read

Aya 245: Ni Nani Atakayemkopesha Mwenyezi Mungu

Maana

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kupigania haki katika Aya iliyotangulia, katika Aya hii anahimiza kutoa mali ya kuwaandaa wapiganaji. Kwa sababu vita, kama vile vinavyohitajia watu, pia vinahitajia mali.

Mwenye kusoma bajeti ya vita, ya madola makubwa hivi sasa, hana budi kupotewa na tarakimu. Baadhi ya Dola za kimagharibi zimefikia zaidi ya elfu mia nne milioni. Lakini bajeti yote hii inahusika na kufanya uadui, kutaka ukubwa kutawala kimabavu, kuwakandamiza watu na kuwatawala katika mambo yao yote. Ama jihadi aliyoihimiza Mwenyezi Mungu katika kitabu chake ni jihadi kwa ajili ya kupigania haki na kujikinga na maadui.

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri.

Ilivyo hii ni amri ya kujitolea. Imekuja kwa njia ya swali ili kuilainisha mioyo ya waumini, waweze kuona wepesi kujitolea kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Na kauli yake Mwenyezi Mungu mkopo mzuri ni kuonyesha kuwa mali itakayotolewa ni lazima iwe ya halali sio ya haram na kujitolea kwa radhi na kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Atimize sharti hizo, ili Mwenyezi Mungu amzidishie ziada nyingi.

Imam Jaffar Sadiq (as) anasema: Iliposhuka Aya hii:

مَنْ جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِنْهَا ۖ {84}

“Atakayefanya wema atapata jaza bora kuliko huo ...” (28:84).

Mtume alisema:“Ewe Mola wangu nizidishie”,Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii: “Atakayefanya wema, atalipwa mfano wake mara kumi ...” (6:160) Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akasema: “Ewe Mola wangu nizidishie” basi Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii “IliMwenyezi Mungu amzidishie ziada nyingi.” Na wingi mbele ya Mwenyezi Mungu hauna idadi.

Na Mwenyezi Mungu hukunja na kukunjua.

Yaani hudhikisha na kufanya wasaa, kwa maana kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwahimiza waja wake kutoa kwa kuwa ana haja; hapana, Yeye ni mkwasi, na wao ni wahitaji. Lengo hasa ni kuwaongoza kwenye amali ya heri.

Na Kwake mtarejezwa.

Ili mwema alipwe kwa wema wake na mwovu kwa wovu wake.

أَلَمْ تَرَ إِلَى الْمَلَإِ مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ بَعْدِ مُوسَىٰ إِذْ قَالُوا لِنَبِيٍّ لَهُمُ ابْعَثْ لَنَا مَلِكًا نُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ۖ قَالَ هَلْ عَسَيْتُمْ إِنْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ أَلَّا تُقَاتِلُوا ۖ قَالُوا وَمَا لَنَا أَلَّا نُقَاتِلَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَقَدْ أُخْرِجْنَا مِنْ دِيَارِنَا وَأَبْنَائِنَا ۖ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ تَوَلَّوْا إِلَّا قَلِيلًا مِنْهُمْ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {246}

Je, Hukuona wakubwa wa wana wa Israil baada ya Musa walipomwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu. (Mtume wao) akasema: Je, haielekei kuwa hamtapigana mtakapoandikiwa kupigana? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa nje ya majumba yetu na watoto wetu? Walipoandikiwa kupigana, wakageuka isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ اللَّهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ۚ قَالُوا أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ الْمُلْكُ عَلَيْنَا وَنَحْنُ أَحَقُّ بِالْمُلْكِ مِنْهُ وَلَمْ يُؤْتَ سَعَةً مِنَ الْمَالِ ۚ قَالَ إِنَّ اللَّهَ اصْطَفَاهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُ بَسْطَةً فِي الْعِلْمِ وَالْجِسْمِ ۖ وَاللَّهُ يُؤْتِي مُلْكَهُ مَنْ يَشَاءُ ۚ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ {247}

Na Nabii wao akawaambia: Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu amemteua juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme Wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ آيَةَ مُلْكِهِ أَنْ يَأْتِيَكُمُ التَّابُوتُ فِيهِ سَكِينَةٌ مِنْ رَبِّكُمْ وَبَقِيَّةٌ مِمَّا تَرَكَ آلُ مُوسَىٰ وَآلُ هَارُونَ تَحْمِلُهُ الْمَلَائِكَةُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ مُؤْمِنِينَ {248}

Na Nabii wao akawaambia: Hakika alama ya ufalme wake ni kuwajia lile sanduku ambalo ndani mna kitulizo na mabaki ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na wa Harun, wakilibeba Malaika. Hakika katika hayo mna dalili kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.

فَلَمَّا فَصَلَ طَالُوتُ بِالْجُنُودِ قَالَ إِنَّ اللَّهَ مُبْتَلِيكُمْ بِنَهَرٍ فَمَنْ شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّي وَمَنْ لَمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُ مِنِّي إِلَّا مَنِ اغْتَرَفَ غُرْفَةً بِيَدِهِ ۚ فَشَرِبُوا مِنْهُ إِلَّا قَلِيلًا مِنْهُمْ ۚ فَلَمَّا جَاوَزَهُ هُوَ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ قَالُوا لَا طَاقَةَ لَنَا الْيَوْمَ بِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ ۚ قَالَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُمْ مُلَاقُو اللَّهِ كَمْ مِنْ فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ مَعَ الصَّابِرِينَ {249}

Basi Talut alipoondoka na jeshi, alisema: Mwenyezi Mungu atawafanyia mtihani kwa mto. Basi atakayekunywa humo si pamoja nami na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka fumba kwa mkono wake. Wakanywa humo isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi walipovuka, yeye na wale walioamini pamoja naye walisema: Leo hatumwezi Jalut, na Jeshi lake. Na wenye yakini ya kukutana na Mola wao walisema: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira.

وَلَمَّا بَرَزُوا لِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالُوا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانْصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ {250}

Na walipotoka kupambana na Jalut na jeshi lake walisema: Mola wetu, tumiminie subira na uisimamishe imara miguu yetu na utasai- die tuwashinde watu makafiri.

فَهَزَمُوهُمْ بِإِذْنِ اللَّهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللَّهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّهِ النَّاسَ بَعْضَهُمْ بِبَعْضٍ لَفَسَدَتِ الْأَرْضُ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْعَالَمِينَ {251}

Basi wakawashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu; na Daud akamuua Jalut, na Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima na akamfundisha aliyoyataka. Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwazuia watu, baadhi yao kwa wengine, ingeliharibika ardhi; lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya viumbe vyote.

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۚ وَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ {252}

Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu, tunakusomea kwa haki; na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.`