read

Aya 238-239: Swala Ya Katikati

Angalieni sana Swala na ile Swala ya katikati

Kuziangalia sana ni kuzitekeleza kwa nyakati zake na njia zake. Mwenyezi Mungu ameihusisha hii kwa kuipa uzito na umuhimu; kama umuhimu wa Jibril na Mikail katika Malaika alipowahusu wao, baada ya kuwakusanya na Malaika wengine katika kauli yake: Ambaye ni adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na Mikail..." (2:98)

Wamehitalifiana kuhusu swala ya katikati, mpaka kufikia kauli kumi na nane; kama ilivyonakiliwa katika kitabu Naylul Awtwar. Kauli iliyo mashuhuri zaidi ni ile inayosema kuwa ni swala ya Alasiri, na kuna riwaya katika hilo. Imesemwa kwamba imeitwa swala ya katikati kwa sababu iko baina ya swala mbili za (Maghribi na Isha) na swala mbili (Asubuhi na Adhuhuri). Ama sababu ya kutajwa kwake ni kwamba inakuwa wakati ambao aghlab watu wanashughulika.

Mwenye tafsir ya Al Manar amenakili kutoka kwa Ustadh wake, Sheikh Muhammad Abduh, kwamba yeye amesema: Lau si kuwako kongamano juu ya tafsiri ya Wusta kuwa ni moja ya swala tano na wala sio tano zote, basi yeye angeliifasiri kwa swala bora; na Mwenyezi Mungu amehimiza na kutilia mkazo swala bora nayo ni ile ambayo moyo unakuwapo ndani ya hiyo swala, nafsi kuwa na mwelekeo wa kuwa na ikhlas kwa Mwenyezi Mungu na kuzingatia maneno Yake. Sio swala ya kujionyesha au ya mwili tu, lakini moyo haupo.

Haya ndiyo maelezo mazuri zaidi niliyosoma katika tafsiri ya Aya hii, nayo yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ {1}

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ {2}

Wamefuzu waumini ambao katika swala zao huwa ni wanyenyekevu."(23:1-2)

Na simameni kwa unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Yaani mumuombe Mwenyezi Mungu katika swala zenu kwa unyenyekevu wa kuhisi ukubwa na utukufu wake, hali ya kuachana na mambo yanayoushughulisha moyo.

Na kama mkiwa na hofu basi ni hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda.

Swala haisamehewi kwa hali yoyote ile. Mtu akiwa anashindwa kufanya baadhi ya vitendo vyake, basi atatekeleza vile atakavyoweza. Akishindwa kufanya vitendo vyote, basi ataswali kwa kutamka na kuashiria. Ikiwa hivyo pia atashindwa, basi ataleta picha ya swala moyoni.

Hapa anaashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba mtu anaweza kufiki- wa na wakati wa Swala naye yuko vitani akiwa amekabiliana na adui, n.k. basi ataswali kadiri atakavyoweza, kwa kwenda au akiwa amepanda kitu; kwa kuelekea Qibla au bila ya kuelekea.

Mwenye Majmaul Bayan anasema: “Swala ya kuhofia adui ni rakaa mbili iwe ni safirini au nyumbani, isipokuwa Maghrib tu, hiyo ni rakaa tatu.

Imepokewa Hadith kwamba Imam Ali (a.s.) katika usiku wa vita vya Harir aliswali kwa kuashiria na ikasemwa ni kwa takbir, na kwamba Mtume (s.a.w.w.) siku ya vita vya Ahzab aliswali kwa kuashiria.

Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale mliyokuwa hamyajui.

Yaani hofu ikiondoka basi swalini swala ya kawaida ile mliyofundishwa mwanzo.

Kuacha Swala Kunapelekea Ukafiri

Tumezungumzia swala katika kufasiri Aya iliyotangulia na sasa tunaunganisha kifungu hicho na haya yafuatayo: Majaribio yamethibitisha kwamba kuacha swala mara nyingi kunapeleka ukafiri na athari zake. Hiyo ni kwamba kafiri hajali kufanya haramu, basi hivyo hivyo mwenye kuacha swala anafanya mambo ya haramu bila ya kujali. Popote penye ukafiri pana uovu na uchafu. Hali hiyo inaletwa na kuacha swala.
Dalili kubwa zaidi inayoonyesha hakika hii ni ufisadi katika zama zetu hizi. Haya mabaa, madanguro na ma casino katika miji yetu. Na pia huku kutembea nusu-uchi kwa mabinti zenu na tabia mbaya za watoto wetu (kuiga wazungu), yote hayo ni natija ya kuacha swala; kwa dalili ya kuwa haya yote hayakuwako wakati wa swala ilipokuwa imezoeleka kwa watoto wetu wa kiume na wa kike.

Hiyo ndiyo tafsir ya Hadith tukufu inayosema: "Tofauti kati yetu sisi na nyinyi (makafiri) ni swala; mwenye kuiacha amekufuru."

Haitamtosha mtu kusema: Mimi ni Mwislamu au kutamka shahada mbili (kushahadia) tu, maadamu amali zake ni za kikafiri na kilahidi.

Hakika mlahidi haoni haya wala kigegezi chochote kuacha swala, na hafichi hilo, bali hutangaza hasa, kwa sababu hafuati dini. Basi hivyo hivyo vijana wetu wa kileo wanaona fahari kujulikana kuwa hawaswali, bali wanamdharau mwenye kuswali na swala yenyewe. Kwa hivyo hakuna tofauti kati yao na walahidi.

Si vibaya kama tukinukuu mawaidha mazuri kutoka katika kitabu Al-Islam Khawatir wa Sawanih cha Mfaransa, Comte Henry Descarte kilichofasiriwa kwa Kiarabu anasema:

"Nilisafiri katika jangwa la jimbo la Hawaran nikiwa na wapanda farasi thelathini, wote wakinihudumia mimi. Wakati tukiendelea na msafara, mara sauti ikanadi kwamba wakati wa swala ya Alasiri umefika. Wapanda farasi wote wakashuka haraka; mara wakajipanga safu za swala ya jamaa, nikawa ninawasikia wakilikariri neno Allahu Akbar kwa sauti ya juu.

Likawa jina hilo la Mungu linaniingia akilini zaidi kuliko nilivyoingiwa akilini na somo la elimu ya Mungu. Nikahisi kukosa raha kuliko sababishwa na haya na kuhisi kwamba hao wapanda farasi ambao walikuwa wakinitukuza muda mchache uliopita, hivi sasa wakiwa katika swala yao, wanahisi kwamba wako katika makao ya juu zaidi na wenye nafsi tukufu zaidi kuliko mimi. Lau ningeitii nafsi yangu ningeliwapigia kelele kwa kusema: Mimi pia ninamkubali Mungu na ninajua Swala.

Ni uzuri ulioje wa mandhari ya watu hao katika swala yao na huku farasi wao wako pembeni mwao wakiwa wametulia kimya kamba zao zikiwa chini, kama kwamba wao nao wanainyenyekea swala; farasi aliyekuwa akipendwa na Mtume kwa mapenzi ambayo yalimpelekea Mtume kuifuta pua yake kwa shuka yake.

Nilisimama pembeni nikiwaangalia wanaoswali na kujikuta mimi niko pweke kabisa nikionyesha alama ya kukosa imani, kana kwamba mimi ni mbwa tu, aliye mbele ya wale wanaomkariria Swala Mola wao kwa unyenyekevu unaotoka katika nyoyo zilizojaa ukweli na imani.

وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنْكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا وَصِيَّةً لِأَزْوَاجِهِمْ مَتَاعًا إِلَى الْحَوْلِ غَيْرَ إِخْرَاجٍ ۚ فَإِنْ خَرَجْنَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِي مَا فَعَلْنَ فِي أَنْفُسِهِنَّ مِنْ مَعْرُوفٍ ۗ وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {240}

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na wakaacha wake, wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi ya mwaka mmoja bila ya kutolewa. Wakiondoka, basi si vibaya kwenu kwa yale waliyojifanyia wenyewe, yanayofuata desturi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ {241}

Na wanawake waliopewa talaka wapewe cha kuwaliwaza kulingana na desturi; hiyo ni haki kwa wenye takua.

كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {242}

Namna hiyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya Zake ili mpate kufahamu.