read

Aya 240-242: Na Wale Wanaokufa

Maana

Ilikuwa ni ada ya Waarabu kabla ya Uislamu kwamba mtu akifa, mkewe hapati urithi wowote isipokuwa posho yake ya mwaka mmoja tu; kwa sharti akae eda katika nyumba ya mumewe. Akitoka kabla ya mwaka, basi hana posho. Aya hii ni uthibitisho wa hayo, na yalikuwapo katika mwanzo wa Uislamu.

Wafasiri na mafaqihi wote wameafikiana kwa kauli moja kwamba Aya hii ni Mansukh hukumu yake (haitumiki tena) na imenasikhwa na Aya mbili:

1. "Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake, wangoje miezi minne na siku kumi..."(2:234)

2. "...Nao (wake zenu) watapata robo ya mlivyoacha, ikiwa hamna mtoto, lakini ikiwa mnaye mtoto basi wao (wanawake) watapata thumuni..." (4:12)

Kwa maana kuwa atajilisha mwenyewe kutokana na fungu lake. Pamoja na kwamba Aya hii haitumiki kabisa hukumu yake katika sharia, lakini tutaifasiri kama walivyofanya wafasiri.

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na wakaacha wake, wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi ya mwaka mmoja.

Ilikuwa kabla ya kutotumika Aya hii ni wajibu kwa wale ambao wanadhihirikiwa na alama za mauti kuusia kwa ajili ya wake zao wazuiliwe majumbani kwa kupewa posho.

Bila ya kutolewa.

Yaani posho itakuwa wajibu kama wakitaka kukaa katika nyumba ya bwana aliyefariki. Ama wakitoka, basi si wajibu. Kwa hivyo ndio akaashiria Mwenyezi Mungu kwa kusema:

Wakiondoka basi si vibaya kwenu.

Yaani hamna jukumu kuwapa posho. Kwa maneno mengine posho ni wajibu kwa kubaki nyumbani, wakitoka hakuna posho.

Kwa yale waliyojifanyia wenyewe, yanayofuata desturi.

Mwanamke akitoka nyumbani kwa mumewe aliyefariki, anaweza kujipamba na kuposwa katika mipaka ya sharia; yaani mwanamke aliyefiwa na mumewe ana hiyari kubaki nyumbani kwa mume kwa muda wa mwaka mmoja na kupewa posho au kutoka asipewe posho.

Na wanawake waliopewa talaka wapewe cha kuwaliwaza kulingana na desturi; hiyo ni haki kwa wenye takua.

Kutoa ni lazima kuangalia hali ya mtoaji; kama ilivyokwishaelezwa katika Aya ya 236. Tamko la wenye kupewa talaka linawakusanya watalikiwa wote ambao wanagawanyika sehemu nne.

1. Mwenye kupewa talaka akiwa amekwishaingiliwa na amekwisha bainishiwa mahari, huyu atapata mahari yote, kama ilivyobainishwa katika Aya ya 229.

2. Mwenye kupewa talaka bila ya kuingiliwa na amekwisha bainishwa mahari; yeye atapata nusu ya mahari; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 237.

3. Mwenye kupewa talaka akiwa ameingiliwa, lakini hakubainishiwa mahari; yeye atapata mahari kiasi cha makisio ya desturi yao. Hilo wameafikiana Waislamu wote.

4. Mwenye kupewa talaka, bila ya kuingiliwa na bila ya kubainishiwa mahari. Huyu hana mahari, isipokuwa atapewa cha kumliwaza tu; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 236.

Kwa ufupi ni kwamba cha kuliwaza hupewa yule mwenye kupewa talaka bila ya kuingiliwa na bila ya kubainishiwa mahari wakati wa ndoa. Ama wengine hakuna ulazima wa kuwapa bali ataachiwa mwenyewe aliyetoa talaka akitaka atampatia cha kuliwaza, asipotaka ni basi imesemwa kuwa ni sunna kumpatia.

Namna hiyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kufahamu.

Yaani mpate kujua. Kwa sababu ambaye haonyeki na kuacha kutumia hukumu za Mwenyezi Mungu, basi yuko katika daraja ya wasiokuwa na akili.

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ خَرَجُوا مِنْ دِيَارِهِمْ وَهُمْ أُلُوفٌ حَذَرَ الْمَوْتِ فَقَالَ لَهُمُ اللَّهُ مُوتُوا ثُمَّ أَحْيَاهُمْ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ {243}

Je, hukuwaona wale waliotoka majumbani mwao nao walikuwa maelfu wakiogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni; kisha akawafufua. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.

وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {244}

Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.