read

Aya 231-232: Mnapowapa Talaka Wanawake

Maana

Na mtakapowapa wanawake talaka, wakafikia muda wao, basi washikeni kwa wema au waacheni kwa wema.
Msemo huu unaelekezwa kwa waumini wote au kwa watu wote; ni kama vile Mwenyezi Mungu ametaka kusema: Enyi waumini! Atakapompa talaka mmoja wenu mkewe.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu kwamba mwenye kupewa talaka ni lazima akae eda, kwamba anaweza kurudiwa na mumewe zikikamili- ka sharti, kwamba ni haramu baada ya talaka ya tatu mpaka aolewe na mume mwingine, na kwamba si halali kuchukua kitu kwa mke kwa ajili ya talaka, isipokuwa ikiwa mke ndiye asiyemtaka mume, baada ya kuyabainisha yote hayo, anatubainishia vile tunavyotakiwa kuchunga haki ya anaekaa eda.

Kuchunga haki kutathibitika kwa kuazimia mwenye kuacha moja kati ya mawili: Kumrejea mtalaka wake wakati inapokaribia kumalizika eda, kwa kukusudia usuluhishi na utangamano mzuri. Na huku ndiko kurejea kwa wema. Au kumwacha bila ya kumtaaradhi kwa ubaya pamoja na kumtekelezea kila analostahiki. Na huku ndiko kumwacha kwa wema.

Kwa hivyo inatubainikia kuwa makusudio ya Aya iliyotangulia siyo makusudio ya Aya hii tuliyonayo. Aya ile iliyotangulia inabainisha kuwa kurejeana ni talaka ya kwanza na ya pili na siyo ya tatu. Na hii inabainisha vile tunavyotakiwa kuwafanyia waliopewa talaka; kama ambavyo makusudio ya kufikilia muda wao ni kukurubia sio kufika hasa.

Wala msiwaweke kwa kudhuriana mkafanya uadui.

Yaani msiwarudie kwa kukusudia kuwaudhi au kuwafanyia ubaya; muwarejee tu kwa makusudio ya kutekeleza haki za unyumba na kusaidiana yale yalio na maslahi kwa wote.

Unaweza kuuliza kwa nini imesemwa kudhuriana, ambapo makusudio ni kuepusha madhara ya mume kwa mke?

Jibu: Kumdhuru mke kunasababisha kudhurika kwa mume pia, kwa sababu ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu juu yake, shutuma za watu kwake, na mke kulipiza kisasi. Hapo ndio unyumba unageuka kuwa Jahannam kwa mume na mke na huenda moto ukaenea kwa jamaa na ndugu. Ndio maana Mwenyezi Mungu anasema: Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu mwenyewe. Yaani si kumdhulumu mke peke yake.

Wala msizifanyie mzaha Aya za Mwenyezi Mungu.

Hiki ni kiaga na kemeo kwa yule mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu katika haki za unyumba. Njia ya kuzifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu, ambaye limetukuka neno lake, ni kwamba kila mwenye kudai kumwamini Mwenyezi Mungu na hakufuata dini kwa sharia zake, halafu akapuuza hukumu zake, halali yake na haramu yake, basi atakuwa amefanya mzaha, atake asitake. Sawa na anayemuahidi mtu kitu hali akiwa na niya ya kutotekeleza. Baadhi ya wahenga wamesema: "Mwenye kutubu dhambi na huku anaendelea nayo ni kama mwenye kumcheza shere Muumba wake."(Mungu apishie mbali!)

Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu.

Miongoni mwa hizo ni kuwa Mwenyezi Mungu ametuumbia wanawake ili tupate utulivu kwao na tusaidiane nao katika yale yenye utengeneo wa familia. Ikiwa tunamwamini Mwenyezi Mungu na tunafuata amri zake kweli, basi ni juu yetu kufanya lile litakaloleta lengo hili na kujiepusha na kila linaloleta uovu katika familia na kuchafua usafi wa maisha ya ndoa.

Na mtapowapa talaka wanawake na wakafikia muda wao, msiwazuie kuolewa na waume zao.

Makusudio ya kufikia muda katika Aya iliyotangulia ni kukaribia kwisha eda na makusudio yake hapa ni kwisha kabisa hiyo eda.

Katika Aya hii kuna mielekezo miwili ya misemo (mnapowapa talaka, na msiwazuie) ambayo wafasiri wamehitilafiana; kwamba, je yote inaelekezwa upande mmoja au pande tofauti?
Kuna wenye kusema kuwa unaelekezwa kwa upande mmoja tu wa waume; na maana yake ni: Enyi waume, mnapowapa talaka wanawake na eda yao ikaisha, basi msiwazuwie kuolewa na waume wengine wanaowaridhia. Kwa sababu mwanamume alikuwa akimhukumu mtalaka wake na kumzuia, kuolewa na mume mwingine baada yake.

Wengine wanasema: Msemo wa kwanza Mtakapowapa talaka, unaelekezwa kwa waume, na wapili msiwazuie, unaelekezwa kwa mawalii; kwa maana ya: Enyi waume, mnapowapa talaka wanawake, basi nyinyi mawalii msiwazuwie watoto wenu kurudiana na waume zao wa kwanza, ikiwa eda imekwisha. Wanaosema hivi wametoa ushahidi wa Hadith ya Mu'ukil bin Yasir.1

Inaeleweka kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mtakapowapa talaka wanawake na wakafikia muda wao msiwazuwie" ni jumla ya pamoja iliyo na sharti, na jawabu lake ni msiwazuie.

Ikiwa sharti ya mwenye kumwambia ni mwingine na jawabu liwe kwa mwingine na maana yawe ni: Enyi waume mtakapowapa talaka wanawake basi nyinyi mawalii msiwazuie, hapa kutakuwa na mkorogano ambao haupaswi kuwapo katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Usahihi hasa ni misemo miwili (sharti na jawabu lake) inaelekezwa kumoja tu kwa waumini wote; sio waume peke yao wala mawalii tu, wala pia sio kwa wote, bali ni kwa waumini. Hali hii inakuja mara nyingi katika maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na maana yanakuwa: Enyi mlioamini mmoja wenu akimpa talaka mkewe, eda ikaisha na akataka kuolewa na mume mwingine au kurudiwa na mumewe wa kwanza, basi msimzuie kama wakipatana kwa wema; yaani wakiazimia kuoana.

Na kauli yake Mwenyezi Mungu: Ikiwa wamepatana kwa wema inafahamisha kuwa mke anaweza kujioza yule anayemridhia, bila ya kumngoja walii.

Unaweza kusema: hakika Aya imeuondoa uwalii (usimamizi) kwa wanawake walioachwa tu, na wala haikuutaaradhi usimamizi kwa wengineo. Kwa hivyo kuuondoa usimamizi kwa wanawali kunahitajia dalili.

Jibu: Kuthibitisha usimamizi ndiko kunakohitajia dalili; ama kuondoa, dalili yake ni ya asili kwamba kila aliyebaleghe mwenye akili mume au mke ni huru katika mambo yake wala hatawaliwi na yeyote, kwa vyovyote atakavyokuwa isipokuwa tu kama atakiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Hayo anawaonywa nayo yule, miongoni mwenu, anayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Hayo ni ishara ya hayo aliyoyataja Mwenyezi Mungu katika hukumu zake. Anaonywa nayo, yaani wanaonyeka nayo wenye imani sahihi. Ama wengineo katika wenye imani mbovu, masikioni mwao mna vizuwizi, hawasikii mawaidha ya Mwenyezi Mungu na hukumu Zake wala uongozi Wake.

Aya hii ni dalili ya wazi kwamba hakuna imani bila ya ucha Mungu na imani sahihi haiepukani na mawaidha, na asiye waidhika wala kunufaika na amri za Mwenyezi Mungu hana hata chembe ya imani.

Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa.

Hayo ni ishara ya mawaidha na kutumia hukumu ya Mwenyezi Mungu katika maisha ya ndoa kwa ujumla na hasa katika waliopewa talaka. Hakuna mwenye shaka kwamba ndoa yenye lengo la utu na kusaidiana katika heri, inaleta ongezeko na usafi katika riziki, usafi wa tabia, heshima na ufanisi kwa watoto. Ama makusudio yakiwa mabaya, basi mwisho wake ni ukafiri, uharibifu, balaa na mashaka katika maisha ya wazazi na watoto.

Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.
Makusudio sio kutupa habari kuwa Yeye ni mjuzi au mjuzi zaidi, hapana. Hilo liko wazi halihiitaji mafunzo wala ufafanuzi. Makusudio hasa ni kutilia mkazo na kuhimiza kutekeleza hukumu Zake Mwenyezi Mungu; hata kama haikutubainikia njia ya manufaa yapatikanayo katika hukumu hiyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hekima yake, haamrishi isipokuwa lenye heri na maslahi na wala si lazima tuijue heri hiyo kwa ufafanuzi; bali inatosha tu kujua kuwa Mwenye kuamrisha na Mwenye kukataza, ni Mjuzi Mwenye hekima, halijifichi lolote Kwake liwe ardhini au mbinguni. Kwa ujumla ni kuwa kuna tofauti kati ya mumin na asiyekuwa mumin. Mumin anaabudu kulingana na kauli ya Mwenyezi Mungu na anafanya amali katika hali ya kuyakinisha kupatikana manufaa, hata kama atashindwa kuyafahamu kwa ufafanuzi.

Ama asiyekuwa mumin hafanyi kitu mpaka ajue au adhani kuwa kuna manufaa anayoyajua yeye mwenyewe kwa akili yake au aongozwe na kiumbe kama yeye, ambapo mara nyingi anaruka patupu na kubainikiwa na kinyume, lakini mumin anakuwa katika amani ya Mwenyezi Mungu na hifadhi Yake.

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَهُ بِوَلَدِهِ ۚ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ ۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَنْ تَرَاضٍ مِنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ۗ وَإِنْ أَرَدْتُمْ أَنْ تَسْتَرْضِعُوا أَوْلَادَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُمْ مَا آتَيْتُمْ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاتَّقُوا اللَّهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {233}

Na wazazi wa kike wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha; na ni juu ya aliyezaliwa mtoto huyo (baba) chakula chao na nguo zao kulingana na desturi. Wala haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa uweza wake. Mzazi (Mama) asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala aliyezaliwa mtoto (baba) kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha (kunyonya) kwa kuridhiana na kushau- riana, basi si kosa juu yao. Na kama mkitaka kuwapa- tia watoto wenu Mama (wengine) wa kuwanyoyesha, basi haitakuwa vibaya juu yenu kama mkitoa mlichowaahidi, kwa desturi. Na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyotenda.
  • 1. Imepokewa kutoka kwa Mu’ukil bin Yasir kwamba yeye amesema: “Nilikuwa na dada aliyeolewa na binamu yake kisha akampa talaka wala asimrejee mpaka ikaisha eda, wakataka kurudiana nikamzuia; ndipo ikashuka Aya hii.”