read

Aya 246-252: Kisa Cha Talut

Tumekwishaeleza katika tafsiri ya Aya ya 2 kwamba Qur'an ni kitabu cha mwongozo na dini, na ni kitabu cha kueleza tabia njema na sharia; sio kitabu cha visa na Historia au Filosofia na Sayansi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akielezea tukio la Kihistoria hulieleza kwa ajili ya mawaidha na kuwataka watu wazingatie; na wala haileti kisa chote kwa upambanuzi katika pande zake zote. Hilo limeelezewa katika Aya kadhaa; kama vile:

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ {111}

"Kwa hakika katika visa vyao, kuna fundisho kwa wenye akili ..." (12:111)

قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانْظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ {137}

"Zimepita desturi kabla yenu, basi tembeeni katika nchi na muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha." (3: 137)

Sheikh Muhammad Abduh anasema; "Kujaribu kuifanya Qur'an kuwa ni kitabu cha Historia ni kuhalifu desturi ya Qur'an na ni kuziepusha nyoyo na mawaidha yake, na pia ni kulipoteza lengo lake na hekima yake. Lililo wajibu kwetu ni kufahamu yaliyomo ndani yake na kuzitumia fikra zetu katika kutoa mafundisho, tujivue na yale yanayoitusi na kuikebehi Qur'an, na tujipambe na yale yanayoisifu Qur'an na kuiweka vizuri.

Mwenyezi Mungu amekidokeza kisa cha Talut katika Aya hizi (246-252), Nasi tutakitaja kama vile yanavyofahamisha matamko ya Aya hizi; kisha tutaidokeza sehemu za mafundisho na mawaidha.

Baada ya kufa Musa (a.s.) walikuwako makhalifa wake katika Manabii waliokuwa wakiendeleza amri za Mwenyezi Mungu katika Waisrail. Miongoni mwa makhalifa ni Mtume aliyeelezwa katika Qur'an bila ya kutajwa jina lake, isipokuwa alikuwa wakati wa Nabii Daud (a.s.), kama zinavyofahamisha Aya. Wafasiri wengi wanasema alikuwa akiitwa Samuel.

Siku moja kikundi cha Waisrail kilimwendea na kumwambia "Tuwekee mkuu wa jeshi ambaye tutafuata rai yake katika kupanga vita, na tupigane pamoja naye katika njia ya Mwenyezi Mungu,"

Mtume wao akawaambia - na alikuwa amekwisha watahini - "Mimi naona mtamwacha kama vita vikianza na mkiitwa kwenye jihad,"

Wakasema: "Tutamwachaje ikiwa adui ametutoa katika majumba yetu; na kutuweka mbali na watoto wetu?"

Basi Nabii wao akamtaka shauri Mwenyezi Mungu kwa yule atakayefaa kuongoza vita, Mwenyezi Mungu akampelekea wahyi kwa kusema kuwa "Mimi nimewachagulia wao Talut kuwa mfalme," Inasemekana - aliitwa Talut kwa sababu ya urefu wake; kutokana na neno la Kiarabu Tul (urefu).

Mtume alipowapa habari hiyo kwamba Mwenyezi Mungu amemchagua Talut walisema: "Atakuwaje mfalme wetu na wala hatokani na ukoo wowote mtukufu tena ni maskini?" Mtume akasema: "Kiongozi hahitaji ukoo isipokuwa awe na ushujaa na maarifa ya kuendesha mambo. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa Talut uwezo wa kielimu na kiumbo na nyenzo nyingine za kiongozi,"
Wakasema: "Basi tunataka alama itakayofahamisha uwezo wake huu."

Akasema:"Alama ni kurudishiwa kasha; litaletwa na Malaika kwa amri ya Mwenyezi Mungu,"

Inasemekana kasha hilo lilikuwa na mabaki ya mbao za Musa, fimbo yake, nguo zake na baadhi ya sehemu ya Taurat. Na walikuwa wamenyang'anywa na Wapalestina katika vita fulani. Pia imesemwa kwamba Mwenyezi Mungu aliliinua kulipeleka mbinguni baada ya kufa Musa. Lilipowajia kasha kutoka kwa Mwenyezi Mungu waliamini uon- gozi wa Talut.

Talut akawaongoza kwenda kupigana na adui yao; akawafahamisha kuwa watapitia kwenye mto ambako watatahiniwa kuangaliwa ikhlasi yao. Ambaye atakuwa na subira hatakunywa isipokuwa kiasi cha kitanga chake cha mkono. Atakayefuata ndiye msafi mwenye kutegemewa. Ama ambaye atakunywa mpaka amalize kiu, sio wa kutegemewa katika vita na jihadi. Walipopitia kwenye mto waliasi kama kawaida yao, wakanywa isipokuwa kikundi kidogo tu, kilithibiti kwenye ukweli na uaminifu.

Yalipokutana makundi mawili, Waisiralil wakiongozwa na Talut (Sauli) na Wapalestina wakiongozwa na Jalut (Goliat), Waisrail wengi waliogopa na kumwambia Talut; "Hatumuwezi Jalut na jeshi lake," Waumini wachache ambao hawakunywa maji wakasema: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu," Wakamwomba Mwenyezi Mungu awape subira uthabiti na ushindi. Mwenyezi Mungu akawatakabalia dua yao baada ya kujua nia yao, azma yao na ukweli katika nia. Daud akamuua Jalut na maadui wakahsindwa vibaya sana. Daud akawa maarufu mwenye kusikika sana baada ya kumuua Jalut.

Baada ya hapo Mwenyezi Mungu akampa Utume, akamtremshia Zabur na akamfundisha kutengeneza deraya na elimu ya dini na upambanuzi wa maneno; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima."

Huu ndio muhtasari wa zinavyofahamisha Aya tukufu. Ama Daud kumwoa binti ya Talut na kujaribu kufanya vitimbi vya kumuua kwa kumuoza binti yake, teo ya Daud na mawe yake, na kisa cha Daud na wanyama wakali mwituni, na mfano wa hayo yaliyomo katika vitabu vya Tafsir, vyote hivi ni visa ambavyo havina tegemeo lolote la mapokezi isipokuwa mapokezi ya Kiisrail.

Ama somo la kisa hiki ni anayefaa kuongoza ni yule mwenye uwezo wa kielimu na kiumbo na wala sio yule mwenye nasaba na fahari au mwenye jaha na mali; na kwamba ushindi utakuwa pamoja na subira na imani na wala sio kwa wingi wa watu; na njia ya kumjua mwema na mwovu ni kwa majaribio na mitihani.

Baada ya kuelezea muhtasari wa kisa na somo lake, sasa tunaingilia kufasiri jumla za maneno.

Maana

Je, hukuona wakubwa wa wana wa Israil baada ya Musa.

Kwa dhahiri msemo unaelekezwa kwa Mtume, na katika maana unaelekezwa kwa wasikilizaji wote; na tamko linaelekezwa kwa mwenye kukijua kisa na asiyekijua pia. Unaweza kumwambia mtu; "Je hujui fulani amefanya nini," wakati huo unataka kumfahamisha aliyoyafanya.

Walipomwambia Nabii wao; Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Inasemekana Nabii waliyemwambia hayo ni Samuel.

(Mtume wao) akasema; Je, haielekei kuwa hamtapigana mtakapo andikiwa kupigana!

Yaani; je mambo yako kama ninavyoona kuwa miongoni mwenu kuna watakaojitoa na kuacha kupigana kama mkifaradhiwa vita?
Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa nje ya majumba yetu na watoto wetu?

Walikanusha kuwa na chochote kitakacho wafanya waache jihadi; na wakabainisha sababu itakayowafanya wapigane ambayo ni kutolewa majumbani mwao na kutenganishwa na watoto wao.

Walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao.

Watu wengi wana sifa hii; wanathibitisha na wanaazimia kufanya mambo, lakini wakati ukifika wanajificha mvunguni. Ufasaha zaidi wa yaliyosemwa kuhusu mambo hayo ni kauli ya Bwana wa mashahidi Hussein bin Ali (a.s.); "Watu ni watumwa wa dunia na dini wameilamba kwa ndimi zao tu, inachukulika yanapokuwa mazuri maisha yao. Wapatwapo na misukosuko, wenye dini wanakuwa wachache.

Na Mtume wao akawaambia; Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali?

Mantiki hii haiwahusu Waisrail tu, bali watu wengi walikuwa na wanaendelea kuwa na mawazo kwamba cheo ni cha mwenye mali na jaha. Mwenyezi Mungu anasema: "Na wanapokuona hawakufanyi ila ni mzaha tu (wanasema); 'Ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa Mtume? "(25:41)

Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu amemteua juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili.

Yaani uongozi haui kwa sababu ya mali na nasaba, bali ni kwa elimu na ikhlasi. Makusudio ya ukunjufu wa kiwiliwili ni kutokuwa na maradhi, kwa sababu maradhi yanamzuwia kiongozi kutekeleza wajibu wake. Inasemekana kuwa Talut alikuwa mrefu zaidi kuliko mtu wa kawaida kwa kiasi cha dhiraa moja ya mkono.

Matakwa Ya Mwenyezi Mungu Na Kiongozi Mwovu

Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Mfalme wa wafalme, humpa ufalme amtakaye na humvua amtakaye; humtukuza amtakaye na humdhalilisha amtakaye; heri imo mikononi mwake na Yeye ni muweza juu ya kila kitu. Hapana shaka katika hilo; lakini, Yeye ambaye hekima yake imetukuka, ni Mwadilifu, hamdhulumu yeyote na hafanyi mambo kiholela. Vipi isiwe hivyo na hali Yeye amesema: “ Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.” (13:8)

Yaani kwa nidhamu na sababu, sio kwa sadfa au kiholela; hata mali ya haramu na utawala wa dhulma una sababu zake za kijamii. Unaweza kuuliza: Je utawala mwovu na utajiri wa unyanga'nyi unatege- mea matakwa ya Mwenyezi Mungu?

Jibu: Hapana, Mwenyezi Mungu ameharamisha dhulma na unyanga'nyi. Na Yeye hajiingizi katika mambo ya kijamii kwa njia ya Kun fayakun (kuwa ikawa). Mwenyezi Mungu hamzuwii kwa nguvu dhalimu kutokana na dhulma yake isipokuwa anamkataza kwa kisheria na kimwongozo na anamuhadharisha na kumtolea viaga. Atakapohalifu atamwadhibu siku ya malipo iliyo kubwa.
Kama angelitaka kumzuwia angelifanya, lakini anaacha mambo yapite kwa sababu zake na desturi zake.

Huenda ikawa huu ndio mwelekeo wa kumnasibishia Mwenyezi Mungu ufalme kwa jumla. Kwa hivyo yanakuwa maana. "humpa ufalme wake amtakaye" ni kwamba Mwenyezi Mungu lau angelitaka kuuzuwia kwa nguvu ufalme kwa asiyeustahiki, angelizuwia na wala asingelifikia kwenye ufalme mtu dhalimu pamoja na kuwepo sababu zake za kikawaida.

Vyovyote iwavyo utajiri wa mtu na ufalme wake unakuja kutokana na natija yakijamii anayoishi. Ama kuunasibisha na matakwa ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya sababu yoyote ni makosa kabisa.

Na Mtume wao akawaambia: Hakika alama ya ufalme wake ni kuwa- jia lile sanduku.

Sanduku hilo lilikuwa la Musa alilokuwa akiwekea Taurat. Mwenyezi Mungu alikuwa amelipaza mbinguni baada ya kufa Musa kwa kuwakasirikia Mayahudi kama ilivyosemwa.

Ambalo mna ndani kitulizo.

Yaani kitulizo cha nyoyo zenu ambapo sanduku lilikuwa na jambo tuku- fu la kidini kwa Wana wa Israil.

Na mabaki ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na wa Harun.

Mwenyezi Mungu hakubainisha ni mabaki gani hayo. Watu wa Musa na wa Harun ni Mitume ambao walilirithi sanduku hilo.

Wakilibeba Malaika.

Yaani kwa miujiza. Basi Talut alipoondoka na jeshi, alisema: Mwenyezi Mungu atawafanyia mtihani kwa mto, basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka fumba kwa mkono wake.

Imepokewa kwamba Talut aliwaambia Waisrail: "Asitoke na mimi kwenye jihadi mzee, mgonjwa, aliyejenga jengo ambalo hajalimaliza, mwenye kushughulishwa na biashara, au mume aliyeoa mke ambaye hajamwingilia." wakakusanyika jamaa wenye sifa zinazotakiwa, na ulikuwa ni wakati wa kiangazi na joto kali, wakafuata njia isiyokuwa na maji. Walipolalamikia kiu, Talut aliwaambia: "Mwenyezi Mungu atawapa mtihani katika utii na uasi kwa mto mtakaoupitia. Atakaye kunywa katika mto huo si katika wafuasi wangu waumini, isipokuwa akinywa kidogo kiasi cha kiganja.

Wakanywa humo isipokuwa wachache miongoni mwao.

Inasemekana idadi ya waumini ilikuwa ni 313 kama idadi ya watu wa vita vya Badr. Hakika wema walikuwa na wanaendelea kuwa ni nadra sana kupatikana.

Basi alipovuka yeye na wale walioamini pamoja naye walisema: Leo hatumwezi Jalut na jeshi lake.

Aliendelea mbele Talut pamoja na wale waliomtii baada ya kuvuka mto mpaka wakakutana na Jalut na jeshi lake. Walipoona wingi wa adui yao, waligawanyika makundi mawili; kundi lilisema hatumwezi Jalut na kundi likasema:

Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira.

Ambao wamejizatiti kwa kupigana jihadi na kujitoa mhanga kwa ajili ya maisha mema yaliyo bora ambayo ni kuishi huru katika nchi iliyo huru na kujitosheleza kwa chakula na wataalamu katika nchi iliyoendelea. Ama kuvumilia udhalili na umasikini ni uchafu katika kazi ya shetani.
Na walipotoka kupambana na Jalut na jeshi lake walisema: Mola wetu, tumiminie subira na uithubutishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu makafiri.

Waumini walipojiona ni wachache na maadui zao ni wengi walikimbilia kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kuomba na kunyenyekea kwa ikhlas; na Mola wao akawatakabalia dua.

Na Daud akamuua Jalut. Na Mwenyezi Mungu akawapa ushindi waumini dhidi ya makafiri. Ikathibitika, kwa fadhila Zake na rehema Zake, dhana ya waliosema: "Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima na akamfundisha aliyoyataka.

Yaani Mwenyezi Mungu alimtawalisha Daud mahali pa Talut baada ya kufa kwake. Hekima ni ishara ya Zabur. Mwenyezi Mungu anasma: "...Na tukampa Daud Zabur." (4:163)

Na akamfundisha kutengeneza deraya (mavazi ya vita), Mwenyezi Mungu anasema: "Na tukamfundisha (Daud) kutengeneza mavazi kwa ajili yenu ili yawahifadhi katika mapigano yenu ..." (21:80)

Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwazuia watu baadhi yao kwa wengine ingaliharibika ardhi. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya viumbe vyote.

Yaani jamii yoyote ambayo ndani yake hamna utawala (serikali) basi itakuwa na vurugu. Na kwamba akili na sharia bila ya nguvu ya utekeleza- ji haiwezi kuleta amani na nidhamu. Imam Ali (a.s.) anasema "Mfalme ni msaidizi wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake... " Lakini mara ngapi wafalme wameiharibu ardhi na watu wake. Pamoja na hivyo, lakini hawa- tengenei watu wasiokuwa na mwendeshaji.

Hizo ni Aya ya Mwenyezi Mungu, tunakusomea kwa haki; na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.

Mwenyezi Mungu alimsomea Mtume wake Aya zake na Mtume akatu- somea ili tuzingatie hakika yake na tuzifanye ndizo desturi za vitendo vyetu vyote ili tuwe na maisha mema yenye utulivu. "Sema mimi nawaonya kwa wahyi na viziwi hawasikii mwito wanapoonywa." (21:45)

MWISHO WA JUZUU YA PILI