read

Aya 228: Waliotalikiwa

Maana

Na wanawake waliopewa talaka wangoje tohara tatu.

Tamko la waliopewa talaka kwa dhahiri ni lenye kuenea kwa yeyote yule aliyepewa talaka, awe anatoka hedhi au amekoma, muungwana au kijakazi mwenye mimba au asiyekuwa nayo, mkubwa au mdogo asiyetimiza miaka tisa.

Lakini dhahiri hiyo siyo makusudio yake. Kwa sababu baadhi ya wanaotalikiwa hawana eda, kwa tamko la Qur'an: "Enyi mlioamini Mtakapowaoa wanawake wenye kuamini kisha mkawapa talaka kabla ya kuwagusa basi hamna eda juu yao mtakayaoihisabu..."(33:49)

Pia aliyekoma. Mafaqihi wa Kishia wanasema kwamba hana eda hata kama ameingiliwa na mume; vile vile mtoto mdogo chini ya miaka tisa.

Na kuna wanawake wanaokaa eda kwa tohara mbili kama mjakazi. Wengine wanakaa miezi mitatu sio tohara tatu; huyo ni yule ambaye yuko katika rika la kutoka hedhi, lakini hatoki; kama ambavyo mwenye mimba muda wake wa kukaa eda unaisha wakati atakapozaa. Mwenyezi Mungu anasema;

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَنْ يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ۚ {4}


"...Na wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa..." (65:4)

Kwa hivyo basi makusudio ya waliopewa talaka katika Aya, ni yule aliyeingiliwa akiwa na umri wa zaidi ya miaka tisa, asiwe na mimba na awe mwenye kutoka hedhi.

Wamefasiri Shia, Malik na Shafii neno Qurui kwa maana ya tohara na makusudio ya tohara ni siku za kutoharika baina ya hedhi mbili. Kama akiachwa wakati wa mwisho mwisho wa tohara yake, itahisabiwa pia katika eda na atakamilisha tohara mbili. Ama Hanafi na Hambal wamefasiri neno Qurui kwa maana ya hedhi tatu.

Wala haijuzu kwao kuficha alichokiumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao.

Ili kufahamu hakika ya jumla hii itabidi kuanza kueleza haya yafuatayo: Mafaqihi wa Kisunni wameigawa talaka kwenye mafungu mawili: ya sunna na bid'a (uzushi). Hebu tuwaachie wenyewe tafsiri ya ‘Sunna’ na Bid'a (talaka ya kawaida na uzushi)
Katika kitabu Al-Mughni cha Ibn Quddam Juzuu 7 Uk. 98 chapa ya tatu anasema : "Maana ya talaka ya sunna ni talaka ambayo inaafiki amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume wake, nayo ni talaka katika hali ya tohara asiyomwingilia." Na katika kitabu hicho hicho Uk. 99 amesema: "Hakika talaka ya Bid'a ni talaka katika hali ya hedhi au katika hali ya tohara aliyomwingilia."Amesema Razi katika tafsiri ya Aya ya 1 katika Sura ya 86; "Utohara katika talaka ni lazima, vyinginevyo haitakuwa ya sunna."

Kwa hali hiyo basi, kupewa talaka mke katika hali ya hedhi au katika hali ya utohara ambapo mke ameingiliwa, siyo talaka ya kisheria, bali ni Bid'a (uzushi) na kila uzushi ni upotevu na kila upotevu ni motoni.

Ama kumtaliki mke katika tohara asiyoingiliwa na mumewe, inakuwa ndiyo talaka iliyofuata sharia ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapo ndio inafafanulika siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.): "wala haijuzu kwao kuficha alichokiumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao." Kwa sababu maarifa ya kutokea talaka kwa njia ya kawaida au uzushi ndiyo yatakayofahamisha hali ya mwenye kuachwa, na kwamba je ana hedhi au yuko tohara.

Kimsingi njia ya kujua sifa mbili hizi (tohara na hedhi) inamtegemea mwanamke mwenyewe. Kwa hivyo itabidi aaminiwe maadamu haujajuliwa uwongo wake. Imam Jaffar Sadiq amesema; Mwenyezi Mungu amewachia wanawake mambo matatu: Tohara, hedhi na mimba." Katika riwaya ya pili imeongezewa eda.

Shia wanaafikiana na Sunni kwamba talaka ikiwa katika hedhi au katika tohara aliyoingiliwa, inakuwa ya uzushi na ikiwa ni katika tohara ambayo hakuingiliwa inakuwa ni ya sharia ya Mtume (s.a.w.w.).

Lakini Shia wamesema Talaka ya uzushi sio talaka kabisa; yaani si sahihi. Na talaka sahihi inayomtenganisha mume na mke, ni talaka ya kawaida; yaani inayotokea katika tohara asiyoingilwa. Sunni wanasema hapana; talaka ya uzushi ni sahihi na inahusika na athari zote za talaka, isipokuwa tu yule mwenye kuacha atapata dhambi.

Hiyo ni kusema kuwa Sunni hawatofautishi kati ya talaka ya kawaida na ya uzushi katika kusihi kwake, isipokuwa wanatofautisha katika kupata madhambi na uasi tu. Ama Shia wametofautisha kati ya hizo mbili, kwa upande wa usahihi, na si upande wa dhambi.

Ikiwa wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Hii ni kuogopesha na kuweka utisho kwa wenye kuficha yaliyo tumboni na wala sio sharti la kuwajibisha kusadiki. Kwa sababu maana yake ni kwamba imani inazuwiya uongo; kama vile kumwambia mtu: "Ikiwa unamuogopa Mwenyezi Mungu usiseme uongo."

Tumetangulia kueleza kuwa mwenye kutalikiwa ndiye atakayeamini- wa katika tohara, hedhi na mimba. Maana yake ni kuwa itakayotegemewa ni kauli yake katika kubaki eda na kwisha kwake. Ilivyo ni kwamba haki ya mume katika kurejea, itategemea kutokwisha kwa eda; kama ambavyo muungano (wa nasaba mtoto) unaambatana na utohara na hedhi. Vile vile kusihi talaka na kutosihi kwa upande wa mafaqihi wa kishia.

Akiwa na hedhi na akasema kuwa ni tohara, basi talaka haitakuwa, na atabaki ni mke wa mtu; kama akisema eda yake imekwisha kwa tohara na kumbe bado, haki ya mume ya kurejea itafutika. Lakini akiolewa katika hali hiyo atakuwa mzinifu. Kwa sababu hii na nyinginezo, ndio Mwenyezi Mungu akawakataza wanawake kuficha vilivyo katika matumbo yao na akawakemea kwa hilo.

Na waume zao wana haki ya kuwarudia katika muda huo, kama wakitaka kufanya suluhu.

Kauli yake Mwenyezi Mungu "katika muda huo" ni ule muda wa kungo- jea (muda wa eda). Maana yanayopatikana ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kubainisha wajibu wa eda, ametaja haki ya mwenye kutaliki kumrejea mtalaka wake katika muda wa eda ikiwa ni talaka rejea.

Hiyo ni haki yake awe mke hakuridhia au ameridhia; wala kurejea mke hakuhitaji kufunga ndoa tena na mahari, kama vile ambavyo hakuhitajii ushahidi kwa mafaqihi wa Kishia. Utakuja ubainifu wake zaidi kwenye Sura ya Talaka (65).

Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu "kama wakitaka kufanya suluhu" ni suluhu kati ya mume na mke bila ya kukusudia madhara katika kurejea.

Unaweza kuuliza: Kama mume akimrejea mtalaka wake ndani ya eda kwa kukusudia madhara sio suluhu, je kurejea kutakuwa sahihi au la? Jibu: Kutaswihi kurejea, lakini mume atapata dhambi, kwa sababu kukusudia suluhu ni hukumu ya taklifa ambayo ni kuhalalisha kurejea na wala sio sharti ya maudhui yenyewe ya kurejea na kuswihi kwake.

Nao (wanawake) wanayo haki sawa na ile iliyo juu yao kwa sharia.

Makusudio ya kufanana haki hapa sio ya kufanana kijinsia, kwamba yanayostahiki kwa mume kama vile mahari na posho, basi na mke pia naye atoe, la; isipokuwa makusudio hapa ni kuwa sawa wajibu na yanayostahiki. Mafaqihi wanasema haki ya mume kutoka kwa mkewe ni kutiiwa kitandani, na haki ya mke kutoka kwa mume ni kumlisha na kumvisha.

Mwenye tafsiri Al Manar anasema haki ya mume kwa mke na haki ya mke kwa mume ni ile kawaida ya mambo ya watu, isipokuwa yale yaliyoharimishwa katika sharia. Linaloonekana kikawaida kuwa ni haki kwa mke na mume, basi litakuwa ni sawa mbele za Mwenyezi Mungu.

Yanayodhihirikia kutokana na mfumo wa Aya ni kwamba haki iliyo kwa mke ni eda, ukweli katika kuitolea habari eda na kuacha kupinga kurejea kulikokamilisha masharti. Na iliyo juu ya mume ni kukusudia suluhu katika kurejea na usuhuba mzuri na wala sio madhara. Ama haki nyingine za mume na mke ziko mbali na Aya hii.

Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao.

Wamehitalifiana wanavyuoni na wafasiri katika makusudio ya daraja hii inayomtofautisha mwanamume na mwanamke. Ikasemwa kuwa ni akili na dini; ikasemwa ni mirathi na pia ikasemwa kuwa ni ubwana; yaani inam- pasa mke kumtii mume na kumsikiliza.

La kushangaza ni kwamba wengine wamefasiri daraja ya juu kwa maana ya ndevu; kama ilivyoelezwa katika kitabu Ahkamul-Qur'an cha Abu bakr Al-Andalusi.

Sio mbali na maana kuwa makusudio ya daraja ni kuijaalia talaka na kure- jea mikononi mwa mume na wala sio mwa mke.

Mwanamume Na Mwanamke Katika Sharia Ya Kiislamu

Uislamu umezitangulia sharia na kanuni zote katika kumkomboa mwanamke na kuzithibitisha haki zake, baada ya kuwa mwanamume alimtumia mwanamke kama bidhaa tu, akamfanya kama mnyama, ambapo mpaka hivi karibuni Ulaya na Marekani walikuwa wakifanya hivyo.

Uislamu unapomtofautisha mwanamke na mwanamume unamtofautisha kwa tofauti za kimaumbile au maslahi ya jamii. Ni jambo lisiloingia akilini wala uadilifu kufanya usawa katika kila kitu kati ya yule mwenye kujishughulisha zaidi na magauni, mitindo ya mavazi, kuchana nywele, n.k.; na yule anayehisi majukumu ya mwenzake (mkewe) na watoto na kustahamili mashaka kwa ajili yake (mke) na kwa ajili yao wote.

Mafaqihi wa Kiislamu wamezitaja tofauti kati ya mwanamume na mwanamke katika hukumu za kisharia kama ifuatavyo:

1. Fidia ya kuuliwa mwanamke ni nusu ya mwanamume.

2. Kutoa talaka na kurejea kuko mikononi mwa mume sio mke.

3. Haijuzu kwa mke kusafiri, na kutoka nyumbani kwake isipokuwa kwa kukubali mume, lakini mume anaweza kufanya hivyo.

4. Si wajibu kwa mwanamke kuswali Ijumaa, hata yakitimia masharti.

5. Haijuzu mwanamke kutawalia jambo wala kuwa Kadhi, isipokuwa kwa Abu Hanifa anasema inafaa katika haki za watu lakini sio za Mungu.

6. Hawezi kuwa Imam wa swala ya wanaume, lakini mwanamume anaweza kuwa Imam wa wanawake.

7. Ushahidi wake haukubaliwi katika mambo yasiyo husiana na mali; hata akiwa pamoja na waume, isipokuwa katika maswala ya uzazi, unakubaliwa akiwa pamoja na waume kwa kuchukulia kuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na wa mwanamume mmoja.

8. Katika mirathi mtoto wa kike anapata nusu ya fungu la mtoto wa kiume.

9. Ni lazima ajifunike mwili wake wote-hata nywele-mbele za waume wasio maharimu, lakini kwa mwanamume mbele za wanawake wajibu wake ni kustiri tupu mbili tu.

10. Hapigani jihadi wala hatoi kodi wala hauliwi vitani iwapo hajapigana.

11. Mama hashirikiani na baba katika usimamizi (uwalii) wa mtoto mdogo au katika matumizi ya mali yake (mtoto).

12. Haifai kushindana mashindano ya farasi na kulenga shabaha.

13. Mafaqihi wametoa fatwa kuwa fidia ya aliyeuawa kimakosa inachukuliwa na ndugu zake wa karibu kwa upande wa baba tu; kama vile kaka, ami na watoto wao lakini sio wakike.

14. Mwanamke akimuua mwanamume, atauliwa bila ya kutoa fidia, lakini kama mwanamume akimuua mwanamke, basi hawezi kuuliwa mpaka walii wa mwanamke atoe nusu ya fidia kwa warithi wa muuaji.

لطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ ۗ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَنْ تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَنْ يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّهِ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا ۚ وَمَنْ يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّهِ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ {229}

Talaka ni mara mbili; kisha ni kushika kwa wema au kuacha kwa ihsani. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlichowapa, isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, itakuwa hapana ubaya kwao kupokea ajikomboleacho mke. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiipetuke. Na watakaoipetuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhalimu.

فَإِنْ طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِنْ بَعْدُ حَتَّىٰ تَنْكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ ۗ فَإِنْ طَلَّقَهَا فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَنْ يَتَرَاجَعَا إِنْ ظَنَّا أَنْ يُقِيمَا حُدُودَ اللَّهِ ۗ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ يُبَيِّنُهَا لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ {230}

Na kama amempa talaka ( ya tatu) basi si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine. Na akimwacha, basi hapo si vibaya kwao kurejeana wakiona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wajuao.