read

Aya 236-237: Talaka Kabla Ya Kuingilia

Maana

Si vibaya kwenu kama mkiwapa wake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari

Yaani hamlazimiwi na mahari. Kwa ujumla maana yake ni kwamba mwenye kufunga ndoa na mwanamke wala asimtajie mahari katika ndoa, kisha akamwacha kabla ya kumwingila, basi hana ulazima wa kutoa mahari; isipokuwa mwanamke anastahiki kupewa kiasi cha kumliwaza tu.

Kiasi hicho ataangalia mume uwezo wake; kwa mfano tajiri anaweza kutoa mkufu wa thamani ya shs.1000, mtu wa kawaida akitoa bangili ya Shs. 500 na masikini akatoa nguo ya Shs. 20. Katika haya Mwenyezi Mungu anasema:

Na wapeni cha kuwaliwaza mwenye wasaa kadiri awezavyo, na mwenye dhiki kadiri awezavyo. Kiasi cha kuwaliwaza, cha kawaida. Ndio Haki kwa wafanyao mema.

Wale ambao wanazifanyia wema nafsi zao kwa kumtii Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Na kama mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa na mmekwisha wakadiria mahari, basi ni nusu ya hayo mahari mliyokadiria.

Ikiwa amefunga ndoa akataja mahari kisha akamwacha kabla ya kumwingilia, basi anastahiki nusu ya mahari.

Isipokuwa (wanawake wenyewe) wasamehe.

Yaani haifai kumzuilia mwanamke nusu ya mahari au kitu chochote, isipokuwa kama akisamehe mwenyewe kwa radhi yake.

Au asamehe ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake.

Mume ndiye ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake. Makusudio ni kwamba mwenye kupewa talaka kabla ya kuingiliwa hastahiki zaidi ya nusu ya mahari yaliyotajwa isipokuwa kama mume atampa yote au kumpa zaidi ya nusu.

Na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua.

Msemo unaelekezwa kwa wote, mume na mke, kuwahimiza kusameheana.

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّهِ قَانِتِينَ {238}

Angalieni sana swala, na ile swala ya katikati. Na simameni kwa unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

فَإِنْ خِفْتُمْ فَرِجَالًا أَوْ رُكْبَانًا ۖ فَإِذَا أَمِنْتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّهَ كَمَا عَلَّمَكُمْ مَا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ {239}

Na kama mkiwa na hofu, basi ni hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale mliyokuwa hamyajui.