read

Aya 243-244: Kuogopa Mauti

Maana

Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu Aya hii, wengi wao wameonyesha kuwa ni kisa cha kihistoria na kuchafua kurasa katika kukielezea kisa hiki. Baadhi yao wamesema hivi:

Watu katika Waisrail waliamrishwa kupigana jihadi dhidi ya adui zao. Wakaogopa kupigana ili wasife, wakayakimbia majumba yao kwa kuogopa kufa. Mwenyezi Mungu akawaua ili kuwafahamisha kwamba hakuna kitu chochote kinachoweza kukinga mauti; kisha akawafufua ili wazingatie na wamalize umri wao uliobakia.

Ya kushangaza zaidi niliyoyasema katika tafsiri ya Aya hii ni kwamba mmoja wa wafasiri anasema: "Mauti ni namna mbili: Mauti ya mateso, nayo ni yale ya ambayo mtu huhuishwa baada ya kufa hapa hapa duniani. Na mauti ya ajali ambayo mtu atafufuliwa akhera."

Wengine wamesema walikimbia maradhi ya Tauni, lakini sio kwa kupigana jihadi. Muhyiddin bin Arabi ameifasiri Aya hii kwa tafsiri yake ya Kisufi kwa kusema: "Mwenyezi Mungu aliwaua kwa ujinga akawafufua kwa elimu na akili."

Sheikh Muhammad Abduh ameichukulia Aya hii ni tamthiliya ya mazinga- tio na maonyo na wala sio tukio la kweli, na kwamba lengo la ishara hii ni kubainisha desturi ya Mwenyezi Mungu katika umma mbali mbali, na kwamba umma ambao unapigana jihadi na kulinda haki yake, utakuwa na maisha mema; na umma ambao una woga na kusalimu amri kwenye dhulma, utaishi maisha ya udhalili.

Kwa hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu kufeni ina maana ishini kwa kutawaliwa na kukandamizwa kwa ajili ya woga wenu, kwa sababu mfano wa maisha kama hayo ni mauti sio uhai. Na kauli yake akawahuyisha; ina maana aliwahuyisha kwa maisha ya uhuru na utukufu kwa sababu ya jihadi yao na kupigania haki yao.

Huu ni muhtasar mfupi sana wa rai ya Sheikh Muhammad Abduh ambayo ameifafanua kwa urefu sana. Na rai hiyo, kama unavyoiona, ni ya kimwamko lakini haitokani na dalili ya tamko la Aya.
Rai yake yenyewe ni sahihi bila ya shaka lakini iko mbali na dalili ya tamko. Huenda ikadhaniwa kwamba ni ya karibu kuliko zile kauli nyingine za wafasiri kwa upande huu.

Kwa sababu kauli zao zinategemea riwaya za Kiisrail na ngano tu. Na kauli ya Sheikh ina lengo la kuhamasisha, kupinga dhulma na kujitoa mhanga kwa ajili ya uhuru na heshima ya mtu, jambo ambalo lina mwelekeo.

Vyovyote iwavyo Aya hii inawezekana kuwa na maana mbali mbali, ndio maana kauli zikawa nyingi; wala hakuna kitu katika tamko la Aya kinachofahamisha kuswihi kauli kwa dhati.

Hata hivyo, kauli ya Sheikh Abduh ndio yenye nguvu zaidi ya kauli zote kwa kuangalia mwelekeo, kama tulivyokwisha eleza. Pia inasaidiwa na mpangilio wa maneno, pale alipofuatishia Mwenyezi Mungu moja kwa moja na Aya inayosema: "Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni msikizi, mjuzi."

مَنْ ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ أَضْعَافًا كَثِيرَةً ۚ وَاللَّهُ يَقْبِضُ وَيَبْسُطُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ {245}

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, ili amzidishie ziada nyingi? Mwenyezi Mungu ndiye anayezuia na hukunja na hukunjua na kwake mtarejezwa.