read

Aya 233: Mama Wanyonyeshe

Maana

Na wazazi wa kike wawanyonyeshe watoto wao.

Wafasiri wamehitilafiana katika makusudio ya tamko la wazazi wa kike. Je, ni waliopewa talaka tu, au ni walio kwa waume zao tu, au wote pamoja? Wengi wanasema kwamba tamko hilo linawakusanya wote kwa kuangalia kidhahiri; wala hakuna dalili ya kuhusisha upande mmoja tu. Na sisi tunaelekea upande huu. Kwa sababu kunyonyesha kunamtegemea mama kwa hali yoyote awayo, sio kwa kuwa na mume wala kwa kuwa ni mtalikiwa.

Wawanyonyeshe watoto wao ni amri ya mapendekezo tu, sio lazima; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "...Na kama mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee (mwanamke) mwingine." (65:6) Maana yake ni kuwa akina mama wanayo haki ya kuwanyonyesha wato- to wao kuliko watu wengine.

Unaweza kuuliza kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na ni juu ya baba chakula chao na nguo zao" inatilia nguvu kuwa makusudio ya Wazazi watakao nyonyesha ni wanawake walioolewa au walio katika talaka rejea tu; na wala sio walioachwa ambao imekwisha eda yao. Kwa sababu mtalikiwa, chake ni malipo ya kunyonyesha tu sio chakula; kwa hiyo Aya haiwahusishi waliopewa talaka.

Jibu: Hapana kizuizi kwa tamko moja kuenea kihukumu kwa upande mmoja na kuhusika upande mwingine pamoja na kupatikana dalili. Iko hadithi na wamekongamana wanavyuoni kuwa mwenye kupewa talaka hana posho isipokuwa malipo ya kunyonyesha; kwa hiyo hakuna dalili iliyohusisha upande fulani, basi tunafuata kuenea kwa wote.(aliye katika ndoa na mtalikiwa)

Miaka Miwili Kamili.

Hapa kuna maswali mawili: Kwanza: Je, inafaa mama kunyonyesha mtoto zaidi ya miaka miwili?

Jibu: Ndio, hasa ikiwa mtoto anahitajia ziada. Kuwekwa kiwango cha miaka miwili kuna faida tatu:

1. Mama asidai malipo zaidi ya miaka miwili.

2. Ukitokea mzozano kati ya baba na mama kuhusu muda wa kunyonyesha mtoto, basi hukumu itakuwa ya Mwenyezi Mungu: 'Miaka miwili kamili.'

3. Kunyonyeshwa mtoto baada ya miaka miwili na mtu kando hakuwezi kusababisha uharamu kati ya mnyonyeshaji na mtoto: Hivyo ndivyo walivyosema Shia na Shafii. Ama Abu Hanifa yeye amesema hiyo ni mpaka baada ya miezi thelathini.

Swali la pili: Je, inafaa kupunguza muda wa miaka miwili?

Jibu: Inafaa kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha.

Na pia kauli yake: Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kur-idhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao

Je, tutarudia sharia katika kiwango cha chini cha muda wa kunyonyesha, au tutaangalia hali ya afya ya mtoto?

Mafaqihi wengi wamesema uchache wa muda wa kunyonyesha ni miezi 21 kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ۚ {15}

"... Na kubeba mimba kwake na kumwachisha ziwa ni miezi thelathini..." (46:15)

Tukitoa miezi tisa ambayo aghlabu inakuwa ya mimba, inabakia miezi ishirini na moja.

Kwa vyovyote ilivyo, umuhimu ni kuchunga afya ya mtoto na maslahi yake ambayo yanatofautiana kwa kutofautiana miili. Na utafiti huu ulikuwa na umuhimu hapo zamani ambapo hakukuwa na lishe ya kutosha. Ama hivi leo ambapo lishe zimejaa tele, suala hili halina maudhui tena.

Na ni juu ya aliyezaliwa mtoto huyo (baba) chakula chao na nguo zao kulingana na desturi.

Kwa dhahiri ulazima wa kulea uliotajwa hapa ni kwa mke na aliye katika eda ya talaka rejea. Kimetajwa chakula na mavazi kwa sababu ya umuhimu wake.

Makusudio ya desturi ni kuangalia hali ya matumizi ya mke katika jamii yake. Ama kuangalia hali ya mume kimali, Mwenyezi Mungu anasema:

Haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa uweza wake.

Tafsir wazi ya jumla hii tunaweza kuipata katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mwenye uwezo atoe kadiri ya uwezo wake; na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yoyote ila kwa kadiri ya alichompa..."(65:7)

Imam Jaffar Sadiq (a.s.) alikuwa na marafiki wengi, mara nyingine walikuwa wakichelewa kuondoka nyumbani kwake mpaka unafika wakati wa chakula, basi huwaletea chakula; mara huwaletea mkate na siki na mara nyingine huwaletea chakula kizuri kabisa. Mmoja akamuuliza sababu ya kufanya hivyo. Imam akamjibu: "Tukiwa na nafasi tunawapa cha nafasi na tukiwa na dhiki tunawapa cha dhiki."

Mzazi (Mama) asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala mwenye kuzaliwa mtoto (baba) kwa ajili ya mwanawe.
Inapasa kuangalia vizuri Aya hii, kwa sababu makadhi hivi sasa wanatoa ushahidi sana kwa Aya hii katika hukumu zao na kuifasiri kuwa baba asimdhuru mama kwa sababu ya mtoto. Ama watu wa tafsiri wanakurubia kuafikiana kwa pamoja kwamba maana yake ni kinyume na hivyo; kwamba mama asikatae kumnyonyesha mtoto wake na kumdhuru kwa kutaka kumkasirisha baba yake kwa hilo.

Mwenye Majmaul Bayan anasema: "Mama asiache kumnyonyesha mtoto wake kwa ajili ya kumuudhi baba yake." Sasa haya yako wapi na ushahidi wa makadhi kwamba baba asimdhuru mama kwa sababu ya mtoto?

Na sisi tunasema, baada ya kuitia akilini Aya bila ya kutegemea zaidi maneno ya mafaqihi na wafasiri, kwamba mara nyingi kunapotokea kutengana kati ya mtu na mkewe, humfanya mtoto ndio chombo cha kukasirishana, na matokeo yake mtoto hudhurika kwa kumfanya mtoto ndio kafara la ugomvi wao.

Mfano mama anaweza kukataa kumnyonyesha mtoto, hata kama iko haja, ili amuudhi baba. Au baba anaweza kumnyang'anya mama mtoto na kumpatia mtu mwingine amnyonyeshe, hata kama mamake anataka kumnyonyesha.

Mwenyezi Mungu amekataza kudhuriana kwa namna yoyote ile, iwe kwa mtoto, baba au mama kwa sababu ya mtoto. Haya ndiyo yanayokuja haraka kwenye fahamu katika kauli yake Mwenyezi Mungu. Wala hayapingani na kauli ya wafasiri, isipokuwa yanayopingana ni kutolea ushahidi makadhi; ingawaje kauli yao yenyewe ni sahihi, lakini makosa yako katika kutolea ushahidi.

Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo .

Wamehitalifiana kuhusu makusudio ya mrithi, je ni mrithi wa baba au mrithi wa mtoto?

Mfumo wa maneno unatilia nguvu kwamba ni mrithi wa mwenye mtoto (baba), lakini maana hayasimami sawa. Kwa sababu mtoto na mama ni katika jumla ya warithi wa baba na kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu mfano wa hivyo inaonyesha ni wajibu kwa mrithi wa baba kutoa posho ile iliyo wajibu kwa baba.

Kwa hivyo inamaanisha posho ya mama ni wajibu kwa mama, kwa mtoto wake na kwa warithi wengine wakiwepo. Inavyojulikana ni kuwa posho ya mama si wajibu kwa yeyote ikiwa huyo mama anauwezo; ni sawa uwezo huo uwe umetokana na kumrithi mume, au la. Kwa hivyo basi hakuna maana kusema kuwa ni wajibu kujilisha kutokana na mali yake.

Kama tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa mtoto, basi itakuwa tunahitalifiana na dhahiri kwa upande mmoja; pia tutakuwa tunahitilifiana na hali ilivyo kwa upande mwingine. Kwa sababu posho ya mama si wajibu kwa anaye mrithi mtoto. Ni kweli kuwa Mama anaweza kuchukua ujira wa kunyonyesha kutoka katika mali ya mtoto wake (anaye mnyonyesha), ikiwa anayo mali, lakini ujira wa kunyonyesha ni kitu kingine na posho ni kitu kingine kwa maana yake sahihi.

Ilivyo hasa ni kwamba Aya hii ni miongoni mwa Aya za mifano zenye kutatiza ndio maana Malik akasema kuwa ni Mansukh (iliyoachwa hukumu yake) kama alivyonakili Abu bakr Al-maliki katika kitabu cha Ahakamul Qur'an. Baadhi ya wafasiri wameiruka na wengine wameinakilia kauli zisizo kuwa na nguvu.

Kutatiza kwake kama tulivyobainisha ni ikiwa itabaki dhahiri ilivyo, maana hayatasimama sawa; yaani tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa baba na kufasiri mfano wa hivyo kwa maana ya posho ya mama. Na kama tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa mtoto na mfano wa hivyo kwa maana ya malipo ya kunyonyesha, maana yatakuwa sawa lakini tutakuwa tunahitalifiana na dhahiri ya matamko mawili (mrithi na mfano wa hivyo).

Lakini hakuna njia nyingine zaidi ya kuhitalifiana na dhahiri ya tamko na kulifasiri kimaana (taawili). Sio mbali kuwa Hadith zenye kupokewa katika kunyonyesha na malipo yake, ni mfano wa dalili ya kuswihi taawili hii.
Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha (kunyonya) kwa kuridhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao.

Yaani baba na mama kwa kushauriana wanaweza kumwachisha mtoto kabla ya miaka miwili au baada yake kwa maslahi ya mtoto; bali inajuzu kwa baba kumpa mnyonyeshaji mwingine; Mwenyezi Mungu amelionyesha hilo kwa kusema:

Na kama mkitaka kuwapatia watoto wenu Mama (wengine) wa kuwany- onyesha, basi haitakuwa vibaya juu yenu kama mkitoa mlichowaahidi kwa desturi.

Msemo 'mkitoa mlichowaahidi,' unaelekezwa kwa akina baba. Maana yake ni enyi akina baba! Hakika mama ana haki zaidi ya kumyonyesha mwanawe kuliko mtu wa kando; naye mama anastahiki malipo ya kawaida. Ikiwa mumempa haki hii na mkamdhamiria kumpa malipo ya kunyonyesha ya kawaida, lakini akataka zaidi, basi si vibaya hapo kuwapatia watoto wenu wanyonyeshaji wengine. Imesemwa kuwa maana yake ni mkiwapatia wanyonyeshaji wa nje malipo ya kawaida si vibaya kwenu.

Vyovyote iwavyo, ni juu ya baba kumpatia haki (malipo) yake kila mmoja, awe mama au mama wa kunyonyesha tu.

وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنْكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنْفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِي أَنْفُسِهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ {234}

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake (hao wake) wangoje miezi minne na siku kumi. Na wanapofikilia muda wao, basi si vibaya kwenu kwa yale wanayojifanyia, yanayoafiki ada. Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُمْ بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ أَوْ أَكْنَنْتُمْ فِي أَنْفُسِكُمْ ۚ عَلِمَ اللَّهُ أَنَّكُمْ سَتَذْكُرُونَهُنَّ وَلَٰكِنْ لَا تُوَاعِدُوهُنَّ سِرًّا إِلَّا أَنْ تَقُولُوا قَوْلًا مَعْرُوفًا ۚ وَلَا تَعْزِمُوا عُقْدَةَ النِّكَاحِ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْكِتَابُ أَجَلَهُ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي أَنْفُسِكُمْ فَاحْذَرُوهُ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ {235}

Wala si vibaya kwenu kuonyesha ishara ya kuwaposa wanawake, au kutia azma katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msifanye nao ahadi kwa siri; isipokuwa mseme maneno yaliyoruhusiwa na sharia. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda uliofaradhiwa ufike. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo katika nafsi zenu, basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, mpole.