read

Aya 229-230: Talaka Ni Mara Mbili

Maana

Talaka ni mara mbili.

Waarabu katika zama za Ujahiliya (kabla ya Uislamu) walikuwa na talaka, eda na kurejeana katikati ya eda. Lakini talaka haikuwa na idadi maalum. Mtu aliweza kumwacha mkewe mara mia na kumrudia. Kwa hivyo mwanamke anakuwa ni kitu cha kuchezewa mikononi mwa mwanamume.

Kuna riwaya inayoeleza kuwa mtu mmoja alimwambia mkewe: "Sitakukurubia milele, na pamoja na hivyo utabaki kwangu tu, hutaweza kuolewa na mwingine." Mke akauliza: "Itakuwaje hivyo?" Mume akajibu: "Nitakuacha mpakaukikaribia muda wa kwisha eda nikurudie, halafu nikuache tena, n.k." Mwanamke akamshtakia Mtume (s.a.w.w.).

Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii: "Talaka ni mara mbili" yaani talaka ambayo mnaruhusiwa kurejea ni talaka ya kwanza na ya pili tu! Ama ya tatu si halali kurejea, mpaka mke aolewe na mume mwingine; kama alivyosema Mwenyezi Mungu; "Na kama amempa talaka si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine."

Kisha ni kushika kwa wema au kuacha kwa ihsani

Mume akimwacha mkewe mara ya pili ana hiyari kati ya mambo mawili akiwa katika eda. Jambo la kwanza ni kumrejea kwa kukusudia kupatana na kutangamana. Huku ndiko kumweka kwa wema. Jambo la pili, ni kumwacha mpaka ishe eda yake, amtekelezee haki yake asimtaje kwa ubaya baada ya kutengana wala asimkatishe anayetaka kumwoa baada yake. Huko ndiko kumwacha kwa ihisani.

Unaweza kuuliza, wafasiri wengi wamefasiri kumwacha kwa ihisani ni talaka ya tatu na wakatoa ushahidi wa Hadith ya Mtume (s.a.w.w.). Sasa imekuwaje wewe kuipinga kauli yao na kufasiri kuacha, kuwa ni kupuuza kumrejea katika muda wa eda?

Jibu: Neno kumwacha, kwa dhati yake linawezekana kuwa ni talaka ya tatu na linawezekana kuwa ni kumnyamazia mtalaka na kuwacha kumrejea. Lakini kwa kuchunga mfumo ulivyo, maana ya neno inarudia maana ya pili; yaani kuacha kurejea, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu "Kama amempa talaka basi mwanamke huyo si halali kwake baada ya hapo."

Inatokana na kumweka; maana yake yanakuwa ni akimwacha baada ya kumweka na akamrejea katikati ya talaka ya pili itakuwa talaka ni ya tatu wala si halali kwa mwenye kuacha kumwoa mpaka aolewe na mume mwingine. Kwa hivyo haiwezekani kuwa imetokana na kumweka kwa maana ya talaka ya tatu, kwa sababu maana itakuwa alimwacha mara ya nne baada ya kumwacha mara ya tatu. Na ilivyo ni kwamba hakuna talaka ya nne katika Uislamu. Ama Hadith iliyofasiri kumweka kwa maana ya talaka ya tatu si thabiti.

Talaka Tatu

Madhehebu manne ya Kisunni yameafikiana kuwa atakaye mwambia mkewe: Nimekuacha talaka tatu au akisema: Nimekuacha, nimekuacha, nimekuacha, basi itakuwa ni talaka tatu na itakuwa haramu mpaka aolewe na mume mwingine. Shia wamesema itakuwa ni talaka moja tu, na ni halali kumrejea, maadamu yuko katika eda.

Katika tafsiri ya Al Manar imepokewa kutoka kwa Ahmad bin Hambal katika Musnad yake, na Muslim katika Sahih yake kwamba talaka tatu zilikuwa moja katika zama za Mtume (s.a.w.w.), za Abu Bakr na baadhi ya miaka ya ukhalifa wa Umar, lakini Umar ikamdhihirikia fikra nyingine akasema; "Hakika watu wamefanya haraka katika jambo lililokuwa na upole kwao, lau tungelipitisha."Basi akapitisha (kuwa kusema talaka tatu ni tatu).

Kisha amenakili mwenye tafsiri Al Manar kutoka kwa Al Qayyim kwamba masahaba wote walikuwa wakikubali kwamba talaka tatu hazikutokea kwa pamoja tangu mwanzo wa Uislamu mpaka miaka mitatu ya ukhalifa wa Umar. Vile vile walifutu hivyo jamaa katika masahaba, Tabiina (waliokuwapo baada ya maswahaba) na waliokuja baada ya hao Tabiina (Tabii-Tabiina), na kwamba fatwa juu ya hilo inaendelea kila wakati hata baadhi ya wafuasi wa Maimamu wanne walifutu hivyo.

Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlichowapa.

Katika mlichowapa hapa ina maana kiwe kingi au kichache; yaani ikiwa mume ndiye asiyemtaka mke na akapendelea kumpa talaka, basi si haki kwake kuchukua vile alivyompa zawadi mke au mahari. Mwenyezi Mungu anasema:

وَإِنْ أَرَدْتُمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنْطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا ۚ أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُبِينًا {20}

"Na kama mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke na hali mmoja wao mmempa rundo mali, basi msichukue chochote katika hiyo. Je, mnachukua kwa dhuluma na kwa dhambi iliyo wazi" (4:20)

Hiyo ni ikiwa mume ndiye asiyemtaka mke. Ama ikiwa mke ndiye asiyemtaka mume, basi hapana kizuwizi cha mke kumpa mume kile kinachomridhia ili amwache, ni sawa chenye kutolewa kiwe ni kiasi cha mahari au kichache au zaidi ya mahari. Talaka hii inaitwa Khul'u (kujivua); na mume katika talaka hii hana haki ya kumrejea katika eda maadamu anaendelea kulipwa. Isipokuwa kama huyo mke atabadilisha katikati ya eda.

Kuhusu talaka hii ya khul'u Mwenyezi Mungu anasema: Isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, itakuwa hapana ubaya kwao kupokea ajikomboleacho mke.

Hii ni kuelezea uwezekano wa kuchukua kitu kutoka kwa mke. Mipaka ya Mwenyezi Mungu ni haki na wajibu wa kila mmoja kwa mwenzake (mke na mume). Maana yake: Enyi waume! Msichukue kitu kutoka kwa watalaka wenu kwa sababu yoyote ile, isipokuwa sababu moja tu, ambayo ni ikiwa mke ndiye anayemchukia mume, wala hawezi kuishi naye, kiasi ambacho hali itapelekea kumwasi Mwenyezi Mungu katika kutia dosari haki za unyumba, na huenda mume naye akaogopa kumkabili mke kwa uovu. Katika hali hii, itafaa kwa mke kudai talaka kutoka kwa mume na kumlipa ridhaa; kama vile ambavyo inajuzu kwa mume kuichukua ridhaa hiyo.

Imekuja Hadith kwamba Thabit bin Qays alikuwa amemuoa bint wa Abdulla bin Ubay. Naye alikuwa akimpenda, lakini mke hampendi mume. Na alikuwa amempatia shamba. Mke akaja kwa Mtume (s.a.w.w.) akasema: "Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Mimi na Thabit kichwa changu hakipatani na chake." Thabit akasaili: "Na lile shamba?" Mtume akamwambia bint Abdulla: "Unasemaje?" Akasema: "Ndio, tena na ziada nitampa." Mtume akasema: "Hapana, shamba tu," Basi wakafanyiana khul'u.

Linakuja swali katika aya hii: Kwa nini ikaja dhamiri ya wawili katika "Isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu." Kisha ikaja dhamiri ya wengi kwa kusema: "Na kama mkiogopa". Kwa nini dhamiri zisiafikiane katika jumla mbili?

Jibu: Dhamiri ya wote wawili ni ya mke na mume na dhamiri ya 'mkiogopa' ni ya mahakimu na wasuluhishi; yaani wakiogopa, mahakimu na wasuluhishi kuacha kusimamishwa mipaka ya Mwenyezi Mungu. Makusudio hasa ni kuondoa hofu ya kutoa na kuchukua kwa wote.

Swali la pili: Kwa nini ikaja dhamiri ya wawili katika: Si dhambi juu yao (mume na mke), na tunajua kuwa anayepokea ni mume tu.

Jibu: Hapa inaonyesha kuwa si vibaya kutoa na kuchukua; kwa kufahamu kuwa kujuzu kutoa kunalazimisha kujuzu kupokea.

Swali la tatu: Ikiwa mke na mume wameridhiana kufanya khul'u, mke akatoa mali ili aachwe; lakini uhusiano wao ni mzuri, je, itaswihi khul'u na itafaa mume achukue fidia?

Madhehebu zote nne zimesema khul'u itafaa na itafungamana na athari zote za khul'u.

Shia Imamia wamesema haiswihi hiyo khul'u wala mtaliki hawezi kumiliki fidia, lakini talaka itaswihi na itakuwa ni talaka rejea kwa sharti zake. Wametoa dalili ya kuharibika khul'u na kutojuzu kuchukua fidia kwamba Aya imeshartisha kujuzu hilo kwa kuogopa kuingia katika maasi, kama ndoa ikiendelea. Ama Aya inayosema:

وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً ۚ فَإِنْ طِبْنَ لَكُمْ عَنْ شَيْءٍ مِنْهُ نَفْسًا فَكُلُوهُ هَنِيئًا مَرِيئًا {4}

"Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni zawadi, kama waki- watunikia kwa ridhia ya nafsi zao, katika hayo (mahari) basi kuleni kwa raha." (4:4)

Makusudio ya Aya hiyo ni kwamba anachotoa mke hapo ni zawadi tu, sio badali ya talaka. Hivyo Aya iko mbali na khul'u.

Swali la nne: Kama mume akifanya makusudi ubaya ili apate mali kutoka kwa mke, na mke naye akatoa mali na ikatolewa talaka kwa misingi hii; je, khul'u itakuwa halali? Na je, ni halali kuchukua mali?

Abu Hanifa anasema: "Khul'u ni sahihi, mali ni lazima itolewe na mume ana dhambi."

Shafi na Malik wamesema: "Khul'u ni batili na mali irudishwe kwa mke, kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "... Wala msiwataabishe ili mpate kuwanyang'anya baadhi ya vile mlivyowapa..." (4:19)

Hayo yamo katika kitabu Al- Mughni, cha Ibn Quddama Juz 7, Uk 55 chapa ya 7.

Shia Imamia wamesema: "Haiswihi khul'u, ni haramu kuchukua mali, lakini itakuwa ni talaka rejea kwa kukamilika sharti zake."

Ama sisi tuko katika fikra ya kuwa talaka hiyo ni upuzi tu, sio khul'u wala talaka rejea. Kwa sababu kinachojengeka kwa uharibifu ndio kimeharibika chote. Hayo tumeyafafanua zaidi katika kitabu Fiqhul Imam Jaffar Sadiq Juz 6 mlango wa khul'u kifungu cha Hukumu za khul'u.

Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine. Na akimwacha (mume wa pili), basi hapo hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Maana ni kuwa mwenye kumwacha mkewe mara tatu, basi si halali kwake kumwoa tena mpaka aolewe na mume mwingine kwa ndoa sahihi tena amwingilie. Imekuja Hadith inayosema: "Si halali kwa mume wa kwanza mpaka wa pili amwonje (amwingilie)."

Huyu mume wa pili ndiye anayeitwa muhallil (mhalalishaji); Ni lazima awe ni baleghe, na ndoa iwe ya daima sio ya Mut'a. Zikitimia sharti; kisha mume wa pili akatalikiana naye kwa mauti au talaka na ikaisha eda, basi itafaa kwa mume wa kwanza kufunga ndoa naye tena.

وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ ۚ وَلَا تُمْسِكُوهُنَّ ضِرَارًا لِتَعْتَدُوا ۚ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ ۚ وَلَا تَتَّخِذُوا آيَاتِ اللَّهِ هُزُوًا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَمَا أَنْزَلَ عَلَيْكُمْ مِنَ الْكِتَابِ وَالْحِكْمَةِ يَعِظُكُمْ بِهِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ {231}

Na mtakapowapa wanawake talaka, wakafikia muda wao, basi washikeni kwa wema au waacheni kwa wema. Wala msiwaweke kwa kudhuriana mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo,amejidhulumu mwenyewe. Wala msizifanyie mzaha Aya za Mwenyezi Mungu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na Kitabu alichowateremshia na hekima, kwa kuwaonya. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَنْ يَنْكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُمْ بِالْمَعْرُوفِ ۗ ذَٰلِكَ يُوعَظُ بِهِ مَنْ كَانَ مِنْكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۗ ذَٰلِكُمْ أَزْكَىٰ لَكُمْ وَأَطْهَرُ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنْتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {232}

Na mtakapowapa wanawake talaka na wakafikia muda wao, msiwazuie kuolewa na waume zao, ikiwa wamepatana kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule, miongoni mwenu, anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.