hali hiyo, kufungua safarini ni wajibu na wala sio ruhusa tu, Yaani haifai kufunga kwa msafiri kwa hali yoyote ile kutokana na kutokuwepo amri ya kufunga. Dalilli yenye nguvu zaidi juu ya hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewajibisha kulipa kwa safari kwa namna ile ile aliyowajibisha kwa maradhi, pale aliposema: Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au yuko safarini, basi (atimize) hisabu katika siku nyingine

Na wala hakusema ukitaka fungua (utimize ) hisabu katika siku nyengine. Na kukadiria hivyo ni kinyume na dhahiri; wala hakuna haja ya kukadiria mambo mengine ikiwa maana yanasimama bila ya kukadiria. Ama ruhusa ya tatu ya kufungua, ni uzee. Mwenyezi Mungu ameonyesha hilo kwa kauli yake: Na wale wanaoweza kwa shida, watoe fidia kwa kumlisha masikini.”

Hukumu hii inamhusu mzee aliye dhaifu kwa sababu ya ukongwe awe mume au mke. Kuweza kwa shida ni kufanya kitu kwa shida na mashaka sana. Huyu anahiyarishwa kati ya kufunga au kufungua pamoja na kutoa fidia ambayo ni kuwalisha maskini. Kuna Hadith sahihi kuhusu hilo kuto- ka kwa Ahlul Bait (a.s.)

Na atakayefanya heri kwa kujitolea basi ni bora kwake.

Yaani mwenye kuzidisha kulisha zaidi ya maskini mmoja au kumlisha masikini mmoja zaidi ya kiasi cha wajibu, basi ni bora kwake. Anayo hiari ya kumwita maskini muhitaji amlishe mpaka ashibe au ampe chakula cha unga au nafaka anachokula, kiasi kisichopungua gramu mia nane (800gm). Inaruhusiwa kumpa pesa zenye thamani ya chakula kwa sharti ya kumwambia: “Ifanye ni thamani ya chakula chako.”

Na kufunga ni bora kwenu.

Yaani mzee mume au mke walio wakongwe, ingawaje wana hiyarishwa kati ya kufungua na kufunga, lakini wakihiyari kufunga, ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kufungua na kutoa fidia.

Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa katika mwezi huo Qur’an.

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Mwenyezi Mungu alipohusisha kufunga katika mwezi wa Ramadhan, amebainisha kwamba hekima katika hili ni kuwa Qur’an, ambayo juu yake ndio kuna mzunguuko wa dini na imani, iliteremshwa katika mwezi huo.

Kisha akanakili mwenye Majmaul-Bayan kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwa njia ya Sunni na Shia kwamba: Sahifa za Ibrahim (a.s.) ziliteremshwa siku ya tatu ya mwezi wa Ramadhan, Tawrat ya Musa (a.s.) siku ya sita, Injil ya Isa (a.s.) siku ya kumi na tatu , Zaburi ya Daud (a.s.) siku ya kumi na nane na Qur’an ilimshukia Muhammad (s.a.w.w) siku ya ishirini na nne.

Unaweza kuuliza: Hakika kauli yake Mwenyezi Mungu. “Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa katika mwezi huo Qur’an” kwa dhahiri inafahamisha kuwa Qur’an imeteremshwa yote katika mwezi wa Ramadhan na inavyojulikana ni kuwa Qur’an iliteremshwa kwa vipindi katika muda wote wa Mtume ambao ni miaka ishirini na tatu?

Jibu: Makusudio ni kwamba kushuka kwake kulianza katika mwezi wa Ramadhan, sio kwamba imeteremshwa yote katika mwezi huo. Na usiku ambao ilishuka Qur’an unaitwa Laylatul-Qadr, yaani, usiku wa cheo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema: “Hakika sisi tumeiteremsha (Qur’an) katika usiku uliobarikiwa ...” (44:3). Zaidi ya hayo ni kwamba msahafu unaitwa Qur’an na sehemu yake pia inaitwa Qur’an.

Ama kauli ya anayesema kwamba Mwenyezi Mungu aliiteremsha Qur’an kutoka Lawhil-Mahfudh, iliyoko juu mbingu ya saba, na kuileta katika mbingu ya dunia kwa mkupuo mmoja katika usiku wa Laylatul-Qadr, kisha akaiteremsha kwa Muhammad (s.a.w.w) kwa vipindi, kauli hii haina dalili yoyote.

Kuwa mwongozo kwa watu na upambanuzi.

Upambanuzi ni kupambanua kati ya haki na batili na kati ya heri na shari.

Tumekwishaeleza maana ya uongozi katika kufasiri Aya ya pili, na kwamba Qur’an si kitabu cha Falsafa, Historia au elimu ya maumbile, isipokuwa ni ufumbuzi, uongozi na rehma. Na kauli yake Mwenyezi Mungu “kuwa mwongozo kwa watu” inafahamisha kuwa mawaidha, hekima na viaga na yote ambayo yako katika Qur’an, yanafahamiwa na watu wote wala hayahusiki na kufahamiwa na mujtahidi au watu mahsusi.

Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na aufunge.

Yaani mtu ambaye hayuko safarini katika mwezi huu ni wajibu kwake kufunga, wala haifai kwake kufungua bila ya udhuru wowote. Linalofahamisha kuwa makusudio ya neno shahida ni kuwa mjini, ni kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia isemayo: “Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini basi atimize hisabu katika siku nyingine.

Amerudia kutaja ugonjwa na safari kwa kutilia mkazo kwamba katika mwezi wa Ramadhan kunajuzu kufungua, ili kuwajibu wale wanaoshikilia kwamba kufungua hakujuzu kwa hali yoyote.

Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi wala hawatakii yaliyo mazito.

Kwa dhahiri ya mfumo wa maneno ulivyo, ni kwamba jumla hii ni sababu ya kujuzu kufungua katika hali ya ugonjwa, safari na uzee, lakini kwa uhakika ni sababu ya hukumu zote. Imekuja Hadith isemayo: “Wafanyieni wepesi (watu) wala msiwafanyie uzito na wapeni habari za furaha wala msiwafukuze.”

Mwenye kusema kuwa kufungua ni amri na wala sio ruhusa atakuwa amefasiri kauli yake Mwenyezi Mungu: “Anawatakia yaliyo mepesi”, kwamba Mwenyezi Mungu anawatakia mfungue katika safari na hataki mfunge. Na mwenye kusema kuwa kufungua ni ruhusa na wala sio amri atakuwa amefasiri kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anawataka muwe na wasaa katika mambo yenu na kuchagua lile ambalo ni jepesi kwenu.

Ikiwa kufungua ndio wepesi kwenu sawa; au ikiwa kufunga ndio kwepesi sawa. Ikiwa yule ambaye inakuwa wepesi kwake kufunga katika mwezi wa Ramadhan na kuona uzito kulipa, basi kufunga ni bora. Hakuna anayetia shaka kwamba kuzingatia dhahiri ya tamko kunatilia nguvu maana haya. Lau si Hadith sahihi kutoka kwa Ahlul Bait kutokana na babu yao (s.a.w.) tungelisema kwamba kufungua katika safari ni ruhusa na wala sio amri.

Na mtimize hisabu hiyo.

Hii ni sababu ya kulipa alikowajibisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake: “Basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.” yaani ni juu yenu kulipa saumu kwa idadi ya siku mlizofungua katika mwezi wa Ramadhan, kwa sababu ya maradhi na safari, ili itimie idadi ya siku za mwezi kamili ambazo mara nyingine huwa thelathini au ishirini na tisa.

Na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amewaongoza na ili mpate kushukuru.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametubainishia hukumu za dini Yake, ili tumtukuze na tumshukuru. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: “Makusudio ya kumtukuza Mwenyezi Mungu, ni takbira za Idd baada ya swala ya Magharibi ya usiku wa Idd, Isha na Asubuhi, na vile vile baada ya swala ya Idd kwa mujibu wa madhehebu yetu; yaani takbira inayokaririwa baada ya swala ya Idd ambayo husomwa hivi: “Allahu Akbar, Allahu Akbar, Lailaha illa llahu Wallahu Akbar, Allahu
Akbar wa lillaahilhamd; Allahu Akbar alaama hadaana.”

Maana yake ni: Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, hapana Mola mwengine isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi kwa aliyotuongoza.

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ {186}


NawajaW


anguwatakapokuulizahabari


Y


angu,Miminiko karibu. Naitikiamaombiya mwombaji anaponiomba; Basinawaniitikienawaniamini,iliwapatekuongoka.