read

Aya 234-235: Eda Ya Kufiwa

Maana

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake; wangoje miezi minne na siku kumi.

Mafaqihi wote wameafikiana kwamba eda ya mwenye kufiwa na mume ni miezi minne na siku kumi. Awe mkubwa au mdogo; mwenye kutoka hedhi au aliyekoma, mwenye kuingiliwa au la. wamelitolea dalili hilo kwa Aya hii.

Ama akiwa na mimba, madhehebu manne ya kisunni yamesema: Eda yake itakwisha kwa kuzaa; hata kama ni muda mchache tu, baada ya kufa mumewe, kiasi ambacho anaweza kuolewa hata kabla ya kuzikwa mumewe, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "... Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa..." (65:4)

Mafaqihi wa Kishia wamesema: Eda yake ni ule muda utakaorefuka zaidi; yaani ikipita miezi minne na siku kumi kabla ya kuzaa atangojea mpaka azae; au akizaa kabla ya kupita miezi minne na siku kumi, atakaa eda ya miezi minne na siku kumi. Wametoa dalili juu ya hilo kwa ulazima wa kukusanya Aya mbili; "Wangoje miezi minne na siku kumi" na "Eda yao ni mpaka watakapozaa."
Aya ya kwanza imejaalia eda kuwa ni miezi minne na siku kumi, nayo inakusanya mwenye mimba na asiye na mimba; na Aya ya pili imeifanya eda ya mwenye mimba ni kuzaa, nayo inakusanya mwenye kuachwa na mwenye kufiwa na mumewe.

Kwa hivyo kutakuwa na mgongano kati ya dhahiri ya Aya mbili kwa mwanamke mwenye mimba ambaye atazaa kabla ya miezi minne na siku kumi: Kwa mujibu wa Aya ya pili itakuwa eda imekwisha na kwa mujibu wa Aya ya kwanza itakuwa bado haijaisha kwa sababu miezi minne na siku kumi haikutimia.

Vile vile utapatikana mgongano ikipita miezi minne na siku kumi, akiwa bado hajazaa; kwa mujibu wa Aya ya kwanza eda itakuwa imekwisha kwa sababu muda wa miezi minne na siku kumi umekwisha; na kwa mujibu wa Aya ya pili itakuwa eda bado haijaisha kwa sababu hajazaa. Na maneno ya Qur'an ni mamoja ni lazima yaafikiane.

Kwa hivyo tukiziunganisha Aya mbili na kuzikusanya katika jumla moja, zikawa hivi; "Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake; wangoje miezi minne na siku kumi. Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa."

Tukizikusanya hivi, maana yake yatakuwa ni: Eda ya mwenye kufiwa na mumewe ni miezi minne na siku kumi, kwa asiyekuwa na mimba; na mwenye mimba ambaye atazaa kabla ya kupita miezi minne na siku kumi. Na itakuwa eda ya mwenye kufiwa, mwenye mimba ambaye atazaa baada ya kupita miezi minne na siku kumi, ni kuzaa. Kama akiuliza mwulizaji: Vipi Shia wamefanya eda ya mwenye mimba, aliyefiwa na mume, ni muda utakaorefuka pamoja na kwamba Aya "Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa", iko wazi kwamba eda inaisha kwa kuzaa?

Shia naye anaweza kujibu kwa kusema: "Vipi madhehebu manne ya Sunni yakasema kuwa eda ya mjane mwenye mimba inaweza kuwa hata miaka miwili kama ikiendelea mimba pamoja na kuwa Aya "Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuwaacha wake, (nao wake) wakae wangoje miezi minne na siku kumi" iko wazi kwamba eda ni miezi minne na siku kumi?"

Kwa hiyo hakuna jengine lolote la kuchukulia Aya mbili isipokuwa kuchukulia kauli ya muda utakaorefuka zaidi.

Na wanapofikia muda wao, basi si vibaya kwenu kwa yale wanayoji- fanyia, yanayoafiki ada Mwenyezi Mungu anazo habari mnayoyatenda.

Yaani kama ukisha muda wa eda ya mjane, basi hapana dhambi kwenu enyi Waislamu kwa mwanamke kufanya yale aliyozuiliwa wakati wa eda; kama kujipamba na kuonekana, na wanaotaka kuwaoa kwa njia ile iliyo maarufu kisheria. Hapa Mwenyezi Mungu anawaambia Waislamu wanaume, kwa sababu ni juu yao kuwazuia wanawake wanapopetuka mipaka ya kisheria. Wameafikiana mafaqihi kwa kauli moja kuwa mjane aliyefiwa na mume wakati wa eda ni wajibu kwake kujiepusha na kila linalomfanya kuonekana mrembo wa kutamanika.

Wala si vibaya kwenu kuonyesha ishara ya kuwaposa wanawake.

Mwenyezi Mungu ameharamisha ndoa katikati ya eda ya namna yoyote, bali ni haramu pia kwa mwanamume kumposa mwanamke akiwa katika eda yake, iwe ni eda ya kufiwa na mume au ya talaka bain, lakini Mwenyezi Mungu anahalalisha kufanya ishara ya posa bila ya kudhihirisha, katika isiyokuwa eda ya talaka rejea. Kwani mtalaka katika eda hiyo bado yuko mikononi mwa mumewe.

Au kutia azma katika nyoyo zenu.

Kila linalopita akilini na kuazimiwa na moyo halina ubaya kwa Mungu, kwa sababu liko nje ya uwezo wa mtu; lililo kwenye uwezo wa mtu ni zile athari. Kwa hivyo mtu akiazimia kuoa mke aliye edani, sio dhambi. Lakini akiidhihirisha azma yake hii akamposa, basi atakuwa ni mwenye dhambi. Kwa sababu kuazimia kuko nje ya uwezo na kudhihirisha kuko ndani ya uwezo wa mtu. Iko Hadith inayosema: "Ukiwa na donge moyoni usilitekeleze."
Hapo amekataza kufanya, ambako ni athari ya hilo donge, lakini hakukataza kuwa na donge kwa sababu hakuzuiliki.

Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka.

Kwa hivyo ndio akawahalalishia kuonyesha ishara, lau angeliwazuia basi mngeliona mashaka.

Lakini msifanye nao ahadi kwa siri.

Hiyo ishara ya kuoa pia haifai kuionyesha kwa siri wakati wa eda katika faragha. Kwa sababu faragha kati ya mwanamume na mwanamke inaleta mambo asiyoyaridhia Mwenyezi Mungu. Iko Hadith inayosema:

"Hakai faragha mwanamume na mwanamke isipokuwa shetani huwa watatu wao." Hasa ikiwa mume anamtamani aliyekaa naye faragha, isipokuwa ikiwa mume ana yakini kwamba faragha haitaleta haramu katika maneno wala vitendo, hapo ndipo itajuzu kusema naye yale ambayo si mabaya, hata kusema kwa dhahiri. Ndio Mwenyezi Mungu akalegeza kidogo kwa kusema; "Isipokuwa mseme maneno yaliyoruhusiwa na sharia."

Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda uliofaradhiwa ufike.

Yaani msifunge ndoa ndani ya eda mpaka ishe.

Ndoa Katika Eda

Baada ya kuafikiana Waislamu wote kwamba kufunga ndoa na kuposa wazi wazi katikati ya eda, ni katika mambo ya haramu, na kwamba ndoa itakuwa batili baada ya kuafikiana hivi, wakahitalifiana juu ya uharamu wa waliofunga ndoa ndani ya eda. Je mwanamke atakuwa haramu milele au inawezekana kufunga ndoa tena baada ya kwisha eda? Hanafi na Shafi wamesema hakuna kizuizi cha kumwoa mara ya pili. Hayo yamo katika kitabu Bidayatul Mujtahid.

Shia wamesema: Akifunga naye ndoa na hali anajua kuwa yuko katika eda, basi atakuwa haramu kwake daima, iwe amemwingilia au hakumwingila. Na akifunga naye ndoa bila ya kujua kuwa yuko kwenye eda, basi hatakuwa haramu, isipokuwa kama amemwingilia, na anaweza kumwoa tena baada ya eda kama hakumwingilia. Hii ndio hukumu ya kufunga ndoa katikati ya eda. Ama kuposa hakuna athari yoyote isipokuwa dhambi tu.

Maajabu niliyoyasoma katika suala hili ni yale yaliyo katika kitabu Ahkamul Qur'an cha Abu Bakr Al Andalusi wa madhehebu ya Malik, pale aliposema: “Akimposa katikati ya eda, kisha akafunga naye ndoa baada ya eda, basi ni lazima amwache talaka moja, kisha aanze upya kumchumbia na kufunga ndoa.”

لَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِنْ طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ {236}

Si vibaya kwenu kama mkiwapa wake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari. Na wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo. Kiasi cha kuwaliwaza, cha kawaida. Ndio haki kwa wafanyao mema.

وَإِنْ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِنْ قَبْلِ أَنْ تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَنْ يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ ۚ وَأَنْ تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ وَلَا تَنْسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {237}

Na kama mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa na mmekwisha wakadiria mahari, basi ni nusu ya hayo mahari mliyokadiria. Isipokuwa (wanawake wenyewe) wasamehe au asamehe ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake, na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua. Wala msisahau fadhila baina yenu; hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyafanya.